Watetezi wa haki za binadamu watoa mwelekeo kukomesha mauaji ya wanandoa
- Washauri itungwe sheria kudhibiti ukatili unaofanyika majumbani.
- Elimu na mafunzo kuhusu maadili yaongezwe kwenye jamii.
Dar es salaam. Wakati mjadala ukiendelea kwenye jamii kuhusu matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya watu kuwaua wapenzi wao kikatili, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kutunga sheria maalum kukomesha matukio hayo.
Tamko la LHRC limekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za mwanamke aliyetambulika kama Swalha Salumu (28) aliyeuawa na mume wake Said Oswayo kwa kupigwa risasi saba kwa sababu ya wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa LHRC, mwezi Mei pekee wamepokea visa saba vya mauaji ya wenza yatokanayo na wivu wa kimapenzi, jambo ambalo siyo kiashiria kizuri kwa mstakabali wa jamii.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, vitendo vya ukatili vimeongezeka kwa kiwango kikubwa ambapo mwaka 2019 yalikuwa matukio 39,365 na mwaka uliofuata yakaongezeka hadi matukio 42,414.
Mwaka 2021 matukio ya ukatili wa kijinsia yalipungua hadi 29,373 huku wanawake wakiwa wahanga zaidi wa matukio hayo ni wanawake kwa asilimia 60 huku mikoa ya Shinyanga, Manyara, Mwanza, Mara na mbeya ikitajwa kuwa na viwango vya juu vya ukatili.
Zinazohusiana:
- Kutana na Aneth David mwanasayansi anayechipukia Tanzania
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
- Esther Mndeme: Muongozaji aliyewashangaza wengi tuzo za filamu 2019
Sheria zirekebishwe
LHRC imependekeza kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria ambazo zina udhaifu ikiwemo Sheria ya Ndoa namba 29 ya mwaka 1979 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Sheria hiyo haielezi bayana ukatili upi mtu akifanyiwa unaweza kusababisha ndoa kuvunjika na sheria hiyo kuruhusu ndoa kwa wasichana wenye umri wa miaka 13.
“Wananchi wanatakiwa kutoa taarifa ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye vyombo vyenye mamlaka ya kuchukua sheria na si kujichukulia sheria mikononi,” amesema Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC.
Vyombo vya dola vimeshauriwa kurudisha imani kwa wananchi kwani tafiti zinaonesha kwamba vitendo vya kujichukulia sheria mikononi vinatokana na wananchi kupoteza Imani na vyombo vya dola baada ya watuhumiwa wa baadhi ya matukio kuonekana mtaani baada ya kufikishwa katika vyombo vya dola bila mafanikio.
Henga aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Mei 31, 2022 jijini Dar es Salaam amesema wazazi nawalezi wa watoto mashuleni watimize wajibu wao wa malezi kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
“Wanandoa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria ya ndoa pindi wanaposhindwa kuelewana na si kutwaa uhai wa mwenza,” amesema Henga huku akiwataka wanandoa kutoa taarifa kuhusu ukatili pale wanapofanyiwa hivyo na wenza wao ili kuweza kupata msaada na kuepusha madhara zaidi.
Serikali imeshauriwa iziwezeshe kamati za watoto za wilaya na mikoa ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na vViongozi wa dini wahubiri mafundisho yenye kueneza upendo na hofu ya Mungu miongoni kwa watanzania.
Sheria zenye mapungufu zirekebishwe ili kuweza kuendana na wakati na mahitaji na pia kutengenezwe sheria ya ukatili wa majumbani ili kuweza kulinda wenza ipasavyo dhidi ya vitendo vya ukatili.
Tangazo: