Mengi kuwekeza Sh68 bilioni uchimbaji wa mafuta, gesi Tanzania

Daniel Samson 0300Hrs   Disemba 11, 2018 Biashara
  • Uwekezaji huo unafanyika kwa kuingia ubia na kampuni ya Swala Oil and Gas Tanzania PLC ili kuendesha shughuli za uchimbaji mafuta nchini kuanzia mwaka ujao wa 2019.
  • Ikiwa makubaliano hayo yatafanikiwa, ETL itamiliki asilimia 46 ya hisa za kampuni ya Swala na kuwa mwanahisa mwenye sauti katika maamuzi ya kampuni hiyo.
  • Dk Mengi katika siku za hivi karibuni amefanikiwa kuingia makubaliano ya kuanzisha viwanda vya kuunganisha magari na kutengeneza simu za mkononi ambavyo vyote vitajengwa nchini.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Dk Reginald Mengi anakusudia kuwekeza Dola za Marekani milioni 30 (zaidi ya Sh68 bilioni) katika kampuni ya Mafuta na Gesi ya Swala ili kuendesha shughuli za uchimbaji mafuta kuanzia mwaka ujao wa 2019.

Taarifa iliyotolewa na Swala ya Desemba 10, 2018 inaeleza kuwa uwekezaji huo unafanyika kupitia kampuni ya Dk Mengi ya Energy Tanzania Limited (ETL) ambapo uwekezaji huo utajikita katika kuendeleza miradi ya awali ya vitalu vya uchimbaji mafuta nchini. 

Ikiwa makubaliano hayo yatafanikiwa, ETL itamiliki hisa za asilimia 46 za kampuni ya Swala na kuwa mwanahisa mwenye sauti katika maamuzi ya kampuni hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Swala, Dk David Ridge amesema katika taarifa hiyo kuwa ushirikiano wataoupata kutoka ETL utaisaidia kampuni yao kutatua changamoto za mahitaji ya nishati hasa wakati huu ambao Tanzania inakusudia kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. 

"Tunafurahi kupata uwekezaji wa uhakika kutoka Energy Tanzania Limited ambayo imekuwa mwanahisa tangu ilipoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE) miaka minne iliyopita. Dk Mengi amegundua sekta ya nishati kuwa ni muhimu kwasababu inatoa fursa kwa Watanzania, na Swala inajivunia kuichagua kama sehemu muhimu ya kuwekeza," amesema Dk Ridge.

Swala inasubiri kibali cha Serikali ili ianze shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta katika kitalu cha Kito-1 katika bahari ya Hindi mwaka 2019. Katika tathmini iliyofanyika hivi karibuni, kitalu hicho kinakadiriwa kuwa na mapipa milioni 185 ya mafuta yenye thamani ya zaidi Sh22.5 trilioni. 


Zinazohusiana: Maumivu: Bei ya mafuta zapaa


Swala imekuwa kampuni ya kwanza ya gesi na  mafuta kuorodheshwa katika soko la hisa katika ukanda wa Afrika Mashariki ikimilikiwa kwa sehemu kubwa na wazawa.  Kampuni hiyo inayofanya utafutaji wa mafuta mkoani Morogoro kilichopo inamiliki hisa za asilimia 7.93 katika kampuni ya Pan African Energy Corporation ya nchini Mauritania.

Wakati Swala ikitangaza kuingia makubaliano na ETL, hisa moja ya kampuni hiyo ilikuwa inauzwa Sh490 katika soko la hisa bei ambayo haikuwa na mabadiliko yeyote na ile ya Desemba 7, 2018. Kampuni hiyo inamiliki ya asilimia 75 mradi wa Kito uliopo katika wilaya za Kilosa na Kilombero na Kitalu D huko nchini Burundi.

Mengi ambaye anatambulika zaidi kama mjasiriamali wa kimataifa ni mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni dada ya IPP Group ambayo inasimamia kampuni zingine za IPP Media, vinywaji na uchimbaji madini. 

Hivi karibuni, mfanyabiashara huyo alisaini makubaliano na kampuni ya Youngsan ya Korea Kusini ya kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari kinachotarajiwa kujengwa Jijini Dar es Salaam ambapo uwekezaji huo utagharimu Sh22.5 bilioni na kuzalisha magari 1,000 kila mwaka chini ya kampuni ya IPP Automobile Company Limited. 

Pia Oktoba 30 mwaka huu, Dk Mengi kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia ya Touchmate kutoka nchini Dubai, alitambulisha rasmi ujio wa kampuni mpya ya IPP Touchmate ambayo itajikita katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki, ikiwemo simu za mikononi na kompyuta huku uwekezaji wake ukiwa zaidi ya Sh11 bilioni.

Related Post