Shirika la ndege la Afrika Kusini kufungwa, wafanyakazi 4,700 kupoteza ajira

April 20, 2020 9:26 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kukosa fedha za kujiendesha na Serikali ya Afrika Kusini kukataa kulipiga jeki.
  • Wafanyakazi wote watalipwa fedha ya kukatisha mikataba kabla ya Aprili 30.
  • Janga la virusi vya Corona nalo lachangia kulimaliza shirika hilo.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) limetangaza uamuzi wa kuwafuta kazi watumishi wake wote 4,700 hadi ifikapo Aprili 30, 2020 baada ya kushindwa kujiendesha. 

Maamuzi hayo ni yamekuja baada ya shirika hilo kushindwa kuishawishi Serikali ya Afrika Kusini kulipatia bajeti kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake na hivyo kuamua kulifunga.

SAA lenye miaka 86 kwenye tasnia ya usafiri wa anga limesema lnatarajia kulipa wafanyakazi wake wote fedha na kuvunja mikataba kabla ya kufunga virago.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeeleza kuwa ili kulipa wadau wanaolidai shirika hilo, shirika hilo limesema litauza mali zake ili kupata fedha ya kumaliza madeni yake.

Hata hivyo, shirika hilo kuuza malizake siyo jambo geni kwani mapema Februari mwaka huu, lilitangaza kuuza sehemu mbili za kutua (night-time landing slots) kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow uliopo nchini Uingereza ili kujipatia fedha ya uendeshaji.


Zinazohusiana


Kuondolewa wafanyakazi wote ni hatua ya mwisho kufanywa na shirika hilo baada ya kufuta safari zake kwenye baadhi ya vituo vyake vya awali. 

Vituo hivyo ni pamoja na Hong Kong na Guangzhou nchini China, London Mashariki (Uingereza), Port Elizabeth, Durban (Afrika Kusini), Sao Paulo (Brazil), Entebbe (Uganda), Munich (Ujerumani), Luanda (Angola), Ndola (Zambia), na Abidjan nchini Ivory Coast February 29, mwaka huu.

Huenda janga la Corona ambalo limesitisha safari nyingi za ndege za abiria duniani, limechangia kulisambaratisha kabisa shirika hilo linalomilikiwa na Serikali ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), sekta ya usafiri wa anga inatarajiwa kupoteza Sh726.4 trilioni kwa mwaka huu kutokana na janga la Corona. 

Enable Notifications OK No thanks