Namna unavyoweza kuepuka corona ukiwa saluni
- Hakikisha mhudumu na mteja mmevaa barakoa.
- Saluni zisijaze wateja kupindukia, mteja mmoja au wawili tu kwa wakati mmoja.
- Hakikisha unanawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kila mara.
- Vifaa vya saluni vitakaswe mara kwa mara kuua virusi hivyo.
Dar es Salaam. Hapana shaka kuwa ni jambo gumu kutekeleza ushauri wa kukaa zaidi ya mita moja ili kuepuka kupata virusi vya ugonjwa wa corona (COVID-19) iwapo unapatiwa huduma ya kutengenezwa nywele saluni.
Kwa vyovyote vile kinyozi au msusi lazima akusogelee ili akuhudumie vema bila kuharibu nywele zako.
Kutokana na sifa hizo, saluni zimekuwa ni moja ya maeneo yaliyowekwa kwenye kanda nyekundu yenye uwezekano mkubwa wa kusambaza virusi vya corona kwa kasi na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa baadhi ya mataifa ambayo yamezuia watu wake kutoka nje ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivyo, saluni ni moja ya huduma zilizofungwa.
Kwa bahati nzuri nchini Tanzania bado huduma hizo zinaendelea kama kawaida kwa kuwa hakuna zuio lolote lililotolewa zaidi ya kuchukua tahadhari za kujizuia kama kunawa mikono na sabuni mara kwa mara, kuvaa barakoa na kujizuia kwenda kwenye mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
“Tofauti na kazi nyingine, saluni huwezi kufanyia mtandaoni hata Serikali imeona jambo hili ni gumu ndiyo maana haijafungia watu kukaa ndani…tuendelee hivi hivi kumuomba Mungu huku tukijilinda kwa kufuata taratibu za kiafya,” anasema Abiudi Godfrey, kinyozi anayefanya shughuli zake Kivule jijini Dar es Salaam.
Nje ya saluni ya Abiudi ameweka maji yanayotiririka na sabuni na kila mteja anayeingia hapa analazimika kunawa vema kabla ya kupatiwa huduma.
“Mimi sina safari za kwenda mjini maanake nikipata ugonjwa huu nitakuwa nimeletewa na wateja wanaokuja kunyoa,” anasema.
“Nimeagiza barakoa tatu kwa ajili ya kujikinga.”
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Pamoja na kuagiza barakoa ili ajikinge, katika saluni hiyo kuna wakati wateja huwa wengi na kujikuta wamejibana katika makochi mawili aliyoyaweka kwanye chumba kidogo cha futi 12 kwa 10.
Ukaaje wa wateja wake kwa mbanano ndani ya mita moja kinyume ya inavyoshauriwa na wataalamu wa afya unahatarisha afya za wengine wanaopata huduma na hata yeye anayetoa huduma.
Je, wakati huu wa corona watoa huduma za nywele na wanaoenda kupata huduma za saluni wanatakiwa kufanya nini ili kuepuka kupata virusi hivyo?
Vaa barakoa kila wakati
“Tumeshajua namna ugonjwa huu unavyoenea na WHO imeshasema kuwa maeneo ya vinyozi ni “high risks” (hatarishi) katika kusambaza corona. Nashauri kila unapoingia Saluni kupata huduma vaa barakoa ili kufunika vema pua na mdomo.
“Kinyozi naye ahakikishe amevaa muda wote barakoa,” Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Elisha Osati aliiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) mapema wiki hii.
Punguza idadi ya wateja wanaosubiri huduma
Inashauriwa kuwa watoa huduma za saluni wasiwe na wateja zaidi ya wawili katika chumba ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kutosha kukaa kwa umbali wa mita moja unaoruhusiwa wakati wanasubiri huduma.
Wengine wanaweza kufanya “booking” kwa simu ili kuzuia mkusanyiko usio wa lazima katika saluni yako. Ikiwezekana kuwa na mteja mmoja kwa wakati mmoja unayemhudumia.
Hakikisha mhudumu na mteja mmevaa barakoa. Saluni zisijaze wateja kupindukia, mteja mmoja au wawili tu kwa wakati mmoja. Picha|Mtandao.
Weka maji tiririka na sabuni
Hakikisha kila mteja anayeingia ameosha mikono na sabuni na maji tiririka uliyoyaweka nje hii ni mbali na ukweli kuwa anatakiwa kuwa amevaa barakoa. Kama una uwezo wa kuwa na vitakasa mikono pia unapaswa kuviweka nje ya maji.
Kaa nyumbani ukijisikia kuumwa, kukohoa au mafua makali
Kuna wakati mhudumu mmoja wapo anapatwa na homa, mafua au kikohozi kikavu, ashauriwe kubaki nyumbani mpaka hali yake itakapoimarika na ikitokea hali inabadilika awasiliane na mamlaka za afya kwa tiba zaidi. Hii inahusu pia watu wanaoenda kupata huduma saluni.
Vifaa vitakaswe na dawa za kuua virusi (disinfectants) mara kwa mara
Usafi umekuwa ni nguzo ya saluni nyingi nchini lakini kwa kipindi hiki usafi huo wapaswa kuwa maradufu. Vifaa vyote vinapaswa kutakaswa mara kwa mara baaada ya kutoa huduma. Vitambaa vinapaswa kuwa vingi na vinavyofuliwa mara kwa mara kupunguza uwezekano wa kuchangia kuambukiza wateja.
Muongozo kwa saluni uliotolewa na Serikali ya jimbo la Connecticut nchini Marekani unashauri kuwa kitambaa au taulo moja litumike kwa mteja mmoja na kuoshwa vyema baada ya kutumika.
Vifaa vyote vya kutolewa huduma vifungiwe eneo safi kuzuia kupata virusi na bakteria wengine.
Hata hivyo, kama unaweza kuzihudumia nywele zako nyumbani ni vema ukafanya mwenyewe ili kupunguza hatari ya kunaswa na virusi hivyo ambayo vimeshawapata watu 299 Tanzania na kuua 10 kati yao.
Watu 48 wameshapona ugonjwa huo hadi sasa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya.