Mazishi ya Mengi yatumika kuwaonya viongozi wabuguzi

May 9, 2019 2:11 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wametakiwa kuacha ubaguzi, kiburi na majivuno ya madaraka badala yake waendeleze unyenyekevu, upendo na amani aliyokuwanayo Reginald Mengi siku za uhai wake.
  • Dk Bashiru, Mbowe wakerwa na kauli zinazodaiwa  ni za kibaguzi zilizotolewa na RC wa Dar, Paul Makonda.
  • Serikali kuisaidia familia ya Mengi kuendeleza miradi yake. 

Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa Serikali na dini wameitumia ibada ya maalum ya kumuaga marehemu Dk Reginald Mengi kwa kukemea ubaguzi katika jamii na kuwataka watanzania wamuenzi mfanyabiashara huyo kwa kuendeleza upendo, unyenyekevu na amani kwa watu wote. 

Ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia Mei 2 mwaka huu mjini Dubai, Falme za Kiarabu imefanyika katika kanisa la KKKT usharika wa Moshi mjini leo (Mei 9, 2019) na kuhudhiriwa na viongozi mbalimbali ikiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. 

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT Dk Fredrick Shoo amesema namna pekee ya Watanzania kumuenzi Dk Mengi ni kuiga maisha yake ya kuwa mnyenyekevu na kutowabagua watu kwa misingi ya dini, ukabila na itikadi. 

Amesema Mengi hakuwa na kiburi kama walivyo baadhi ya viongozi vijana waliopata madaraka na aliwapenda watu wote na kuwasaidia walio wadogo na wenye uhitaji katika jamii. 

“Tena akafanya hivyo bila kuwabagua, hakuwabagua sijui ni wadini gani, tabaka gani, wa itikadi gani, wala hakuwabagua kwa misingi ya kikabila. Sasa mimi nawaomba sana kama kuna kitu ambacho tunaweza kumuenzi ndugu yetu huyu na tukaiga ni ile roho yake ya upendo ya kutokuwabagua watu kwa misingi niliyoitaja hapa,” amesema Dk Shoo.

Amesema kama Watanzania wanataka kupokea baraka kutoka kwa Mungu, waache kubaguana na kujenga zaidi maridhiano kama alivyofanya marehemu Mengi siku za uhai wake. 

“Dk Mengi alithamini sana maridhiano ya Watanzania wote licha ya tofauti zetu maskini, matajiri, wenye mamlaka na wasio na mamlaka. Kama kuna dhambi ambayo tunapaswa kuitubu ni dhambi ya kubaguana. Tunahitaji kutubu kama kweli tunahitaji kupokea baraka kutoka kwa Mungu,” amesisitiza Dk Shoo. 

Kutokana na tabia ya unyenyekevu na upendo aliyokuwanayo Mengi alikuwa mpatanishi wa makundi mbalimbali katika jamii na kuwa chachu katika shughuli za Maendeleo. 


Soma zaidi:


Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mengi atakumbukwa kwa kutumia utajiri wake kuwasaidia watu wote bila ubaguzi hasa wasio na uwezo na wenye mahitaji maalum. 

“Alikuwa mtu muungwana na mpenda amani na mwenye moyo wa kusaidia wengine. Katika mambo ambayo yamenigusa sana ni kitendo cha Dk Mengi kupata chakula na watu wenye ulemavu tangu mwaka 1990,” amesema Majaliwa.

Amesema Serikali iko tayari kuisaidia familia ya Mengi kusimamia miradi aliyoiacha kama itahitaji msaada ili kuendelea kumuenzi mwanzilishi huyo wa makampuni ya IPP. 

Viongozi mbalimbali wa nchi wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakiwa katika ibada ya kumuaga Dk Mengi hapa Kanisa la KkKT, Usharika wa Moshi. Picha|Radio One.

Sakata la Makonda laibukia msibani

Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk Bashiru Ally ametumia msiba huo kumuombea msamaha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye inadaiwa alitoa maneno ya kibaguzi dhidi ya watu wa kabila la wachaga wakati wa kumuaga Mengi jijini Dar es Salaam. 

“Kuwa viongozi bora, watiifu, wanyenyekevu na wenye heshima, naomba nitumie fursa hii kumuombe msamaha kijana wangu Makonda mimi namfahamu na hii ni mara yangu ya pili namsema hadharani,” 

Amesema ubaguzi unaofanywa na viongozi hasa vijana unatokana na kutoandaliwa vizuri katika maadili na uongozi.

“Kuhusu uongozi na umuhimu wa kuwaandaa vijana wetu, baba Askofu kazi hiyo hatujaifanya na kwasababu hatujaifanya hatujavuna matunda ya kutokuwaandaa vijana wetu,” amesema Dk Bashiru.

Baadaye Makonda alipita mbele ya kanisa na kumshukuru Dk Bashiru kwa kumuombea msamaha akisema “Namshukuru Katibu Mkuu kwa kuomba radhi kwa niaba yangu, hakika ni upendo wa hali ya juu.”

Sakata la Makonda kuhusu kauli yake kuwa hakuamini kama mchaga anaweza kuwasaidia walemavu limeibuliwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) Freeman Mbowe ambaye alipopewa nafasi ya kutoa salamu alikemea kauli za kibaguzi zinazotolewa na viongozi ambao wamejaa kiburi cha madaraka na utajiri.

“Kauli za kuambiana kwamba kuna makabila fulani hayawezi kuwasaidia walemavu si za kweli ni za kibaguzi na lazima tuwakemee. Nawaomba wale wote walioguswa na kauli zile tutoe msamaha ni kweli tunataka kumuenzi mzee wetu Mengi tujifunze kusema kweli na ukweli utatuweka huru,” amesema.

Baada ya Makonda kuomba msamaha alishikanishwa mikono na Mbowe ikiwa ni ishara ya mapatano kwa watu wote ambao hawakupendezwa na kauli yake. 

Hatimaye, safari ya mwisho ya Mengi imehitimishwa leo kwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele katika makaburi ya familia yaliyopo katika kijiji cha Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro. 

Enable Notifications OK No thanks