Matatizo ya afya ya akili: Kaburi jipya la wanandoa

Esau Ng'umbi 0250Hrs   Julai 04, 2022 Ripoti Maalum
  • Wataalam wa afya wasema afya ya akili ina mchango mkubwa kwa ukatili kwa wanandoa.
  • Ni baada ya kuongezeka visa vya wanandoa kuuana.
  • Serikali, wadau waungana kutafuta suluhu ya kudumu.

Dar es Salaam. Ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao yote ya duniani.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, taasisi hiyo ya ndoa lazima ihusishe watu wawili waliokubali kuishi pamoja bila kulazimishwa.

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti katika siku za hivi karibuni, ndoa imekuwa sehemu ya kukatisha maisha ya wenza walioapa kuwa pamoja.

Hii imedhihirika mara baada ya  kuripotiwa matukio kadhaa ya kikatili hususani visa vya mauaji  ambapo  mwanandoa mmoja hutoa uhai wa mwenza wake kisha  na yeye kujiua au kutokomea kusikojulikana  kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi.

Tukio la mauaji ya wanandoa lililoteka hisia za wengi ni lile lililotokea  jijini Mwanza Mei 28, 2022 ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Swalha Swaum aliuwawa kwa kupigwa risasi saba na mume wake Said Oswayo ambaye naye alijiua baadaye. Sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) katika taarifa yake ya Mei 2022 kwa vyombo vya habari kimeeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mauaji ya wenza ambapo mwaka 2021 yaliripotiwa mauaji 31.

Mwaka 2022 ndani ya kipindi cha mwezi Mei pekee kituo hicho kilipokea visa saba vya mauaji ya wenza.

Afya ya akili isipodhibitiwa inaweza kuharibu maisha ya mtu. Picha| Unsplash/Yosi Prihantoro


Sababu za mauaji hayo ni nini?

Kwenye jamii yapo mengi yanayozungumzwa kuhusu sababu zinazosababisha mauaji ya wenza ikiwemo imani za kishirikina, mafarakano ndani ya ndoa, wivu uliopitiliza pamoja na matatizo ya afya ya akili.

Licha ya afya ya akili kutotajwa sana kama kisababishi cha vifo vya wanandoa, ni miongoni mwa mambo yanayotakiwa kupewa kipaumbele katika kudhibiti na kupunguza matukio hayo ya mauaji.

Eva Milola kutoka Mwanza anasema wakati mwingine msongo wa mawazo na hasira zinaweza kusababisha mtu  kufanya mauaji kwa mwenza wake kutokana na kufanyiwa jambo fulani ikiwa ni pamoja na kutothaminiwa.

“Hasira, msongo wa mawazo inaweza ikawa sababu ya mtu kufanya mauaji, mtu anawaza sasa nifanyeje anaona bora aue,” anasema Milola.

Mkazi wa jijini Dar es salaam, Alto Haule anasema yeye haoni uhusiano uliopo kati ya matatizo ya afya ya akili na vitendo vya mauaji kwa sababu anaamini kuwa kabla watu hawajaoana huwa na muda wa kusomana na kubaini kasoro za mwenza wake.

“Mtu mwingine anaweza akaenda kwa mganga wa kienyeji akaambiwa fanya hivi, muue mke wako na yeye akafanya. Sababu nyingine ni maneno ya ufitinishi mtu anaweza akawa anachukua maneno kutoka kwa watu bila kuangalia kama ni kweli au uongo,’ anasema Haule.

Wakati Haule akiwa haamini kama matatizo ya afya ya akili yanaweza kuwa sababu ya mauaji kwa wanandoa, Umoja wa Mataifa (UN) unaeleza kuwa tatizo hilo lipo kwenye jamii na limekuwa chanzo cha kuharibu mahusiano ya watu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Mwaka 2019, takribani watu bilioni 1 wakiwemo asilimia 14 ya vijana wote duniani walikuwa wanaishi na tatizo la akili ambapo  mtu mmoja  kati ya 100 hujiua na asilimia 58 ya wanaojiua ni watu wenye umri wa chini ya miaka 50. 


Soma zaidi: 


WHO Inabainisha kuwa watu wenye tatizo kubwa la afya ya akili kwa wastani hufariki dunia miaka 10  hadi 20 mapema zaidi kuliko watu wa kawaida kutokana na magonjwa ya mwili yanayoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa LHRC, sababu kubwa ya mauaji yatokanayo na wivu wa kimapenzi ni kutokana na migogoro isiyokoma ndani ya ndoa.


Mchango wa afya ya akili katika mauaji ya wanandoa

Kwa mujibu wa asasi ya kiraia ya Tap Elderly Women's Wisdom for Youth (TEWWY) katika kitabu chake cha Maswali Yaulizwayo na Jamii Kuhusu Afya ya Akili na Majibu Yake, afya ya akili inahusu ustawi wa mtu katika ngazi kuu tatu ambazo ni  nafsi na utashi, akili na fikra, mwili na hisia/mihemuko.

Hivyo afya ya akili inahusiana sana na jinsi mtu anavyofikiri, anavyojisikia na anavyotenda kwa maana mtu akifikiri vizuri ni rahisi kujisikia vizuri na kutenda mambo mazuri. 

Mtu akiwa na fikra hasi, atajenga hisia hasi na kisha matendo yake yatakuwa hasi pia. Ikiwa mtu hana afya njema ya akili basi atajikuta katika matatizo ya akili ambayo yana mchango kutokea kwa ukatili kwa wanandoa.


Matatizo ya afya ya akili hurithiwa

Mtaalamu wa masuala ya afya ya akili, Dk Sylvia Ngonyani anabainisha kuwa matatizo ya afya ya akili hurithiwa kutoka kwa wazazi na wakati mwingine huchangiwa na matumizi ya dawa za kulevya.

“Watu wengine magonjwa ya akili wanarithi kutoka kwa wazazi nyuma kabisa…lakini watu wengine wanapata ukubwani kutokana na mtindo wa maisha, mazingira na namna wanavyoishi…

“…siku hizi tuna wimbi kubwa sana la watu wanaotumia vilevi kupita kiasi, kuvuta bangi kupita kiasi, kunywa pombe kupita kiasi vinaweza kusababisha mtu kutokuwa na afya ya akili,”  anasema Dk Ngonyani.

Dk Ngonyani anasema ikiwa mmoja wa wanandoa akapata tatizo hilo anaweza kufanya ukatili kwa mwenzake ikiwemo kumpiga au hata kumuua kwa sababu atakayoona inafaa kwake licha ya kuwa ni kinyume cha sheria kutwaa uhai wa mtu. 


Tangazo


Mtaalamu wa Saikolojia kutoka mkoani Mbeya, Pulumba Msafiri anasema magonjwa ya akili yanaweza kumpata mtu endapo atafanya au kufanyiwa jambo litakalosababisha awe na msongo wa mawazo kupita kiasi.

Mathalan, kukutana na majanga kama ajali, uvamizi, au ubakaji, jambo ambalo huathiri utendaji kazi wa akili yake na hivyo kuwa chanzo cha kumdhulu mtu mwingine. 

“Ni wachache sana wanaopata magonjwa ya akili kwa kurithi asilimia kubwa wanapata kutokana na madhila mbalimbali tunayopitia kwenye maisha yetu ya kila siku,” anasema Msafiri.

Watalaam hao, Msafiri na Dk Ngonyani wanasema afya ya akili isipopewa kipaumbele katika mahusiano inaweza kuleta madhara makubwa kwa wanandoa ikiwemo kuibuka kwa ukatili. 

Utamtambuaje mwanandoa mwenye matatizo ya akili? Utamsaidiaje mtu mwenye matatizo ya akili? Serikali, wadau wanachukua hatua gani kudhibiti tatizo hilo? Usikose sehemu ya pili ya makala hii.

Related Post