Saadani: Mahali unapoweza kuwaona Simba, Twiga wakila upepo wa ‘beach’

Daniel Mwingira 0312Hrs   Agosti 04, 2018 Safari
  • Hifadhi ya Taifa inasifa ya pekee ya kuwa na mbuga ya wanyama inayopakana na bahari.
  • Mbali na kufaidi kutazama wanyamapori, watalii wanaotalii hifadhi hiyo wanaweza pia kuona maboma ya kale yaliyojengwa na Wajerumani.
  • Ni rahisi sana kufikika kwa wakazi wa Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro na Dodoma.

Iwapo upo jijini Dar es Salaam unahitaji kumpumzika baada ya kuchoshwa na mchakamchaka wa jiji, Hifadhi ya Saadani inaweza kuwa miongoni mwa maeneo ya karibu yanayoweza kukupa utulivu unaostahili. 

Licha ya ukweli kwamba huenda umewahi kusikia mengi ya kuvutia kuhusu hifadhi hiyo, kubwa kuliko yote na kivutio cha wengi ni upekee unaotokana na ufukwe wa Bahari ya Hindi kukutana na hifadhi hiyo Mashariki mwa Tanzania. Makutano hayo yanayoitwa kwa Kiingereza “Where the beach meets the bush” yanaifanya Saadani kuwa moja ya maajabu machache ulimwenguni. 

Upekee huo wa hifadhi kukutana na Bahari ya Hindi unawapa fursa adhimu watalii kuona makundi ya wanyamapori kama tembo, nyani, ngiri, simba, twiga, swala, fisi na hata chui wakiwa pembezoni mwa ufukwe. Wakati maeneo mengine kama Dar es Salaam ni kawaida kukutana na watu ‘beach” Saadani si ajabu pia ukamkuta Simba akiwa amejilaza ‘beach’ akila upepo mwanana. Wewe huenda ukawa miongoni mwa watu wanaoweza kufurahia kivutio hicho na kuwa chanzo cha picha za wanyama hao.

Mbali na wanyamapori, vivutio vingine unavyoweza kuviona vile vya kihistoria na utamaduni kama maboma ya mawe yaliyojengwa na wajerumani.

Sifa nyingine ndani ya hifadhi ni kitendo cha maji safi, maji yasiyo na chumvi kutoka Mto Wami unaotirirsha maji yake kwenda baharini hukutana na maji ya chumvi kutoka Bahari ya Hindi. Sehemu hiyo imevutia sio wanayama tu hata wageni wengi wa kitalii kushuhudia tukio hilo la kijiografia.

Hifadhi hiyo, inayopatikana katika mikoa miwili ya Pwani na Tanga, ina ukubwa wa kilomita za mraba 1,062.
Jina la  hifadhi hiyo lina uhusiano na waarabu waliokaa katika eneo hilo toka karne ya 19. Kwa mujibu wa S
hirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) jina halisi la hifadhi hiyo lilikitokana na kuwa kijiji cha wavuvi cha Utondwe na baadaye lilibadilishwa kuwa Saadani.

Tembo akiwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Ufukwe huo ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii katika hifadhi hiyo. Picha| Minna Expedition. 

Saadani haibaki tu na historia ya kutembelewa na wafanyabishara maarufu nyakati hizo kama  kama Johannes Rebman, El-Masoud, Ptolemy, na Richard Burton lakini  ilikuwa pia ni kiunganishi cha wafanyabiashara ikiwemo biashara haramu ya utumwa.

Ikiwa ni hifadhi ya 10 kwa ukubwa Tanzania kati ya hifadhi 16, Saadani  ilipandishwa hadhi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 kupitia Gazeti la Serikali namba 188 baada ya kuongezewa eneo la  msitu wa Zaraninge, Ranchi ya Mkwaja na Mto Wami.

Unafikaje Saadani?

Tofauti na hifadhi nyingine za Taifa kama Katavi au Ruaha, hifadhi ya Saadani inafikika kirahisi na wakati wote wa mwaka yaani ije mvua au lije jua. Hata hivyo, ili ufaidi vizuri ‘utamu’ wa hifadhi  inashauriwa upange safari yako kati ya Juni hadi Februari.

Saadani inaweza kuwa ni eneo rafiki zaidi la kumpumzika kwa wakazi wa Dar es salaam, Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma. Kutembelea huenda kusikugharimu sana mfuko wako kutokana na kuwa na gharama za chini za usafiri na kiingilio.

Tanapa inaeleza kuwa unaweza kuingia katika hifadhi hizo kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupitia Dar es Salaam hadi Chalinze  na baadaye kupitia Kijiji cha Mandera. Katika njia hiyo, utatakiwa kusafiri kwa kati ya saa mbili hadi tatu kutoka Mandera hadi katika geti la Mvave. Hata hivyo, wakazi wanaotokea Dar es Salaam wanaweza pia kufika kupitia njia ya Bagamoyo.

Kwa wanaotoka njia ya Tanga wanaweza kuingilia Tanga Mjni kupitia Mjini hadi geti la Mkwaja ambapo watahitajika kutumia barabara ya vumbi yenye urefu wa Kilomita 120 wakitumia wastani wa saa tatu hadi tano. Inashauriwa ufanye mawasiliano vyema na Tanapa au waongozaji wageni kabla ya kuanza safari kwa ajili ya muongozo. 


Unatakiwa kuvunja 'kibubu' kwa kiasi gani?

Kwa Mtanzania au mgeni kutoka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki utatozwa Sh5,000 kwa siku wakati mgeni kutoka nje ya jumuiya hutozwa Dola za Marekani 30 (Sh65,000). Watoto wa Kitanzania wenye miaka chini ya miaka mitano mpaka 15 hutozwa Sh2,000, wakati mwenye umri chini ya miaka mitano ni bure.

Ukiwa Saadani unaweza kufanya utalii kwa kutumia gari kuanzia saa 12.30 asubuhi mpaka saa 12.30 jioni.
Hata hivyo, siyo magari yote yanaweza kuingia huko kama Toyota Vitz ama Passo. Unahitaji gari imara na maalum lenye  nguvu na uwezo wa kuhimili mikiki ya porini licha ya njia za hifadhi hiyo kupitika kirahisi wakati wa kiangazi kuliko masika.

Matembezi ya saa tatu  ndani ya msitu pia ni aina ya utalii unaoweza kufanyika kuanzia saa 12.30 asubuhi hadi saa 4:00 na wakati wa jioni kuanzia saa 9.30 jioni hadi saa 12.30 jioni huku taarifa muhimu zikihitajika kutolewa hifadhini.

Mtalii pia anaweza kuvuka mto wami kwa kutumia boti ndani ya masaaa mawili kama sehemu ya utalii wake na kuijionea vivutio mbalimbali sambamba na beach nzuri ya Bahari ya Hindi.


Related Post