Rais Magufuli, watanzania wamlilia Mengi

Mwandishi Wetu 0026Hrs   Mei 02, 2019 Habari
  • Amesema atamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa. 
  • Awatumia salamu za pole wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara kwa kumpoteza mfabiashara huyo.

Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha mfabiashara na mmiliki wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, Rais John Magufuli amesema amesikitishwa na kifo chake na atamkumbuka kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa. 

Mengi ambaye alizaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro  umauti umemkuta akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu usiku wa kumakia leo, vyombo vya habari alivyokuwa anamiliki vya runinga ya ITV, na Radio ONE vimethibitisha. 

Rais Magufuli ametoa masikitiko hayo katika ukurasa wake wa Twittiter ambapo amesema, “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na Rafiki yangu Dkt. Reginald Mengi. Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa ktk maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo ktk kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara.”

 

 

Mengi ambaye anatambulika zaidi kama mjasiriamali wa kimataifa ni mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni dada ya IPP Group ambayo inasimamia kampuni zingine za IPP Media, vinywaji na uchimbaji madini. 

Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Mengi alimfunza mengi siku za uhai wake ambapo alikuwa na sifa ya uongozi, urafiki na mzazi. 

"Umeacha alama kubwa! Nimejifunza mengi kwako, Rafiki, Mshikaji, Kiongozi na Mzazi! Ulinifundisha kuwa KUKATA TAMAA NI DHAMBI! {Msalimie Mzee Sitta, mkumbushe kile kikao chetu Cha mwisho nyumbani kwako Pumzika kwa Amani Dk R.A Mengi," inasomeka sehemu ya ukurasa wa Nape ambaye aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Naye Hashim Rwegasira amesema Mzee Mengi alikuwa mtu wa watu aliyewajali sana walemavu na watu wenye uhitaji mbalimbali. 

"Ni msiba mzito wenye majonzi Mzee Mengi alikuwa mtu wa watu mpenda maendeleo aliwajali walemavu maskini na watu wote kwa ujumla kulingana na uhitaji wao atakumbukwa daima kwa mchango wake katika taifa letu la Tanzania niseme tu sisi ni wa Mwenyezi Mungu na Hakika kwake tutarejea," ameandika Rwegasira katika ukurasa wake wa Twitter.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Patrick Ole Sosopi amesema kifo cha Mengi ni ni habari mbaya kwa Taifa tunazipata katika wakati ambao tunawahitaji watu wenye moyo kama yeye. 

"Kwa niaba ya @bavicha_taifa tunatoa pole nyingi Kwa familia na watendaji wote wa IPP," ameeleza Sosopi katika ukurasa wake wa Twitter.

Kutokana na umaarufu wake hasa katika uwekezaji, Mengi alipata fursa ya kufanya kazi na jumuiya za kimataifa duniani ambazo zina uhusiano wa karibu na Tanzania. 

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tamko kufuatia kifo hicho ambapo umeeleza kuwa umepokea kwa majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Mengi asubuhi ya leo kwa sababu ulifanya naye kazi hasa katika shughuli za kiuchumi. 

Related Post