Samsung yatambulisha simu yenye bei ya uchumi wa kati

Rodgers George 0930Hrs   Agosti 06, 2020 Teknolojia
  • Simu hiyo ni masahihisho ya Galaxy Fold ya mwaka 2019 iliyozinduliwa na kupata kasoro lukuki.
  • Galaxy Z Fold2 inaskrini yenye ukubwa wa inchi 7.6 ambayo ni kubwa kuliko zote kwenye matoleo ya Samsung Fold.
  • Gharama ya simu hiyo inatosha kulipia familia tatu bima ya afya ya juu kwa mwaka mzima.

Dar es Salaam. Kampuni inayotengeneza vifaa vya kielektroniki ya Samsung imetangaza toleo jipya la simu za muundo wa kukunja (fold) ambayo bei yake ya awali kwa sasa inakadiriwa kuwa takriban Sh4.6 milioni kabla ya kodi, takriban mara mbili ya wastani wa kipato cha Mtanzania.

Simu hiyo ya Samsung Galaxy Z Fold2 iliyotangazwa usiku wa kuamkia Agosti 6 kwa saa za Afrika Mashariki ni maboresho ya Galaxy Fold ambayo iliingia sokoni mwaka 2019 na kukabiliana na kasoro lukuki kiasi cha kuifanya kampuni kusitisha kwa muda usambazaji wake na kurejesha tena sokoni.

Licha ya simu ya Galaxy Z Fold2 kutokuwepo sokoni kwa sasa haya ndiyo Nukta Habari (www.nukta.co.tz) tunayoyahamu kwa sasa. 

Yanayoonekana kwa macho

Tofauti na mtangulizi wake aliyetamba mwaka jana, Galaxy Z Fold 2 itaingia sokoni ikiwa na ukubwa wa inchi 6.2 ikiwa imefungwa na ikifunguliwa, itampatia mtumiaji muonekano wa “Tablet” yenye ukubwa wa inchi 7.6. 

Galaxy Fold ya mwaka jana ina ukubwa wa inchi 4.6 ikiwa imefungwa na ikifunguliwa, ukubwa wake unafikia inchi 7.3. 

Maboresho yanayoonekana kwenye toleo la Galaxy Z Fold 2 ni baada ya baadhi ya wadau wa simu yake kulalamikia skrini ya mbele kuwa ndogo sana.

Meneja Masoko wa Samsung duniani Victor Delgado wakati akiitambulisha simu mpya alisema “baada ya kuzindia simu ya kwanza (Galaxy Fold) watumiaji walisema wanatumia skrini ya mbele kama waitumiavyo skrini kuu. Tulisikia na kulifanyia kazi.”

Simu hiyo inakadiriwa kuuzwa kwa Dola za Marekani 1,980 sawa na Sh4.6 milioni ambayo ni takriban mara mbili ya pato la mtu kwa mwaka nchini Tanzania. Picha| Samsung.

Baadhi ya wadau wa teknolojia waliisema Galaxy Fold kuwa na skrini ya plastiki ambayo haikuwa na mvuto kwa watumiaji wa simu janja makini.

Kati yao ni mdau wa YouTube anayechambua simu mbalimbali Marques Brownlee ambaye amesema kupitia video yake kwenye mtandao huo kuwa, endapo utatumia kucha na kuibonyeza kwa nguvu simu ya Galaxy Fold, unaweza kuharibu skrini.

Mbali zaidi, baadhi ya watu walionunua simu hiyo walijikuta wakiibandua plastiki hiyo wakijua imewekwa kama “Protector” ya kuilinda skrini ya simu hiyo.

Ilichofanya Samsung kwenye Galaxy Z Fold2 ni kuachana na skrini ya plastiki na kuweka kioo ambacho kwa mujibu wa kilichosemwa wakati wa utambulisho, “wembamba wake ni zaidi ya nywele ya binadamu.”

Galaxy Z Fold2 imeondoa kamera moja (ya mbele) iliyokuwa kwenye Galaxy Fold na kubakiza kamera tano. Kamera tatu zipo nyuma na mbili zinaonekana ukiifungua simu hiyo na tofauti na zile za Galaxy Fold, kamera za sasa zipo kwa mfumo wa duara dogo au kama Samsung inavyoliita, “punch hole”.

Yasiyoonekana kwa macho

Uwezo wa simu hiyo uhifadhi kumbukumbu umegawanywa kutoka gigabytes (GB) 512 tu iliyokuja na Galaxy Fold ya mwaka jana na kumpa mtumiaji uwezo wa kuchagua kati ya GB 512 na 256 za uwezo wa uhifadhi. Utofauti huo wa kuhifadhi taarifa hapana shaka utazitofautisha bei simu za aina hiyo.

Zaidi, Galaxy Z Fold2 inayotumia mtandao wa 5G ina uwezo wa uhifadhi wa Random access memory (RAM) sawa na Galaxy Fold ambazo zote zina GB12 ambayo inazifanya simu hizo kufaa kwa wadau wa filamu za mtandaoni na michezo ya video (video games).


Zinazohusiana


Bei yake ni ya kukata na shoka

Inakadiriwa na baadhi ya wachambuzi kuwa bei yake ya sasa ni sawa na takriban Sh4.6 milioni mara mbili ya pato la mtu kwa mwaka nchini Tanzania ambalo lilifikia Sh2.58 milioni mwaka 2019 kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Licha ya kuwa Samsung imetangaza ujio wa simu hiyo, kama ilivyo kuwa kitendawili cha lini itaingia sokoni rasmi, bei ya simu hiyo haijulikani.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa teknolojia wakiwemo Techradar, wanakadiria simu hiyo kuuzwa kwa Dola za Marekani 1,980 sawa na Sh4.6 milioni ambayo ni takriban mara mbili ya pato la mtu kwa mwaka nchini Tanzania lililofikia Sh2.58 milioni mwaka 2019 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha na Mipango. 

Hata hivyo, kwa sasa Samsung wamefungua madirisha kwa wale ambao wangependa kuweka oda ya simu hizo ili ziwafikie punde tu zinapotoka.

Kwa muonekano, Galaxy Z Fold2 inavutia muundo wake na kamera zake zinazofanana na zile za Samsung Galaxy Note 20 huku ikisemwa kuja kwa rangi mbili tu.

Delgado amesema, simu hiyo ipo kwa rangi zinazotikisa mwaka 2020 ambazo ni “Mystic Bronze” na “Mystic Black”.

Je, upo tayari kuungana na wadau wengine kwenye simu za kukunja?

Related Post