Raphael Maganga: Mfanya usafi hadi mwakilishi wa baraza la biashara la Afrika Mashariki-Tanzania

September 9, 2020 9:31 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Mkurugenzi wa kampuni ya Rakestar Group na mwakilishi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) -Tanzania.
  • Wakati akiitwa Mkurugenzi leo, Maganga amewahi kufanya kazi za usafi wa vyoo na uwanja, kutunza wazee na kusambaza magazeti.
  • Ushauri wake kwa vijana ni kutokutaka vitu kwa pupa na kutokuchagua kazi zinazokuja mbele yao.

Dar es Salaam. Baadhi ya vijana wamekuwa wakitamani kupata mafanikio ya maisha kwa haraka bila kufahamu kuwa kila jambo huja kwa wakati wake na mambo makubwa huja hatua kwa hatua.

Hali hiyo huwafanya kutamani kazi nzuri na zinazolipa vizuri mara baada ya kuhitimu masomo yao ya elimu juu hasa zile za ofisini zinazoambatana na mishahara minono mwisho wa mwezi.

Hata hivyo, hali huwa tofauti pale ambapo matarajio yao yanaposhindwa kutimia na wengi hukata tamaa na kufikiri hawana maana tena ya kuishi maisha mazuri. 

Kitu ambacho hawafahamu ni kuwa safari ya mafanikio ni ndefu na inahitaji uvumilivu huku ukijiwekea malengo ya kufika kule unakotaka kufika. 

Huenda unayesoma makala haya ni mmoja wao. Leo fikra zako zinaweza kubadilishwa baada ya kumfahamu Raphael Maganga, kijana ambaye mwanzo wa mafanikio yake ulikuwa mdogo lakini sasa amefika pale alipowahi tazamia kufika. 

Maganga (34) ambaye ni mtaalam wa masuala fedha na uwekezaji,  ni mwakilishi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) Tanzania, ambalo limekuwa likiziunganisha nchi za Afrika Mashariki katika shughuli mbalimbali za kibiashara.

Kufikia nafasi hiyo ya uwakilishi, ilikuwa siyo ndoto ya siku moja, ni safari ndefu iliyomlazimu kufanya kazi zinazoonekana ni za hadhi ya chini na za watu walalahoi. 

Maganga akimwelezea aliyekuwa Makumu wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka kuhusu bidhaa ya umeme wakati wametembelea mojawapo ya kiwanda nchini China. Picha| Raphael Maganga.

Safari yake ya ajira ilianzia ughaibuni

Safari ya ajira kwa Maganga inaanzia mwaka 2008 akiwa nchini Australia wakati anachukua masomo yake ya fedha na uhasibu ya shahada ya kwanza.

Akiwa masomoni, Maganga alitamani kupata kazi ilhali alikuwa bado anasoma. Aliongea na baba yake mdogo aliyekuwa Marekani aliyemuunganisha na rafiki yake mmoja aliyekuwa Australia.

Maganga alikutanishwa na dada wa Kitanzania anayefahamika kama  Judy, ambaye alikuwa Australia kwa muda mrefu, na  kumueleza kuwa anahitaji kazi ya ziada atakayoifanya wakati hana vipindi vya darasani.

Baada ya siku chache bila hiana, Judy ambaye aligeuka kuwa familia pekee akiwa Australia alimtafuta akimjulisha kuwa kazi imepatikana.

“Nilishangaa ananionyesha kazi ya usafi. Ulikuwa uwanja wa mchezo wa Cricket (kriketi) wenye uwezo wa kubeba watu 100,000. Unaweza kufikiria hali ya uwanja unavyokuwa baada ya mechi,” anasema Maganga.

Pia alikuwa akisafisha hadi vyoo vya uwanja huo na kulipwa Dola za Australia 18 kwa saa moja sawa na Sh30,439 ambapo alitakiwa kufanya kazi hiyo saa tatu kwa siku na mara tatu kwa wiki.

Raphael Maganga wa tatu kutoka kushoto akiwa na baadhi ya marafiki zake nchini Australia mwaka 2009. Picha| Raphael Maganga.

Pesa hiyo unaweza kudhani ni nyingi ukilinganisha na matumizi ya Kitanzania, lakini ilikuwa ni fedha kwa ajili ya matumizi madogo madogo akiwa Chuo Kikuu cha Monash kilichopo Melbourne, Australia.

“Nilisema hivi shangazi yupo serious (makini) na maisha kweli? Sina shida hizo za kuanza kuosha choo lakini kwa kuwa nilimuomba nikaanza tu kuosha choo,” anasema Maganga wakati akiongea na Nukta (www.nukta.co.tz). 

“Nikajisemea kama kazi ni hii, itabidi niwe mfanyakazi bora, lakini huko mbeleni sitafanya kazi hii tena,” ameongeza Maganga ambaye alifanya kazi hiyo kuanzia jioni hadi saa sita usiku na kuingia darasani asubuhi.

Usafi wa uwanja na vyoo vyake ilikuwa ni kazi ambayo Maganga aliifanya kwa miezi mitatu na kisha alipata kazi nyingine ya kusambaza magazeti, kazi aliyoiona ni afadhali kuliko kusafisha vyoo japo ilihitaji kuamka mapema.

Baada ya miezi miwili ya kusambaza magazeti, Maganga alihamia kwenye kufanya kazi ya kufaya utafiti wa masoko.

“Kampuni inakuchukua uende ukafanya utafiti madukani au unanunua bidhaa unaijaribu na kuwapa mrejesho,” anasema kijana huyo ambaye hakufanya muda mrefu kazi hiyo na kuingia katika shughuli nyingine za kuuza umeme nyumba kwa nyumba na baadaye  kufanya kazi ya kijamii ya kulea wazee na watu wenye ulemavu.

“Nikaifanya hiyo kazi kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Takriban miaka mitatu. Ni kazi ambayo kwa kweli inahitaji moyo. Ilihitaji kuwaogesha, kuwavalisha, kuwalisha, kuwapikia na hata kufanya nao matembezi,” ameelezea Maganga ambaye amesema kazi hiyo ilikuwa ikimlipa vizuri. 

Maganga mbaye nyumbani alipata mahitaji yote ikiwemo fedha ya kujikimu na malazi anasema kwa kazi hiyo “nilijifunza kutokuchagua kazi. Ukiwa na shida na hata usipokuwa na shida ni muhimu sana vijana kujishughulisha.”


Soma zaidi


Kutoka chini, kwenda juu

Licha ya kuwa Maganga alikuwa akilipwa vyema kwa kutunza watu wenye ulemavu na wazee, bado hakukata tamaa taaluma yake kwani hata akiwa akiendelea na kazi na masomo yake, alikuwa akituma maombi ya kazi walau mara tatu kwa mwezi tangu Julai mwaka 2009.

Maganga amesema ilifikia kipindi, alikuwa amezoea kutopata kila kazi aliyoomba kiasi cha kutokuumizwa na barua pepe alizokuwa anapokea kuwa hajafanikipa kazi aliyoomba. .

 “Ugumu wake ulikuwa kwanza, sikuwa na ukazi wa kudumu Australia na pili sikuwa nimepata uzoefu katika sekta yangu,” anasema Maganga ambaye aliwahi kuomba hadi kazi ya mkurugenzi wa benki moja wapo nchini humo licha ya kuwa CV (wasifu) yake iliandikwa kazi alizofanya zikiwemo za kusafisha choo na kulea wazee ili tu kuwakera hao waliokuwa wanamkataa.

Tabia yake ya kuomba kazi ilizidi kumjenga mpaka pale alipofanikiwa kupata kazi ya kuwa mshauri wa masuala ya fedha na uchumi katika moja ya taasisi za uwekezaji nchini humo ya AMP Financial Institution ambayo aliipata baada ya kumaliza masomo yake mwaka 2012.

“Nilipopata ile kazi, mmoja ya wasaili aliniambia kuwa sababu iliyofanya niipate kazi ile ni walipoona nimelea watu walemavu na wazee hivyo inanifanya kuwa mtu ambaye ninauelewa wa watu na hivyo kuweza kuhudumia na kushauri watu,” anasema Maganga. 

“Sikutegemea!” ameeleza Maganga ambaye amesema ndipo hapo alipoamini kuwa kila kitu alichokifanya kilikuwa ni hatua kuelekea katika mafanikio ya ndoto zake licha ya kukataliwa kwenye kazi zaidi ya 100.

Maganga (Nyuma wa kwanza kulia)  akiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Peter Stoyanov ( Raisi mtaastafu wa Bulgaria kati ya1997 na 2002 wa nne kutoka kulia mbele) na Kalonzo Musyoka  (Makamu wa Rais wa Kenya kati ya 2008 na 2013 wa nne kutoka kushoto mbele) nchini China kutafuta wawekezaji kuwekeza Kenya na Tanzania. Picha| Raphael Maganga.

Akiwa Australia, Maganga alifanya kazi na AMP pamoja na kampuni ya Domain Wealth Services kama mshauri wa masuala ya uchumi na fedha kwa miaka miwili. 

Baadaye kazi hizo zilimkutanisha tena na Makamu wa Rais wa zamani wa nchini Kenya, Kalonzo Musyoka ambapo alifanya naye kazi kama mshauri wa masuala ya uwekezaji.

Kwa Maganga ambaye hakuwahi kutamani kuwa raia wa nchi yoyote zaidi ya Tanzania, wito wa kurudi nyumbani uliendelea kusikika kichwani mwake mara kwa mara ili kutoa mchango wake wa maendeleo.

Mwanzo Mgumu, uliopelekea Mafanikio

Wakati Maganga akifanya kazi na Musyoka nchini Kenya, alikuwa akichochea uwekezaji nchini humo ambapo alifanikiwa kuunganisha wawekezaji kutoka mataifa mbali mbali ya Asia na Ulaya na nchi hiyo.

Hata hivyo, kiu ya Maganga ilikuwa ni kuendeleza nchi yake na hivyo alikuwa akitafuta mianya ya kuunganisha wawekezaji na Tanzania licha ya kuwa ilimpa ugumu kwa sababu alikuwa hajuani na watu wengi wa  Tanzania. 

“Ilikuwa ni vigumu sana maana kwa miaka 20 sikuwa Tanzania ,yaani nimetoka mwaka Mkapa anaingia madarakani na nikarudi Raisi Kikwete anatoka madarakani,” anasema Maganga.

Maganga akiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali na sekta binafsi nchini Tanzania. Picha| Raphael Maganga.

Hata hivyo kutokana na kazi aliyoifanya nchini Kenya, ilimkutanisha na Watanzania wa wizara mbalimbali na hapo ndipo safari ya kurudi nchini Tanzania iliposhika kasi.

“Nilipoanza kufuatilia miradi ambayo wawekezaji waliweza kuwekeza Tanzania, Nilianza kufahamiana na watu na kupata watu wa kufanya nao kazi na ilipofikia mwaka 2016, nilirudi Tanzania rasmi,” anasema.

Aliporejea nchini aliungana na baadhi  ya watu aliowafahamu na kuanzisha kampuni ya Rakestar Group Limited inayotoa ushauri wa masuala  ya uwekezaji. 

Hata hivyo, kampuni hiyo haikufanya vizuri wakati huo kwa sababu Maganga na wenzie walikuwa bado ni wageni nchini mwao.

Mwaka 2019, kijana huyo mwenye uthubutu aliona fursa ya uwakilishi Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC). Maganga aliipata nafasi hiyo na ndiyo sababu ya kuwa hapo alipo leo.

Kama kijana, bado ana macho ya tai huku matazamio yake yakiwa ni kujinoa zaidi katika diplomasia ya kimataifa, fani ambayo tayari anaitumikia kwa sasa. 

Neno moja kwa vijana

“Ukipewa fursa na mtu na unaihitaji, usiikatae haijalishi ni ndogo au ni kubwa kiasi gani, muhimu ni kuwa malengo. Mtu anaweza kufanya kazi yoyote akifundishwa, kwahiyo haijalishi ni kazi ambayo haujawahi kuifanya, uwe tu na utayari wa kujifunza. ,” anaeleza Maganga.

Unataka kufanikiwa katika ndoto zako, heshimu mchakato!

Enable Notifications OK No thanks