Fursa uzalishaji wa maua Tanzania

Daniel Samson 0201Hrs   Septemba 16, 2020 Ripoti Maalum
  • Uzalishaji bado uko chini licha ya mahitaji yake kuongezeka kila siku.
  • Serikali yasema itahamasisha ushirika katika zao hilo ili kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima.

Dar es Salaam. Licha ya uzalishaji wa maua kuongezeka kila mwaka nchini Tanzania, bado uzalishaji wake ni mdogo ikilinganishwa na mazao mengine ya bustani, jambo linalowafanya wakulima wapishane na fursa lukuki za zao hilo ikiwemo masoko ya kimataifa. 

Mazao ya bustani hujumuisha maua, mboga, viungo na matunda ambayo hutumiwa kwa matumizi mbalimbali ya binadamu na uzalishaji viwandani. 

Takwimu za Wizara ya Kilimo za mwaka 2020, zinaeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2018/19 uzalishaji wa maua ya asili ulifikia tani 13,240 kutoka tani 11,615 mwaka 2017/18.

Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 4.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

“Ongezeko hilo, lilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hayo kwenye vitalu nyumba (Green house) katika maeneo mbalimbali,” ameeleza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/21. 

Licha ya kuwa uzalishaji wa maua unaongezeka Tanzania, lakini kasi yake ni ndogo ikilinganishwa na mazao mengine ya bustani yakiwemo matunda.

Mathalan, mwaka 2018/19 zilizalishwa tani milioni 4.5 za matunda ikiwa ni zaidi ya mara 327 ya uzalishaji wa maua mwaka huo. 

Matunda yamechangia kwa sehemu kubwa kuongezeka kwa uzalishaji wa jumla wa mazao ya bustani kutoka tani milioni 5.9 mwaka 2015/2016 hadi tani milioni 6.5 mwaka 2018/2019. 

Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hayo, thamani ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwemo mboga na maua nje ya nchi imeongezeka toka Dola za Marekani milioni 412 (Sh955.7 bilioni) mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 (Sh1.8 trilioni) mwaka 2018/19 na kuifanya tasnia ya mazao ya bustani kuchangia asilimia 38 ya fedha za kigeni zinazotokana na sekta ya kilimo.

Hata hivyo, wakulima hasa vijana wana nafasi ya kuongeza uzalishaji wa maua ili kufaidika na soko la ndani na kimataifa hasa katika nchi za Ulaya ambazo zina watumiaji wengi. 

Maua hutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kutengeneza dawa, manukato, mapambo ya nyumbani na kupeana zawadi kwa wapendanao. 

Zao hilo la biashara hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na  Njombe na linaweza kulimwa nyumbani ikiwa kuna usimamizi mzuri. 

Baadhi ya mashamba makubwa ya maua yaliyopo Arusha ni pamoja na Arusha Blooms Ltd, Kili Flowers, Kombe Roses, Shilla Flowers, Allua Flowers, Finlays na Flamingo ambayo yanamilikiwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. 


Soma zaidi:


Waziri Hasunga amesema katika hotuba hiyo kuwa ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya bustani ikiwemo maua, wizara yake itahamasisha uanzishwaji wa ushirika katika mazao hayo ili kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo ugani, pembejeo, mitaji, teknolojia bora za kupunguza upotevu baada ya kuvuna na kuwaunganisha wakulima na masoko.

Pia wizara hiyo itasimika miundombinu ya kuhifadhi bidhaa za mazao ya 117 bustani katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe ili kurahisisha usafirishaji wa mazao hayo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini

“Hatua hii itawezesha mazao ya bustani kushindana katika masoko ya kimataifa, kumnufaisha mkulima na kuongeza mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi,” amesema waziri huyo. 

Una mpango wa kuwekeza katika kilimo cha maua Tanzania, endelea kufuatilia tovuti hii ya habari (www.nukta.co.tz) kufahamu kwa undani soko, watumiaji wa maua na mambo mtambuka kuhusu zao hilo duniani.

Pia tutaangazia mitazamo ya wanawake na wanaume kuhusu maua yanavyotumika kudumisha mahusiano ya familia na jamii. 

Related Post