Rangi za maua na maana zake

September 25, 2020 3:36 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Maua ni njia mojawapo ya mawasiliano na kila rangi ya au hubeba ujumbe fulani kwa mtu anayepokea.
  • Rangi nyekundu huonyesha hisia za upendo na pia hutumika zaidi na wapendanao.
  • Kama una wivu au unahitaji kutoa onyo, ua la njano litafaa kufikisha ujumbe kwa muhusika.

Dar es Salaam. Sikuwahi kufikiria kuwa kila rangi ya ua ina maana yake. Binafsi nilijua ua lolote liwe jeupe, la njano, jekundu na hata dhambarau ni ishara ya upendo, thamani na njia ya kuonyesha hisia kwa mtu unayempatia.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, mtazamo wangu kuhusu rangi za maua haukua sahihi kwa sababu sikufahamu kuwa kila rangi ya au ina maana yake kila inapotumika.

Maua ni njia moja wapo ya mawasiliano na kila rangi ya au hubeba ujumbe fulani kwa mtu anayepokea.

Maua ninayozungumzia leo ni maua asilia ambayo hulimwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kupeana kama zawadi na mapambo. 

Rangi nyekundu ni ishara ya upendo na utamaduni huo umedumu vizazi na vizazi. Picha| Unsplash.

Hivyo basi, ili kuepuka kuwasiliana isivyo sahihi kwa kutumia maua, ni muhimu kufahamu rangi za maua zina maana gani kabla hujatumia katika shughuli mbalimbali:

Ua jekundu

Bila shaka una ufahamu juu ya rangi hiyo, kwa sababu ni maarufu kwa mtu aliyewahi kuwa katika mahusiano.

Kopa (alama ya umbo la moyo) jekundu, ua jekundu na zawadi nzuri yenye rangi nyekundu kwa umpendaye, ina maanisha kuwa unaonyesha upendo wako. Kama umewahi kushiriki katika sikukuu ya wapendanao (Valentine’s Day), unaelewa lugha ninayozungumza.

Muuzaji wa maua eneo la Mbuyuni jijini Dar es,  Ramadhan Bunga ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa rangi nyekundu ni ishara ya upendo na utamaduni huo umedumu vizazi na vizazi.

Ua lenye rangi nyeupe

Maua yaliyo na rangi hii yana maanisha amani. Bunga amesema ndio sababu inayosababisha ua hili kutumika katika misiba  ili kuwafariji wafiwa. 

Mtaalamu huyo wa maua amesema maua yenye rangi hiyo, pia yanafaa kuwapelekea wagonja walio hospitalini na hata marafiki au ndugu.

Pia, ua lenye rangi hii huonyesha hali ya utulivu pamoja na utu.

“Endapo umesingiziwa kosa na umpendaye, unaweza kumpelekea ua lenye rangi hii kumuonyesha kuwa hauna hatia,” amesema Bunga.

Ua la pinki ni ishara ya kuwa unamthamini, ishara ya kushukuru na kumuomba akuamini. Picha| IMGBIN.

Ua la pinki

Ua hili limelenga zaidi jinsia ya kike na hata jamii imeamua kuitenga rangi hii kwa ajili ya wanawake, japo wapo wanaume ambao wanavutiwa na rangi hiyo. 

Unapompelekea mpenzi wako ua la pinki ni ishara ya kuwa unamthamini, ishara ya kushukuru na kumuomba akuamini.

Muuzaji wa maua wa duka la Haika Florist lillilopo Mbuyuni Jijini Dar es Salaam , Haika Kimaro amesema ua lenye rangi hii halina msimu kama ua jekundu ambalo linauzwa zaidi msimu wa sikukuu ya wapendanao inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka.

“Ni rafiki tu au kuna mengine? Chukua hili hapa,” amesema Kimaro ambaye alifungasha waridi lenye rangi ya pinki baada ya kumwambia nahitaji ua moja kwa ajili ya rafiki yangu wa kike.

Ua la njano

Kwa mujibu wa wataalam wa maua, rangi hii inaashiria wivu pamoja na onyo. Mbali na Bunga aliyetaja maana hizo, tovuti ya globalrose.com imeelezea kuwa rangi ya ua la njano inaweza kutumika kuonyesha furaha, urafiki pamoja na kuonyesha kuwa unajali.

Tovuti hiyo pia inaeleza kuwa ua hilo lenye rangi ya jua linaweza kutumika kumkaribisha mtu pale anapotoka safarini na kumsisitiza mtu akukumbuke pale anaposafiri na hata kumtakia mtu bahati nzuri.

Ua lenye rangi ya machungwa

Tovuti hiyo inayosaidia kufahamu maana ya rangi za maua, inaeleza kuwa rangi ya machungwa ni ishara ya hamu na shauku huku  fiftyflowers.com inaobainisha kuwa endapo unafurahia mafanikio ya ndugu, jamaa na rafiki, maua yenye rangi ya machungwa ndiyo yanafaa kumpatia.


Soma zaidi


Elimu ya nyongeza

Mawasiliano kwa njia ya maua ni mapana sana na kwa baadhi ya nyakati, watu hutumia maua mchanganyiko kuwasiliana.

Katika mchanganyiko wowote wa maua yenye rangi zaidi ya moja, ua lililochukua nafasi zaidi ndiyo linabeba maana ya ua zima huku mengine yakiwa ni ya kuongezea maana.

Mfano kwa kifurushi cha ua chenye maua mengi ya njano na machache mekundu, Bunga amesema hiyo ni sentesi iliyotimilika yenye maana ya “nakupa onyo la mwisho lakini nakupenda.” 

Tovuti ya fityflowers.com pia imeonyesha kuwa mchanganyiko wa maua meupe na mekundu ni kiashiria cha muunganiko na ndiyo maana hutumiwa zaidi na wana ndoa.

Namini hautapata tabu ya kuchagua maua yanayokufaa kwa ajili ya shughuli yako au kumpelekea yule umpendaye ili kudumisha mahusiano, urafiki na undugu. 

Enable Notifications OK No thanks