‘Wiki ya Ubunifu’ inavyoangaziwa kuleta mabadiliko Tanzania

Mwandishi Wetu 0238Hrs   Machi 19, 2019 Teknolojia
  • Itafanyika Machi 25-30, 2019 na huwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili hatua zilizopigwa katika kuendeleza ubunifu nchini.
  • Litakuwa jukwaa muhimu kuainisha sekta zilizoachwa nyuma katika ubunifu wa teknolojia.

Mara nyingi ubunifu hutafsiriwa kama matumizi ya njia bora kutatua changamoto mpya, changamoto ambazo tayari zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi bado, au changamoto zilizopo kwenye soko au jamii kwa kipindi fulani. 

Dhana hiyo hukamilika pale ambapo bidhaa, huduma, teknolojia  au njia nyingine yoyote inayoweza kutatua changamoto husika katika jamii haipatikani kirahisi.   

Ubunifu unapatikana katika sekta zote ambazo zinamuhusisha binadamu na shughuli za maendeleo. Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, vijana wengi wamekuwa wakijitokeza na kutumia uwezo na ubunifu wa teknolojia kutafuta suluhisho la changamoto zilizopo katika jamii inayowazunguka, lengo ikiwa kujipatia kipato na kujiajiri.

Kutokana na kuthamini ubunifu wa teknolojia, kila mwaka huandaliwa ‘Wiki Ya Ubunifu’ ambayo huwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili hatua zilizopigwa katika kuendeleza ubunifu nchini na maeneo yanahitaji msukumo wa kipekee wa matumizi ya teknolojia.

Wiki ya Ubunifu kwa mwaka huu itafanyika 25-30 Machi, 2019 katika jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ambapo litakuwa jukwaa maalum litakalowakutanisha wabunifu kuonyesha kazi zao na kutambuliwa rasmi kutokana na mchango wao kwenye jamii. 

Tukio hilo limeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Costech ambapo kampuni ya Nukta Africa itakuwa mmoja wa washiriki wakiongoza mada ya mchango wa vyombo vya habari kukuza ubunifu Tanzania.

Kwa kutambua umuhimu wa wiki hiyo, tunakuletea mfululizo wa makala zinazoangazia hali ya ubunifu, utendaji wa kampuni zinazochipukia (Startups) na mchango unaotolewa katika jamii ili kuboresha na kurahisisha maisha. 

Pia sekta zinazopaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo mzuri wa ubunifu nchini. 

Usikose kufuatilia mfululizo wa makala haya kuanzia Machi 19, 2019.

Related Post