Sababu za kufanya unachokifanya sasa

Rodgers George 0341Hrs   Machi 23, 2019 Maoni & Uchambuzi
  • Mafanikio ya chochote unachokifanya ili kukuletea tija katika maisha yanatagemea zaidi mapenzi uliyonayo juu ya kile unachoweka mkono wako kufanya.
  • Licha ya kuanzisha bidhaa au huduma bora waanzilishi wana sababu ya kujenga timu zao.

Ukosefu wa ajira, uthubutu na nia ya kuwa na biashara binafsi ni mambo kadhaa yanayochochea uanzishwaji wa kampuni zinazochipukia nyingi zinazoanzishwa na vikundi vya vijana nchini.

Malengo makuu ya kuanzishwa kwa kampuni hizo sehemu kubwa ni kujikwamua na hali ya kiuchumi na hata kusaidia jamii katika mambo mbalimbali. Mfano, kupitia teknolojia baadhi ya vijana wamebuni programu za simu ama kompyuta ambazo zinasaidia kujifunza kwa wanafunzi wa chekechea hadi elimu ya juu kama Ubongo Kids na zinginezo.

Kila mwanzilishi ana sababu za kuanzisha bidhaa au huduma. Hata hivyo, ni sababu gani hufanya vijana wengi kufanya shughuli za ujasiriamali wanazozifanya?

Mmoja kati ya wapiga picha maarufu nchini kutoka mradi wa kupiga picha wa K15 Photos, Emannuel Feruzi ameiambia www.nukta.co.tz kuwa licha ya kusomea masuala ya programu za kompyuta, amependelea zaidi kupiga picha kiubunifu na kuifanya kazi hiyo kuchukua takriban asilimia 80 ya shughuli zake.

Sababu kuu ya Feruzi kuanza kupiga picha miaka minane iliyopita ni kupenda kupiga picha za mtoto wake na baadaye aliifanya kazi ya kupiga picha kama biashara rasmi.

“Nilipenda kupiga picha za mwanangu na hadi sasa uhandisi ni kazi ninayoifanya mara moja moja,” amesema Feruzi licha ya ukweli kuwa uhandisi ni miongoni mwa dili zinazolipa kwa waliofanikiwa kupata kazi au miradi ya kufanya.

Kinachomfanya Feruzi aendelee kuishi kwenye kazi yake licha ya kuwepo na ushindani mkubwa ni mapenzi alionayo juu ya kazi yake huku akieleza kuwa kama pesa zikikuangusha au timu yako ikikuangusha ni upendo juu ya kazi yako tu ndio utakaobaki kuiendesha kazi hiyo.

“Nimeanguka nikaamka mara nyingi tuna pengine ni zaidi ya mtu yeyote. Upendo juu ya kazi yangu ndiyo uliofanya niendelee kuifanya,” amesema.

Wengi hufikiri kuwa kuanzisha kampuni ni rahisi lakini kuna jambo nyuma ya kuipenda kazi unayoifanya licha ya kuwa kila anayeanzisha kitu huwa ana mapenzi nacho.

Given amekuwa kijana mwenye ushawishi na kuwavutia vijana wengine ambao wamekuwa wanapenda ubunifu wa teknolojia. Picha| Given Edward

Mwasisi wa programu tumishi (Apps) zinazosaidia masuala ya elimu, “My elimu “ na “Mtabe” Given Edward (25) amesema msukumo juu ya mambo ya programu ulianza tangu akiwa mtoto na msukumo huo ulizidi kukua kadri alivyokua akiongeza miaka kwenye maisha yake. 

Kwake yeye kufanikiwa kwa shughuli zake ni kwa sababu ya kupangilia vizuri timu yake kuweka sawa mpango kazi wake na zaidi kuwa na uhakika wa bidhaa yake. 

Amesema wengi wanaoshindwa kuendeleza kampuni zao ni kwa sababu tofauti ikiwemo kushindwa kuelewa nini wanafanya. 


Ufanye nini basi ukitaka kuanzisha kampuni yako au biashara?

Kwa watu wote waliofanikiwa katika biashara zao watakubali ya kwamba kuanzisha biashara ni zaidi ya mtaji na pia ni zaidi ya mapenzi ya kazi hiyo. Yafuatayo ni makusanyo ya maswali ya kuzingatia pale unapohitaji kuanzisha biashara yako.

Dhamira yako ni nini?

Kwa mujibu wa Lucy Odiwa (35), ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya “Women Choice” inayotengeneza taulo za kike (pedi) na hata za watoto ambazo zinaweza kutumika kwa zaidi ya miaka miwili, mafanikio ya kazi yake yamefuatia dhamira aliyokuwa nayo ya kuhakikisha mtoto wa kike hakosi masomo pale anapokuwa kwenye siku zake.

“Sababu ya period (hedhi), niliwahi singizia naumwa ili nisiingie darasani. Historia hiyo ilikua ni msukumo wa mimi kutafuta mbadala wa pedi za kutumia mara moja,” amesema Odiwa.


Zinazohusiana: ‘Wiki ya Ubunifu’ inavyoangaziwa kuleta mabadiliko Tanzania

                         Matumizi ya simu za mkononi yazidi kuchangia maendeleo Tanzania



Unaelewa unachokifanya?

Watu wengi wanaanzisha biashara yeyote ama kampuni kwa kukurupuka. Wakipata mshawasha kidogo tu kwa kuwa wana pesa basi huamua kuanzisha kampuni bila kujua kiundani ni nini kampuni hiyo itafanya.

Mshairi mashuhuri nchini, Zuhura Seng’enge mbali ya kuigiza sauti kwenye matangazo mbalimbali ya biashara, amefanikiwa kutoa albamu mbili za mashahiri. 

Amesema bila kuelewa kitu unachofanya ni rahisi kukata tamaa pale majanga yanapokutokea.

“Mafanikio hayaji kirahisi na hivyo ni kusema kama hujui ulifanyalo nilazima utakata tamaa pale mambo yanaposhindwa kukaa sawa,” amesema Zuhura.

Meena Ally ni moja ya watangazaji wa vipindi vya redio aliyejipatia umaarufu kutokana na uwezo wake wa kutangaza vizuri katika kipindi cha Amplifaya. Picha| BBC


Unapenda unachokifanya?

Meena Ally ambaye ni mtangazaji wa kipindi maarufu cha Amplifaya kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM amesema bila kuipenda kazi yake asingeweza fika hapo alipo. 

Amesema “Kama hupendi unachokifanya huwezi fika uendako” kwa kuwa ni mengi yalimkatisha tamaa lakini kwa sababu alipenda kuwa mtangazaji ndio maana anashikilia nafasi aliyopo kwa sasa.

Hata hivyo, Mhadhiri wa masomo ya mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es salaam (TUDARCo) Richard Ngaiza amesema kuna mambo mengi sana ambayo yanaweza kumwezesha mtu kufikia lengo la kuanzisha kampuni.

Zaidi ya yote amesema ni muhimu kufanya utafiti kwa kuwa utamfanya mtu kufahamu kama kuanzisha kampuni au biashara hiyo kuna faida kwake au kukidhi mahitaji yaliyopo kwenye jamii inayomzunguka.

“Watu huanzisha kampuni wakitaka kupata faida na saa zingine ni kutoa huduma tu. Cha muhimu ni kufanya utafiti na maswali yote mtu aliyonayo ataweza kuyajibu,” amesema.

Hata hivyo, amesema sababu za kuanguka kwa kampuni nyingi zinazoanzishwa ni pamoja na kushindwa kufundisha timu nzima na kuwaelewesha kusudio la kampuni hiyo, kukosa fedha za uendeshaji na hata kukosa soko.

Ngaiza amesema masaibu yote hayawezi kumkuta mwanzilishi wa biashara kwa kuwa atakua ameshafanya utafiti na kujua hatma ya biashara ama kampuni hiyo.

Related Post