Serikali yajipanga kuongeza viwango vya ukusanyaji kodi Tanzania

Lucy Samson 0719Hrs   Februari 27, 2024 Biashara
  • Yataka kodi inayokusanywa ifikie asilimia 15 ya pato la Taifa.
  • Sababu za kutokulipa kodi zabainishwa.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania iko mbioni kutafuta suluhu itakayoongeza viwango vya ukusanyaji wa kodi hadi kufikia asilimia 15 ya pato la Taifa ili kuwezesha shughuli maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa muda wa zaidi ya miaka 10 tangu mwaka 2010/2011 hadi mwaka 2022/2023 viwango vya ukusanyaji kodi nchini Tanzania vimekuwa chini ya asilimia 12 ya pato la Taifa jambo linalotishia ukuaji wa uchumi.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango aliyekuwa anahutubia katika jukwaa la kodi na uwekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 27, 2024 amewaambia wahudhuriaji wa mkutano huo kuwa kushindwa kukusanya kiwango hicho kunarudisha nyuma shughuli za maendeleo nchini.

“Wawekezaji na wafanyabiashara wasipolipa kodi ipasavyo wanadhoofisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake kwa umma…hatuna budi kuibua mikakati itakayotufikisha kiwango cha kodi cha angalau asilimia 15 au zaidi,” amesema Dk. Mpango.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango Tanzania ina kazi kubwa ya kufanya kufikia kiwango cha ukusanyaji wa kodi angalau kinachoendana na nchi ambazo zipo katika kipato cha kati cha chini kama ilivyo Tanzania.

Nchi hizo ni pamoja na Senegal yenye asilimia 18.7 za ukusanyaji wa kodi, Zambia asilimia 16.8, Ghana 14.1 pamoja na Cameroon yenye asilimia 13.3.

Sababu za kutokulipa kodi zabainishwa 

Aidha, Dk. Mpango amebainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kiwango cha ukusanyaji wa kodi kushindwa kufikiwa ni kasumba iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya kudhani kuwa kodi ni kikwazo kwa wafanyabiashara nchini.

Hoja hiyo imetiliwa mkazo na Waziri wa Fedha  Dk. Mwigulu Nchemba ambaye amesema wakati mwingine wafanyabiashara husingizia ubovu wa mashine za kutoa risiti pamoja na changamoto za kimfumo.

“Jambo la mapato ni jambo la nchi yetu na ni jambo la maendeleo na siyo jambo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) peke yake,”amesema Nchemba.

Licha ya changamoto hizo Nchemba amesema wizara yake itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya ufanyaji wa biashara nchini.

Jukwaa la kodi na uwekezaji kutoa suluhu?

Ikiwa ni mara pili tangu jukwaa la kodi lianzishwe, wadau wa kodi, sekta ya fedha, biashara na uwekezaji wamebainisha kuwa na matarajio makubwa juu ya jukwaa hilo kutatua baadhi ya changamoto zinazozuia ukusanyaji wa kodi kusua sua nchini.

Raphael Maganga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (Tpsf) amesema wakati Serikali inatafuta suluhu ya kuongeza viwango vya ukusanyaji wa kodi nchini ni vyema ijikite katika kuvutia uwekezaji mpya.

Maganga amefafanua kuwa uwekezaji mpya utaihakikishia Serikali kodi upatikanaji wa vyanzo vipya vya kodi huku wakirekebisha sera mbalimbali za uwekezaji zenye migogoro.

“Ni muhimu kuvutia uwekezaji mpya nchini kwani ndio njia endelevu ya kuongeza kodi, uwekezaji huu utaongeza ajira na kuchangia kodi mbalimbali,” amesema Maganga.

Jukwaa la kodi kwa mwaka 2024 linafanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wadau watajadili mwenendo wa uchumi duniani pamoja na maeneo ya kimkakati katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2024/2025.

Related Post