Nje, ndani: Rais Samia afanya mabadiliko makubwa wakuu wa mikoa Tanzania

May 15, 2021 1:43 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Awaingiza wakuu wa mikoa 10 wapya. 
  • 10 waondolewa katika nafasi zao baada ya kustaafu na kupangiwa majukumu mengine.  
  • Mikoa ya Kigoma na Njombe haijaguswa na mabadiliko hayo. 

Dar es Salaam. Usiku wa leo huenda ukawa wa tabasamu au maumivu kwa baadhi ya watu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko makubwa ya wakuu wa mikoa Tanzania Bara huku baadhi wakibadilishiwa vituo, wakiondolewa na kuingiza wapya akiwemo David Kafulila. 

Mabadiliko hayo yametangazwa leo Mei 15, 2021 katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ambapo wateule hao wataapishwa wiki ijayo Mei 18 Ikulu jijini Dar es Salaam. 

Rais Samia amemteua Kafulila ambaye aliwahi kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe wakati wa uongozi wa Hayati Rais John Magufuli kuwa Mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya Idd Kimanta aliyestaafu.

Kafulila aliwahi kuwa mwanachama wa Chama NCCR-Mageuzi na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kutimkia CCM. 

Rais Samia pia amemteua mjumbe Kamati Kuu ya CCM, Makongoro Nyerere kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Joseph Mkirikiti aliyehamishiwa Rukwa kuchukua nafasi ya Joachim Wangabo aliyestaafu.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amehamishiwa Dodoma kuchukua nafasi ya Dk Binilith Mahenge aliyehamishiwa Mkoa wa Singida kuchukua nafasi ya Dk Rehema Nchimbi ambaye kwa mujibu wa taarifa ya Msigwa amestaafu.

Kwa sasa Mkoa wa Simiyu utaongozwa na John Mongella ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Mkoa wa Mbeya utaongozwa na Juma Homera ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mwanamvua Mrindoko. 

“Amemteua Zainab Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Kabla ya uteuzi huo, Telack alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na anachukua nafasi ya Godfrey Zambi ambaye amestaafu,” imeeleza taarifa hiyo.

Baada ya Telack kwenda Lindi, Shinyanga itakuwa chini ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati ambapo nafsi yake imechukuliwa na Ali Hapi.

Queen Sendiga ambaye aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 kwa tiketi ya chama cha ADC anaenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Hapi. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Baraza la Eid ElFitr ambalo Kitaifa limefanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam Mei 14, 2021. Picha| Ikulu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella amehamishiwa Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Loata Ole Sanare ambaye amemaliza muda wake huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam  Malima amehamishiwa Mkoa wa Tanga.

Mara kwa sasa itaongozwa na Robert Gabriel akitokea Mkoa wa Geita ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rosemary Senyamule. 

Mabadiliko yatikisa mpaka Dar

Katika uteuzi huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na Watanzania baada ya Rais Samia kuapishwa Machi 19 ili kupanga safu yake mpya ya uongozi, amemuhamisha kituo Aboubakar Kunenge aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Pwani kuchukua nafasi ya Evarist Ndikilo aliyestaafu.

Kunenge aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Julai 2020 na Hayati Rais Magufuli akichukua nafasi ya Paul Makonda aliyekwenda kugombea nafasi ya Ubunge wa jimbo la Kigamboni ndani ya CCM.

Hata hivyo, Makonda hakufanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera katika jimbo hilo kupitia CCM na badala yake aliteuliwa Dk Faustine Ndungulile ambaye ni Mbunge na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam ambao ni kitovu cha shughuli za biashara nchini Tanzania utaongozwa na Amos Makalla.

Makalla ambaye amewahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro, ni kama ana bahati kwa sababu amerudishwa tena katika mkoa huo uliopo mashariki mwa Tanzania. 


Soma zaidi:


Brigedia Jenerali Charles Mbuge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya Meja Jenerali Marco Gaguti.

Meja Gaguti amehamishiwa Mtwara akichukua nafasi ya Gelasius Byakanwa ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Aliyekuwa Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya Anna Mghwira ambaye alikuwa akiongoza mkoa huo kustaafu.

Mabadiliko zaidi

Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akichukua nafasi ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM.

Kabla ya uteuzi huo, Brigedia Jenerali Ibuge alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Omary Mgumba aliyewahi kuwa Mbunge wa Morogoro Kusini na Naibu Waziri wa Kilimo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela aliyestaafu. 

 

Mikoa ambayo haijaguswa

Wakuu wa Mikoa waliobaki katika maeneo zao ni Thobias Andengenye (Kigoma) na  Marwa Rubirya ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Enable Notifications OK No thanks