Tanapa yatakiwa kupitiwa upya tozo za viingilio katika hifadhi za Taifa

July 20, 2019 9:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hiyo inatokana na malalamiko kuwa tozo hizo zimekuwa zikidumaza utalii nje ya hifadhi za Taifa.
  • Pia imepunguza ajira na maendeleo ya baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi za Taifa. 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imetakiwa kupitia upya utekelezaji wa sheria ya tozo za viingilio kwa watalii ili kuhakikisha jamii zinazozunguka hifadhi za Taifa zinafaidika na ujio wa watalii katika maeneo yao. 

Kutokana na sheria hiyo maarufu kama ‘Single Entry’, watalii walio wengi hulazimika kukaa ndani ya Hifadhi hadi muda wa saa 24 bila kutoka katika hifadhi ili kukwepa kulipa gharama zaidi ya mara moja endapo watatoka nje ya hifadhi. 

Hali hiyo imekuwa ikiwanyima fursa watalii kuyafikia maeneo au vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kujionea bidhaa za utamaduni na kukutana na watu wa maeneo husika. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema mapitio hayo ya sheria yatawasaidia waongoza  watalii kutoka nje ya hifadhi na watalii wao kwa ajili kuzitembelea jamii zilizokaribu na hifadhi na hivyo kuzisaidia jamii kunufaika moja kwa moja kupitia utalii wa kiutamaduni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, maagizo hayo yametolewa na Kanyasu wakati alipokuwa akifunga maonyesho ya 8 ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti mkoani Mara.


Zinazohusiana:


Katika mapitio hayo, Kanyasu ameagiza Tanapa iangalie maeneo ambayo inadhani ni muhimu  kwa Single Entry iendelee kutumika  na iweke  mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa vidole (Biometric Identity) utakaoweza kutumika kubaini udanganyifu endapo utafanyika.

“Mfumo huo utawalazimisha watalii kuweka kidole wakati wakiwa wanaingia na wakati wanapotoka nje ya hifadhi,” inaeleza taarifa hiyo. 

Amesema tangu kuanzishwa kwa Single Entry kumesababisha kudumaa kwa shughuli za utalii katika baadhi ya maeneo yaliyopo karibu na Hifadhi za Taifa ukiwemo ukanda wa Magharibi katika geti la Ndabaka katika Hifadhi ya Serengeti na katika  Hifadhi ya Ruaha.

Maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na kuwepo kwa Single Entry ni yale maeneo ambayo hayajapitiwa na barabara kuu pamoja na viwanja vya ndege.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema kwa sehemu kubwa wilaya yake imezungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kutokana na uwepo wa Single entry wilaya hiyo imekosa watalii wanaotembelea vijijini tofauti na ilivyokuwa mwanzo kabla ya kuanzishwa.

“Mhe Waziri tunakuomba uliangalie suala hili, utalii wa kiutamaduni uliosaidia kuajiri wananchi wengi umekufa kutokana na Single Entry,” amesisitiza.

Enable Notifications OK No thanks