Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’

Daniel Samson 0502Hrs   Agosti 27, 2018 Maoni & Uchambuzi
  • Ni fursa ya kufanya utalii, kuburudika na kujifunza mambo mbalimbali.
  • Unaepuka usumbufu wa kukaguliwa muda mrefu na kuachwa na ndege.
  • Fanya mawasiliano na shirika la ndege unalosafiria ili kufahamu muda muafaka wa kufika 'Airport'

Dar es Salaam. Umepata safari ya kusafiri kwa ndege, nyaraka zote za kusafiria na mizigo yako iko mahali pake, lakini unaweza kujiuliza ni mapema kiasi gani unatakiwa kuwahi uwanja wa ndege (Airport)? 

Kwa wanaotumia usafiri wa ndege mara kwa mara hili halina tatizo lakini kwa mtu anayesafiri kwa mara ya kwanza kuna mambo unatakiwa kuzingatia ili safari yako iwe ya mafanikio. 

Kwa mujibu wa taratibu za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es Salaam wasafiri wanashauriwa kufika saa tatu kabla ndege haijapaa ili kukamilisha taratibu za ukaguzi wa vitambulisho, nyaraka za kusafiria na mizigo. 

Lakini shirika la ndege la Fastjet linalofanya shughuli zake hapa nchini, linamtaka msafiri  kufika saa mbili au dakika 40  kabla ya ndege kuruka na atakayefika kwenye dawati la ukaguzi baada ya dakika 40 zilizowekwa hawezi kuruhusiwa kuingia ndani ya ndege na atalazimika kuahirisha safaria au akate tiketi nyingine.

Taratibu hizo hazitofautiani na zile za viwanja vya ndege vya kimataifa ambapo kwa wasafiri wanaoenda nje ya nchi wanashauriwa kufika saa tatu kabla na wasafiri wa ndani ya wanashauriwa kufika saa mbili kabla ya ndege kupaa.

Zipo sababu mbalimbali zinazowataka wasafiri wa ndege kuwahi katika viwanja vya ndege ikiwemo kuepuka usumbufu wa kuchelewa kukaguliwa hasa pale ambapo dawati la ukaguzi linakuwa na wasafiri wengi. Pia unahitaji muda wa kuhakikisha mizigo yako iko sawa na inakidhi vigezo vya usafirishaji na kufahamu vizuri mazingira ya  kiwanja cha ndege unachosafiria ili kuepuka usumbufu wa kuachwa na ndege.

“Fika mapema zaidi ili kuepuka usumbufu. Siyo vizuri kupata usumbufu kwa kila hatua unayoiendea ni vema ukaokoa dakika chache,” anasema Ben Schlappig, mwandishi wa blogu ya wasafiri ya One Mile at a Time


Zinazohusiana:


Muonekano wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na huduma mbalimbali zinazotolewa yakiwemo maduka na migahawa. Picha| Costruction Review Online.


Unatakiwa kufika mapema kiasi gani ‘Airport’?

Kwa wasafiri wa ndege zinazoruka nje ya nchi wanashauriwa kuwasiliana na mashirika ya ndege wanayosafiria ili kufahamu muda muafaka wa kufika uwanjani. Mchakato wa ukaguzi wa safari za nje ni mrefu kidogo kuliko ule wa ndege za ndani kwasababu unahusisha uhakiki wa pasi za kusafiria, visa, mizigo, uraia, vituo itakavyosimama ndege, sheria na kanuni ambazo msafiri anatakiwa azingatie kwenye nchi anayokwenda.

Mfano ndege za Uingereza na Marekani zinawataka wasafiri wa ndege za kimataifa kufika dakika 60 kabla ndege haijaruka lakini wanashauri kuwahi mapema zaidi ya saa 3 ya muda huo ili kukamilisha taratibu zote mapema na kuwa tayari kuingia kwenye ndege. 

Kwa wasafiri wa ndani,  muda mzuri wa kufika uwanjani ni saa mbili kabla ndege haijaruka, lakini kila shirika la ndege lina utaratibu wake. Ni muhimi kufuata muongozo wa ndege husika ili usipoteze nafasi ya kusafiri kisa tu umechelewa au haujazingatia taratibu za usalama kabla ya kusafiri.

Ikiwa utachelewa kufika mapema na kukuta muda wa ukaguzi umepita utalazimika kulipia ndege nyingine na unaweza kusafiri siku nyingine tofauti na uliyopanga kutegemeana na mpangilio wa safari za shirika husika la ndege.

Kwa mfano ukiwa unasafiri kutoka Anchorage, Los Angeles kwenda Miami ndani ya Marekani utalazimika kutumia dakika 30 kwa ajili ya ukaguzi wa begi au mizigo, kwa maana hiyo unatakiwa kufika uwanjani dakika 60 kabla ya ndege kuruka

 

Ufanye nini baada ya kufika mapema ‘Airport?

Ikiwa umefika mapema uwanja wa ndege na umefanikiwa kukamilisha taratibu zote za ukaguzi na una muda mwingi kabla hamjaanza safari, una mengi ya kufanya. 

Viwanja vingi vya ndege duniani vina maeneo maalum ya kupumzika na kupata burudani. Siyo tu vina intaneti ya bure kukuwezesha kuperuzi kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, tovuti na sehemu za kuchaji simu bali zina huduma zaidi ya hizo.

Unashauriwa kabla ya kusafiri kupitia tovuti za kiwanja cha ndege husika ili kufahamu huduma zinazotolewa. Kwa mfano JNIA una maduka na mgahawa unaoweza kupata huduma ya chakula na vinywaji.

Lakini kwa viwanja vya ndege vya kimataifa kama Singapore ambavyo vina eneo kubwa la uwekezaji vina huduma mbalimbali ambazo hazipatikani kwenye viwanja vingi vya nchi za Afrika.

“Kiwanja cha ndege cha Changi, Singapore kina bustani ya vipepeo, ukumbi wa sinema, mazoezi, bwawa la kuogelea na mambo mengi,” anasema Schlappig. Viwanja vya ndege kila siku vinabuni huduma muhimu kuwavutia wateja wake, “Saluni, maonyesho ya sanaa na mambo ya kale, matamasha na burudani mbalimbali.”

Kama unatazamia kutotumia fedha, kuna vitu vingi unaweza kufanya; kutembea ili kunyoosha miguu, kufurahia maonyesho ya sanaa, kutafakari na kusoma vitabu kwenye chumba cha mapumziko. 

“Viwanja vya ndege vinasonga mbele kuwapa wateja vitu wanavyotaka,” anasema Steve Mayers, Mkurugenzi wa huduma kwa wateja katika Uwanja wa ndege cha Hartsfield-Jackson,kilichopo Atlanta Marekani. Uwanja huo una hekali 30 za bustani yenye aina mbalimbali ya maua na wanyama, “Huo ndio mstakabali wa wasafiri.”

Bustani wanayotumia wasafiri kumpumzika wakati wakisubiri ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kmataifa wa Changi, Singapore. Picha| Born2Invest.

Related Post