Sera 4 kukuza uchumi, usawa Afrika

Sayuni Kisige 0915Hrs   Aprili 09, 2024 Biashara
  • Ni kupanua uwezo wa uzalishaji wa sekta binafsi.
  • Sekta za fedha zisielemee watu masikini. 

Dar es salaam. Benki Dunia imeweka wazi hatua nne za kisera zitakazosaidia kukuza uchumi wenye nguvu na usawa katika nchi za Afrika ikiwemo kuweka kipaumbele katika sera za mageuzi kushughulikia umaskini. 

Ripoti ya Afrika Pulse kuhusu kupunguza kukosekana kwa usawa katika uchumi na umaskini toleo la tisa iliyotolewa na benki hiyo Aprili 8, 2024 inaeleza kuwa upunguzaji wa umaskini na tofauti za kiuchumi barani Africa hautafikiwa kwa kasi kupitia sera ya fedha pekee.

“Inahitaji kuungwa mkono na sera zinazopanua uwezo wa uzalishaji wa sekta binafsi ili kuunda ajira nyingi na bora kwa makundi yote ya jamii.

“Hatua kadhaa za kisera kama kurejesha uimara wa uchumi mkuu, kukuza uhamaji kati ya vizazi, kusaidia upatikanaji wa masoko pamoja na kuhakikisha kwamba sera za fedha hazielemei masikini zinahitajika,” imeeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, tofauti za kiuchumi katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara ikiwemo Tanzania zinatokana na kutofautiana kwa miundo ya ukuaji wa uchumi, masoko pamoja na shughuli za uzalishaji ambazo zimeathiri uchumi katika kanda hiyo.

“Kukosekana kwa usawa barani Afrika kwa kiasi kikubwa kunatokana na mazingira ambayo mtoto huzaliwa na kusisitizwa baadaye maishani ni vikwazo vya kushiriki kwa tija katika masoko na sera za fedha zinazorudi nyuma” amesema Gabriel Inchauste mwandishi mwenza wa ripoti ijayo ya Benki ya Dunia kama ilivyoelezwa kwenye ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia imeangazia uchumi wa Afrika unaotarajiwa kukua kwa asilimia 3.4 mwaka 2024 kutoka asilimia 2.6 ya mwaka 2023 na ifikapo 2025 uchumi utafikia asilimia 3.8.

“Licha ya ongezeko hilo, kasi ya upanuzi wa uchumi katika kanda inasalia chini ya kiwango cha ukuaji wa muongo uliopita (2000-2014) na haitoshi kuwa na athari kubwa katika kupunguza umaskini,” imeeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa ili nchi hizo zijikwamue katika janga la umaskini inatakiwa sera hizo nne zitiliwe mkazo kwa ufanisi zaidi kwa matokeo mazuri.

Related Post