Ujasiriamali: Abuni jukwaa la mtandaoni kurahisisha manunuzi Tanzania

September 3, 2020 1:07 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni jukwaa liitwalo “Nitume Kariakoo na kokote Dar” linalorahisisha shughuli za manunuzi jijini Dar es Salaam. 
  • Limebuniwa na binti ambaye hadi sasa ana timu ya watu nane wanaojifunza kupitia mfumo wake.
  • Ndoto ya binti huyo ni kuufanya mfumo wake kuwa moja ya kampuni kubwa nchini na duniani.

Dar es Salaam. Muamko wa vijana kujiajiri katika shughuli za ujasiriamali unazidi kupamba moto hasa wakati huo ambao wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira baada ya kuhitimu masomo yao.

Ukosefu huo wa ajira umeendelea kuwafanya wajasiriamali wengi kukuna vichwa kwa kuangazia ni jinsi gani wanaweza kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii kwa kutumia teknolojia rahisi inayoweza kuwakikishia kipato cha kujikimu kimaisha.

Otilia Mtitu ni miongoni mwa vijana wa Tanzania ambao wameamua kupambana na changamoto za ajira kwa kubuni huduma ya manunuzi ya bidhaa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoani. 

Huduma hiyo inaendeshwa na jukwaa la mtaoni la “Nitume Kariakoo na kokote Dar” inawasaidia watu ambao hawana muda wa kwenda kununua bidhaa katika soko la Kariakoo, kuzipata bidhaa hizo popote walipo nchini. 

“Unakuta kuna mtu anaishi Kigoma. Atoke huko aje Dar anunue mzigo arudi nao ni lazima atatumia gharama nyingi kuanzia nauli, malazi, chakula. Sisi tunarahisisha hilo kwa kumfanyia manunuzi,kumtumia ama kumpelekea mzigo wake naye atatulipa gharama za huduma,” anasema Otilia. 

Binti  huyo ambaye anajiita Machinga wa kidijitali amesema “Nitume Kariakoo na kokote Dar” inafanya kazi kama tinga tinga (Bulldozer) yaani akiwa na maana ya kuwa chochote unachohitaji ilimradi kipo jijini Dar es Salaam, kitanunuliwa na kufikishwa hadi kwenye mlango wako kwa gharama nafuu.

Kwa sasa anatumia mawasiliano ya simu na mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Instagram na Twitter kuwasiliana na wateja wake kuwafanyia manunuzi hayo. 

Otilia ameiambia Nukta kuwa kwa siku anaweza kupata oda hadi kumi japo kuna siku nyingine, siku inapita bila hata mlio wake kusikika. Picha| Otilia Mtitu.

Safari ya kuanzisha jukwaa hilo

Ni kawaida kwa wajasiriamali kupata mawazo ya biashara kwa kutumia muda mwingi kufikiri baada ya kuona wengine wanavyoendesha shughuli zao, lakini kwa Otilia ni tofauti kwani alifanya maombi kwa Mungu wake na ndiyo yalimsaidia kupata wazo lake. 

Licha ya kuwa hakuwa mgeni kwenye biashara, Otilia baada ya kufanya maombi kwa muda mrefu alijikuta “Nitume Kariakoo” ikiwa ni sauti inayojirudia kichwani mwake mara kwa mara. 

“Kabla ya hapo nilikuwa natengeneza mawigi na kuyauza. Kwa kuwa wigi moja lilitumia siku tatu kutengenezwa, mahitaji ya sokoni yalinizidi uwezo nikafunga biashara. 

“Baada ya wazo la “Nitume Kariakoo” kuniijia kichwani, nilishtuka usiku na kuandika “Nitume Kariakoo Coming Soon” kwenye WhatsApp Status na nikalala baada ya hapo nikaanza kulifanyia kazi,” anasema Otilia.

Otilia ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) anasema timu yake yenye watu wanne inatoa huduma tatu ambazo ni kufanya manunuzi, utafiti wa bidhaa na usambazaji kwenye mikoa zaidi ya sita Tanzania na Kenya. 

Binti huyo ameiambia Nukta kuwa, wateja wake wengi ni wajasiriamali ambao huagiza mzigo kwaajili ya kuuza na wengine ni watu binafsi wanaoagiza mahitaji ya nyumbani.

“Kwa siku unaweza usipate mteja hata mmoja lakini siku zingine unapata wateja watano, watatu hadi kumi. Siku zingine unapokea tu simu za watu wanakuulizia,” ameelezea Otilia.

Hadi sasa, Otilia ametoa nafasi kwa vijana nane kujifunza kupitia jukwaa la Nitume Kariakoo na kokote Dar. Picha| Otilia Mtitu.

Otilia anapataje “mpunga”?

Kama mjasiriamali yeyote, biashara hukua kwa kukuza mtaji na kupata faida ya biashara unayofanya. Otilia naye ametengeneza mfumo katika huduma yake ambao unamsaidia kujipatia kipato.

Binti huyo amesema, pale anapopata oda za mteja huenda kuzinunua kwa bei halisi ya dukani na kisha hutuma bidhaa kwa mteja aliyeagiza  akiambatanisha na risiti halisi ya manunuzi.

“Baada ya kunua mzigo, mimi nitamtoza mtu gharama za huduma ambapo kwa Dar es Salaa, kima cha chini ni Sh10,000 na kwa mkoani, kima cha chini ni Sh20,000,” anasema mwanadada huyo aliyeelezea bei inaweza kubadilika kulingana na gharama na uzito wa mzio pamoja na umbali wa usafirishaji.

Changamoto ni sehemu ya biashara

Mbali na kuanguka katika biashara zaidi ya mara moja, kwa binti Otilia hiyo haijawa sababu ya kuachana na biashara yake kwani kwake “biashara isiyo na changamoto siyo biashara”.

Otilia amesema, kwa biashara yake changamoto kubwa ni wateja kutokuamini ukweli wa biashara za mtandaoni.

Kwa kipindi chote cha biashara yake, ni mara nyingi amepokea simu za watu waliohitaji kununuliwa bidhaa jijini lakini changamoto hujitokeza kwa mteja kukataa kutuma fedha ya bidhaa kabla hajaipata.

“Kuna mteja wangu wa Kigoma alihitaji mzigo wa Sh500,000, ilipofikia hatua ya kuwa anatakiwa anitumie pesa, alisitia. Alilazimika kubadilisha mawazo na kununua mzigo wa Sh100,000,” anasema. 

Changamoto nyingine aliyosema binti huyo, ni pamoja na watu anaowafahamu kutumia jina la biashara yake katika kujinufaisha wao wenyewe.

“Unakuta unarafiki amekusaidia kuposti tangazo lako. Unakuja kushangaa kesho anakuulizia kitu fulani unanunulia wapi. Basi unamuelekeza tu anaenda,” ameelezea Otilia alieonyesha kutoridhishwa na tabia hiyo.


Zinazohusiana


Tutegemee nini mbeleni kutoka kwa Otilia na jukwaa lake?

Mbali na utofauti kati yake na huduma zingine zinazofanana na kile anachofanya, Otilia amesema ndoto yake ni kuiona “Nitume Kariakoo na kokote Dar” kuwa kampuni kubwa kama zilivyo DHL na Amazon.

Licha ya kuwa kwa sasa amesajili jina la biashara na kujipatia kitambulisho cha mjasiriamali, amesema yupo mbioni kutengeneza programu (app) itakayorahisisha ukusanyaji wa oda na mawasiliano na wateja wake. 

Anachokipigania Otilia, ni kuhakikisha kila mteja anapata kitu alichokiagiza kama matarajio yake.

“Nikiagizwa nyanya, napenda nimfikishie mteja nyanya na siyo uji wa nyanya,” ameeleza Otilia.

Binti huyo ni mfano kwa vijana kuongeza ubunifu kubuni katika shughuli wanazofanya ili kuwafikia watu wengi kwa kutumia simu za mkononi.

Enable Notifications OK No thanks