Nini kinafuata baada ya Fastjet kusitisha safari zake?

December 18, 2018 9:50 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wachambuzi masuala ya usafiri wamesema hatua hiyo ni pigo kwa sekta ya usafiri wa anga  kwa sababu nchi inaweza kurudi katika enzi za shirika la ndege la Taifa kuhodhi biashara ya anga.
  • Hatua hiyo inawaweka njiapanda wafanyakazi wa kampuni hiyo ambayo imedumu soko kwa miaka sita sasa.
  • Wadau wa utalii wasema suala la Fastjet halitakuwa na athari kubwa katika sekta hiyo kwa sababu watalii hutumia ndege kubwa za kimataifa.
  • Mashirika mengine ya ndege yapewa changamoto ya kudhibiti mapato na gharama za uendeshaji.

Dar es Salaam. Kufuatia shirika la ndege la Fastjet Tanzania kutangaza kusitisha safari zake za mwezi huu na Januari 2019, wachambuzi wa masuala ya biashara na uchukuzi wameeleza kuwa hali hiyo inaweza kuleta mtikisiko katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo usafiri wa anga na utalii.

Fastjet jana (Desemba 17, 2018) ilieleza kwenye taarifa yake kwa umma kuwa wateja wake wote waliokata tiketi kwa ajili ya kusafiri kati ya Desemba 2018 na Januari mwakani watarudishiwa fedha zao na menejimenti ya Fastjet.

Uamuzi huo ulikuja muda mfupi baada ya  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA) kueleza kuwa shirika hilo limepoteza sifa ya kuendelea kutoa huduma ya usafiri na kulipa notisi ya siku 28 kushughulikia matatizo yake la sivyo litafutiwa leseni ya kuendesha biashara hiyo nchini.

Kwa mujibu wa TCAA, shirika hilo halina fedha za kujiendesha na limekiuka leseni ya usafiri wa anga kwa sababu halina ndege zozote kwa sasa.

Katika msimu huu wa sikukuu ambapo watu husafiri katika maeneo mbalimbali, shirika hilo limewaacha katika sintofahamu wengi waliokuwa wakitumia usafiri huo wa gharama nafuu katika mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro na Mwanza na baadhi ya nchi nyingine za Kusini mwa Afrika.

Tayari baadhi ya abiria wameanza kulalamika katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwa kueleza kuwa uamuzi huo umevuruga mipango yao lukuki hasa katika kipindi hiki cha sikukuu ambacho wengi hurudi makwao kupumzika kutoka katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha, na Mwanza.

Baadhi ya wachambuzi wameileza nukta.co.tz  kuwa hali hiyo inaweza kuwa na matokeo mchanganyiko katika sekta mbalimbali hasa ya usafiri, uchumi na shughuli za utalii. 


Biashara na usafiri wa anga

Kusitishwa kwa safari za Fastjet huenda ikiwa ni pigo kwa sekta ya usafiri wa anga ingawa upande wa pili maamuzi ya TCAA yamesaidia kuwaondolea usumbufu abiria wanaokata tiketi bila ya kusafiri. 

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Lugome amesema hatua hiyo inaweza kuathiri ushindani wa kibiashara na kuna uwezekano wa  kurejea katika  enzi za shirika la ndege la Taifa kuhodhi biashara ya anga na mwishowe na wenyewe kushindwa kumudu mahitaji ya wasafiri. 

“Lakini wale wachache watakaobaki kuendesha biashara hii watakuwa wanajiamulia muda na bei ilihali sasa hivi wateja walikuwa wanaamua kusafiri muda fulani na kwa gharama fulani kwa sababu tu wana uchaguzi mpana wa aina ya usafiri,” amesema Lugome ambaye ana uzoefu wa usafiri wa anga kwa muda mrefu sasa.

Tangu kuanzishwa kwa Fastjet Tanzania imekuwa ikitoa ushindani kwa mashirika mengine ya Air Tanzania na Precision Air hasa katika safari za ndani. 

Wachambuzi wengine wameiambia Nukta kuwa Fastjet imekuwa kichocheo kikubwa cha kufufuka kwa  Air Tanzania ambayo imeibuka kipindi ambacho shirika hilo limekuwa likifanya vizuri katika soko kwa sababu ni mshindani mkubwa na iwapo Air Tanzania litabaki peke yake kuna hatari ya kujisahau.

Mwenendo wa huo wa kusuasua wa Fastjet unawaweka njia panda wafanyakazi wa shirika hilo ambalo limedumu kwa miaka sita sasa.

Katika mkutano wake na wanahabari jana jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari aliitaka kampuni hiyo ya ndege kuwalipa wafanyakazi wake stahiki zao kikamilifu iwapo itashindwa kuendelea na biashara hiyo hapo baadaye.


Zinazohusiana: 


Kufa kufaana

Hata hivyo, kufa kufaana. Kusitishwa kwa muda kwa safari za Fastjeti ni fursa kwa Precision na Air Tanzania kujitanua katika maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa yanashikiliwa na Fastjet zikiwemo safari za Mwanza na Mbeya. 

 “Njia ya Mbeya ina tija sana na ndiyo maana umesikia jana Meneja wa Mawasiliano wa ATCL akisema kuwa wameongeza routes  (safari) za Mbeya na Mwanza. Kwa Kigoma, Air Tanzania tayari ina wateja wengi kwa siku nyingi ndiyo maana Fastjet nao walitaka wawe wanaenda na Kigoma,” amesema Lugome.


“Sekta ya utalii haitaathirika sana”

Baadhi ya wadau wa utalii nchini wameiambia Nukta kuwa uamuzi wa Fastjet kusitisha kwa muda safari zake huataathiri sana sekta hiyo kwa sababu watalii hutumia zaidi ndege kubwa zinazotoka nje ya nchi kuja nchini. 

“Unajua watalii hutumia zaidi ndege kubwa za kimataifa kuja nchini, kusitishwa kwa safari za Fastjet kutaathiri kidogo sana utalii kwa sababu haihusiki zaidi na kubeba watalii,” amesema  Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Utalii nchini (Tato), Wilbard Chambulo. 

Chambula amesema watalii hutumia ndege za kukodi na kwenda nazo kwenye vivutio vya utalii, jambo linalowahakikishia kuendelea na shughuli za utalii kwa sababu kuna njia nyingine mbadala ikiwemo usafiri wa magari na treni ambao utasaidia kupunguza gharama kubwa za kupanda ndege. 

Ripoti ya Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (2017) inaeleza kuwa mafanikio ya sekta ya utalii yanachagizwa na uwepo wa usafiri wa ndege, ambapo zaidi ya asilimia 54 ya watalii wa kimataifa wanasafiri kwa kutumia ndege. 

Kuhusu ‘anguko’ la Fastjest hasa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, Chambula amesema itakuwa ni manufaa kwa mashirika mengine kama Air Tanzania na  Precision Air ambayo yanaweza kutumia nafasi hiyo kupata wateja wengi na kuongeza mapato. 

Hata hivyo, bado mashirika hayo yametakiwa kujiimarisha zaidi kwa kuongeza idadi ya ndege na kuboresha huduma kwa wateja ili kuondoa usumbufu uliojitokeza kwa Fastjet kabla hawajachagua aina nyingine ya usafiri. 

“Cha msingi ni kuongeza safari hususani mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa ambayo ina ‘culture’ (tamaduni) ya watu kwenda kula sikukuu makwao. Fastjet ilikuwa na karibu safari tatu za Mwanza na mbili za Kilimanjaro na hapa unazungumzia abiria zaidi ya 1,600 kwa return kwa siku,” amesema Godfrey Boniventura ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi.

Katika taarifa yao ya Jumanne,  Fastjet ilieleza kuwa “wateja wote watarudishiwa fedha zao za nauli kwa utaratibu walionunua kuanzia Desemba 20 mwaka huu pia makampuni na mashirika mbalimbali ambayo yalikuwa yanafanya biashara na fastjet yawasiliane nasi kupitia barua pepe au maofisa husika, tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”

Msemaji wa Fastjet Lucy Mbogoro jana hakuwa tayari kuzungumzia kwa kina matatizo yanayoikumbuka kampuni hiyo kwa sasa.


‘Kilichoimaliza’ Fastjet na funzo kwa mashirika mengine

Inaelezwa kuwa mfumo wa kibiashara waliokuja nao Fastjet kwa mazingira ya Tanzania haukuwa rafiki kutoka mwanzo kwa sababu mazingira ya uendeshaji wa biashara ya usafiri wa anga kwa Afrika ni mgumu.

“Kuna tozo nyingi sana za Serikali na za uendeshaji. Na kama hujaziba mianya mingi na kuwa na mipango endelevu wa kuongeza wateja na kuwavutia waendelee kuzitumia huduma zako basi uwezekano wa kuporomoka ni mkubwa,” amesema Lugome.

Wakati mashirika mengine ya ndege yakifurahia fursa zilizoachwa na Fastjet kwa muda, Lugome amesema yanatakiwa kujipanga katika kudhibiti wa mapato ya mauzo ya tiketi na mengineyo na kudhibiti matumizi ili kupunguza gharama za uendeshaji

“Ilifika wakati ilikuwa si rahisi kuwa na uhakika wa safari za Fastjet kwa sababu walikuwa wanachelewa sana au kuaihirisha mno safari zao. Mashirika ya kimataifa yakazuia wafanyakazi wao kuitumia Fastjet kama “air transport vendor”. Hii ilikuwa pigo kwao,” amesema Lugome.

Kampuni ya Fastjet ilianza kupata changamoto za kifedha baada ya mmiliki wa awali Fastjet PLC aliyekuwa na asilimia 49 kujiondoa ambapo shirika hilo liliuzwa kwa wawekezaji wa ndani.

“Kuendesha kampuni ya ndege ni kazi sana, ni ‘business’ (biashara) inayohitaji pesa nyingi sana, sina hakika kama Mh. Masha (Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha) anayo hiyo pesa ya kufanyia hii business,” amesema mdau wa usafiri wa anga ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Licha ya Fastjet kusuasua, bado inaendelea kukumbukwa kutokana na mchango mkubwa ilioutoa katika kukuza sekta ya usafiri wa anga hasa katika kipindi ambacho Air Tanzania ilipokuwa ikikabiliwa na changamoto za kiuendeshaji.


Fastjet bado ni “rafiki wa walalahoi”

Boniventura anasema mfumo wa gharama ndogo za usafiri ulisaidia sana kuhamasisha wananchi kupanda ndege za kampuni hiyo na kuona umuhimu wa kutunza muda katika shughuli zao. 

“Kimsingi hamasa ya umuhimu wa usafiri wa ndege ulisababishwa na Fastjet,” amesema Boniventura.

Abiria wa Fastjet sasa watalazimika kutumia ndege za mashirika mengine kupata huduma za usafiri. Picha| The Citizen.

Mchango wa Fastjet katika usafiri anga Tanzania

Fasjet walikuwa na role (mchango) kubwa ya kuhamasisha usafiri wa anga nchini na kupanua sekta ya utalii na kuwaunganisha Watanzania na nchi jirani na rafiki za Zambia, Afrika ya Kusini na Msumbiji,” Lugome.  


Fastjet Tanzania imekuwa kwenye mpango wa kununua hisa zote ili imilikiwe na watanzania kwa asilimia 100 baada kampuni ya Fastjet PLC kutangaza kusitisha kutoa fedha kwa kampuni hiyo.

Mapema mwezi huu, baadhi ya vyombo vya habari Tanzania viliripoti kuwa waziri wa mambo ya ndani wa zamani, Lawrence Masha ameongeza umiliki katika kampuni hiyo hadi kufikia asilimia 68 kutoka asilimia nne za hapo awali. Umiliki huo wa zaidi ya theluthi mbili ya kampuni hiyo unamfanya awe mfanya maamuzi na Mwenyekiti Mtendaji.

Kampuni hiyo ya kimataifa inayosifika kwa utoaji wa huduma kwa gharama nafuu ukilinganisha na mashirika mengine ina makao yake Afrika Kusini na Uingereza. 

Imeandikwa na Zahara Tunda na Daniel Samson.

Enable Notifications OK No thanks