RC Makonda awatoa hofu walemavu waliokuwa wanasaidiwa na Mengi

May 2, 2019 2:53 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema Mungu atawainulia mtu mwingine ili yale mema waliyokuwa wanayapata kwa mfanyabiashara huyo waendelee kuyapata.
  • Mengi aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP,  amefariki dunia usiku wa kuamkia leo  akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
  • Amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuonyesha mshikamano na ushirikiano wakati wakisubiri ratiba ya mazishi.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewatoa hofu walemavu wote waliokuwa wanasaidiwa na mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia leo, kuwa Mungu atawainulia mtu mwingine wa kuwashika mkono. 

Mengi aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP,  amefariki dunia akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Makonda aliyekuwa akizungumza na Wanahabari leo (Aprili 2, 2019) wakati alipokwenda kutoa  pole kwa wafiwa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, amesema walemavu wote ambao walikuwa wanasaidiwa na Mengi, Mungu atawaunulia mtu mwingine ili yale mema waliyokuwa wanayapata waendelee kuyapata.

“Lakini nataka kuwahakikishia kuwa Mungu aliyemuinua Mzee Mengi atainua mtu mwingine wa kusisima na walemavu ili yale mambo mema mliyokuwa mnayapata muendelee kuyapata kwa sababu Mungu hawezi kuwaacha yatima, wajane na walemavu,” amesema Makonda.

Watu wenye Ulemavu waliohudhuria hafla ya utoaji tuzo ya I CAN pamoja na chakula cha mchana iliyoandaliwa na Taasisi ya Dkt. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha|Mtandao.

Amesema yeye na Mengi walikuwa na mipango ya kujenga kiwanda kwa ajili ya kuzalisha ajira kwa walemavu ambapo Mengi alikubali kutenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kutekeleza azma hiyo. 

“Niwaambie ndugu zangu walemavu katika ombi nililokuwa nimemwomba la kujenga kiwanda na akakubali kutenga zaidi ya Sh2 bilioni, najua huko waliko wana hofu matumaini ya ajira yamepotea,” amesema Makonda na kuwataka walemavu hao wasiwe na hofu yoyote. 

Kwa nyakati tofauti Mengi amekuwa akishiriki katika matukio ya walemavu ikiwemo kula nao chakula na kuwasaidia kwa mahitajai mbalimbali ili kuwawezesha kuwa sehemu ya jamii 

Disemba 7, 2018 Mengi kupitia taasisi yake inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu (Dk Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation) ilizindua tuzo za ‘I CAN’ yenye lengo la kuwaenzi na kuwapa motisha walemavu ya kujiona wanaweza. 

Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inatoa haki ya kushiriki na kushirikishwa kikamilifu kwa watu wenye ulemavu katika shughuli zote za kijamii.


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, Makonda amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kushikamana wakati taratibu za mazishi ya marehemu zikisubiriwa. 

“Tuunganike tuwe kitu kimoja, mambo mengine yote yanawezwa kusemwa au sababu zote zinaweza kusemwa lakini ratiba ya msiba na muda wa kukuita ukifika Mungu anakuita yeye. 

“Nieendelee kutoa pole na tuendelea kuwa na ushirikiano, familia itakapotupa ratiba ya kwamba anakuja lini mpendwa wetu basi nitawaomba tushiriki wote kwa pamoja,” amesema Makonda.

Enable Notifications OK No thanks