Mwandishi wa Nukta Africa ashinda tuzo ya takwimu ya NBS 2023
- Ni Esau Ng’umbi ambaye amekuwa mshindi wa kwanza
- Asema tuzo hiyo imempa hamasa ya kuandika zaidi habari za takwimu.
- Hii ni mara ya tatu kwa Nukta Africa kushinda tuzo hizo tangu zilipoanzishwa mwaka 2019.
Dar es Salaam. Mwandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Esau Ng’umbi ameshinda tuzo ya takwimu kwa mwaka 2023 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Ng’umbi ambaye pia ni mhariri wa habari wa tovuti ya habari ya Nukta (www.nukta.co.tz) amekuwa mshindi wa kwanza katika kinyanganyiro cha tuzo hizo ambazo hutolewa kila mwaka na NBS kumtambua mwandishi bora wa takwimu Tanzania.
Tuzo hizo zimetolewa katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika leo Novemba 21, 2023 katika makao makuu ya NBS jijini Dodoma.
Habari iliyompa ushindi Ng’umbi inahusu teknolojia ya vifuu vya nazi na itakavyo waokoa wachimbaji na madhara ya kemikali ya zebaki ambayo hutumika kuchenjua madini yakiwemo ya dhahabu.
Hii ni mara ya tatu kwa Nukta Africa kung’ara katika tuzo hizo. Mwaka 2019, Daniel Samson ambaye sasa ni mkuu wa mafunzo na utafiti wa kampuni hiyo aliibuka mshindi wa kwanza katika tuzo hizo zilizotolewa jijini Dar es Salaam. Na huo ndio ulikuwa mwaka ambao NBS ilizindua tuzo hizo kwa mara ya kwanza.
Mwaka 2020 aliyekuwa mwandishi wa habari wa Nukta Africa, Rodgers George, alishika nafasi ya tatu katika tuzo hizo zilizotolewa mkoani Kigoma.
Soma zaidi:Teknolojia ya vifuu vya nazi itakavyo waokoa wachimbaji na madhara ya zebaki
Akizungumza na Nukta Habari mara baada ya kutangazwa kuwa mwandishi bora wa takwimu mwaka huu, Ng’umbi amesema tuzo hiyo imempa hari ya kuendelea kuandika zaidi habari za takwimu na anajisikia furaha kuwa miongoni mwa washindi.
“Tuzo hii inamaanisha Serikali na jamii sasa inatambua kazi kubwa ambayo tumekuwa tunaifanya, hususani ya kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia takwimu…
…Imenikumbusha kuendelea kuandika zaidi makala hizi za takwimu ili kuwafikia watu wengine zaidi, msisitizo umewekwa katika kuwafikia zaidi vijana,” amesema Ng’umbi.
Mshindi wa pili katika tuzo hizo ni Efraim Bahemu na wa tatu ni Aurea Simtowe wote kutoka gazeti la Mwananchi linalochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL).
Soma zaidi:Waandishi Nukta Africa wang’ara tuzo za Ejat 2022
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Rosemary Senyamule ameipongeza NBS kwa kutoa tuzo hizo kwani zinaongeza hari ya uandishi wa habari za takwimu zenye manufaa kwa jamii.
“Napenda kuwapongeza wa kuendesha shindano hili kwa kuwa linasaidia si tu kuimarisha uandishi bora wa habari zenye uhakika lakini pia linasaidia kujenga jamii inayopenda kutumia takwimu…
…kwakuwa wananchi wengi wanasoma habari za takwimu zinawasaidia kuongeza uelewa kuhusu masuala ya takwimu na matumizi yake katika nyanja mbalimbali za maendeleo na maisha kwa ujumla.
Aidha, Kiongozi huyo pia amawewataka waandishi na maafisa takwimu kuhamasisisha matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi sahihi katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.