Unayotakiwa kufanya kurejesha furaha kazini

Rodgers George 0438Hrs   Oktoba 07, 2019 Kolamu
  • Weka mazingira ya kazi kuwa safi na salama wakati wote
  • Jitahidi kutofautisha maisha ya nyumbani na ofisini
  • Imarisha mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzako lakini usijaribu kubadilisha tabia zao binafsi.

Dar es Salaam. Kuna mambo mengi yanayoweza kukusababisha utafute sababu za kuacha kazi uliyonayo sasa  na kutafuta nyingine inayoweza kukamilisha furaha au malengo yako. 

Lakini kabla hujaanza kufikiria yote hayo, bado kazi uliyonayo inaweza kukupatia furaha unayoitaka.  

Kupitia dondoo hizi, unaweza kurudisha amani iliyopotea na hivyo kukufanya uwe na furaha kazini na kuongeza ufanisi wako katika kutekeleza majukumu yako ya kila siku:

Panga vizuri ofisi yako

Ofisi ya kazi yako ni eneo muhimu linalohitaji kuwa safi na lenye kuvutia. Wakati mwingine unakosa furaha kwa sababu mazingira unayofanyia kazi siyo salama na mazuri.

Una wajibu wa kupanga vizuri ofisi yako ili iwe na muonekano mzuri, utakaokufanya ufanye kazi zako kwa ufanisi wakati wote. 

Pangilia vizuri meza, viti na nyaraka zako. Pia hakikisha ofisi inaruhusu hewa safi kuingia wakati wote. Muonekano wa eneo la kufanyia kazi, una mchango mkubwa wa kukupatia au kuondoa furaha ukiwa kazini. 

Usijaribu kubadilisha tabia za wafanyakazi wenzako

Kila moja ana tabia yake ambayo kwa wengine inaweza kuwa sawa na wengine isiwe sawa. Ili, kuepuka purukushani na wafanyakazi wenzako, jitahidi kukimbilia kubadilisha tabia zao hasa pale wanapokuwa hawajaonyesha kuhitaji msaada wako.

Wasaidie kuhakikisha wanatimiza majukumu yao na acha maisha yao yawe jinsi wanavyotaka kama hayaingiliani na majukumu ya kazi zako. Picha| Mtandao

Unaweza kujaribu kuwashauri lakini siyo kuwalazimisha wabadilike. Wasaidie kuhakikisha wanatimiza majukumu yao na acha maisha yao yawe jinsi wanavyotaka kama hayaingiliani na majukumu ya kazi zako.

Tofautisha maisha yako binafsi na kazi

Kama ulivyoweza kutenganisha maisha ya ofisini na nyumbani, unatakiwa ufanye hivyo hivyo kuweka mbali maisha ya nyumbani kwako na ofisini.  

Jitahidi kutimiza majukumu yako yote ya nyumbani ili yasikusumbue ukiwa ofisini. Changamoto za nyumbani kwako zibaki nyumbani kwako. Kazi ndiyo inayokuingizia kipato cha kuendesha maisha, si vema ikatatizwa na changamoto za nyumbani. 


Zinazohusiana


Jipongeze pale unapofanya mambo mazuri

Unastahili kujipongeza pale unapokuwa umefanya jambo zuri na lenye kunufaisha wengine. Jipongeze kwa kwenda kula chakula cha jioni na wafanyakazi wenzako au hata kutazama filamu. 

Kusherehekea mafanikio yako ni jambo la busara lakini linakuwa zuri zaidi kama utajumuika na wenzako. Hii itakusaidia kujiona ni mshindi na mwenye furaha wakati wote. 

Hakikisha unatunza afya yako

Hata kama unafanya kazi, ni vyema kuhakikisha kuwa afya yako ni kipaumbele. Fahamu vema chakula chako kabla ya kula na epuka kujaribu vitu vipya bila tahadhari. 

Fanya mazoezi ili kuimarisha utendaji wa mwili na ubongo wako. Afya ni mtaji namba moja katika maisha yako. Fanya kazi katika muda unaoshauriwa na ukichoka pumzika. 

Wakati mwingine tunakosa furaha kwa sababu ya kufanya kazi muda mrefu bila kupumzika. Jenga mazoea ya kupima afya kila wakati.

Fahamu vema chakula chako kabla ya kula na epuka kujaribu vitu vipya bila tahadhari. Picha| Rodgers George

Kuwa na mtazamo chanya kila mara

Hauhitaji kujitesa kwa kufikiria mambo hasi kila mara. Jaribu kujiweka kwenye viatu vya mtu kabla ya kulaumu na jaribu kutafuta zuri hata katika baya ulilofanyiwa na mfanyakazi mwenzio.

Mfanyakazi mwenzako anaweza akawa amesahau kutimiza baadhi ya majukumu muhimu, hauna haja ya kumfokea kabla ya kujua sababu. Kwanza muulize sababu, pili mwache ajieleze na tatu chukua hatua ya kumkanya kama ni matokeo ya uzembe na kumshauri pale inapohitajika.

Lifanye eneo la kazi kama sehemu ya kujipatia furaha na amani daima. Wewe ndiye mwenye jukumu la kujipa furaha na siyo mtu mwingine. Jukumu namba moja uwapo kazini ni kuitafuta furaha yako mwenyewe. 

Kama umefanya kila jitihada kutafuta furaha kazini  na umeikosa, ufanye nini? Utafute kazi nyingine? Ni katika makala nyingine itakayokujia wiki ijayo. 

Related Post