Matarajio waliyonayo Watanzania kwa Rais Samia wa Tanzania

March 20, 2021 5:20 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi yao wamesema wanapenda kuona anaivusha Tanzania kiuchumi na kisiasa ili kupata maendeleo.
  • Wengine wanapenda kuona akiendeleza kazi nzuri ya mtangulizi wake Hayati Rais John Magufuli.
  • Mazingira ya kufanya biashara na umoja wa kitaifa ni tarajio lingine la Watanzania. 

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Samia Suluhu Hassan kuapa kuwa Rais wa sita wa Tanzania, wananchi mbalimbali wameeleza matarajio waliyonayo kwa kiongozi huyo mkuu wa nchi huku baadhi yao wakisema wana imani itaivusha nchi salama na kuukuza kiuchumi wa nchi. 

Mama Samia ameapishwa leo Machi 19 Ikulu mkoani Dar es Salaam akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Rais John Magufuli ambaye alifariki dunia Machi 17 mwaka huu kwa maradhi ya moyo. 

Rais Samia katika hotuba yake mara baada ya kuapa amewataka Watanzania kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini kwa sababu Serikali yao iko imara na wanatakiwa kushikamana ili kujenga nchi yao. 

“Si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo. Si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wakushikana mikono na kusonga mbele. 

“Ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu za pamoja kujenga Tanzania mpya ambayo mpendwa wetu Rais Magufuli aliitamani,” amesisitiza Samia, Rais wa awamu ya sita wa Tanzania. 

Hata wakati kiongozi huyo mkuu wa nchi akionyesha mwanga wa matumaini siku zijazo kwa Tanzania, wananchi nao wameeleza matarajio waliyonayo kutoka kwa kiongozi huyo na Serikali itakayoiongoza mpaka mwaka 2025. 

Mkazi wa Mbeya, Bedom Mwakaje amesema siku ya leo imekuwa ni muhimu sana kwa mwanzo mpya wa Tanzania ikizingatiwa kuwa Watanzania walitoka kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana wakiwa na tofauti mbalimbali ambazo huenda zimeleta mgawanyiko hasa wa kisiasa.

“Hotuba yake nimeisikiliza ilikuwa nzuri inaonyesha matumaini makubwa ya kuijenga Tanzania mpya yenye mshikamano. Nadhani atayatekeleza aliyoyasema hasa kuwafanya wananchi wa kada mbalimbali kuwa wamoja ili kujiletea maendeleo ya kweli,” amesema Mwakaje ambaye ni mkulima. 

Amesema pia anatarajia kuona hali ya kiuchumi ikiimarika hasa kwa wakulima kuwekewa mazingira mazuri ili wafaidike na kilimo kwa kuwapatia masoko ya uhakika ya mazao ambayo kwa sehemu kubwa yameathiriwa na janga la Corona. 

Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania. Picha|Steven Genya

Wakati Mwakaje akitazamia mwanzo mpya, baadhi ya wananchi wa jiji la Mwanza wanatarajia Mama Samia aliyekuwa Makamu wa Rais ataendeleza mambo mazuri aliyoyaanzisha mtangulizi wake Magufuli. 

Juma Peter, mkazi wa jiji hilo lilipo kanda ya Ziwa amesema anaamini kuwa Taifa litaendelea kuwa imara kama alivyoliacha Rais Magufuli, japo siyo viongozi wote wanaweza kuendeleza aliyoyaacha mtangulizi wake. 

“Tunaelewa Hayati Magufuli ameacha alama na ameonyesha mwelekeo ambao kila mmoja ameuona, hivyo hata kwa kiongozi huyu aliyeapa leo nina imani atatimiza yale aliyoyaacha,” amesema Peter

Amewataka Watanzania kushikamana kuhakikisha wanatimiza ndoto za Rais Magufuli na hawapaswi kumwangusha Rais mpya badala yake aungwe mkono kwa kazi atakazokuwa anafanya.

Rais Samia mwenye umri wa miaka 61 anakua rais wa kwanza mwanamke Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkazi  wa Nyakato jijini humo, Rachel Mayala amesema siku zote Mama Samia amekuwa ni kiongozi, mwalimu na mchapa kazi, kazi aliyoapa kuifanya leo kwa mujibu wa katiba ataitekeleza. 

“Tumwombee, tumwamini atafanya tuna imani atatekeleza kwa kiwango kikubwa, Watanzania tupo nyuma yake tunamuombea,” amesema Rachel ambaye uso wake ulijawa na furaha wakati akihojiwa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Hata hivyo, Thobias Mayaya ambaye ni Mkazi wa Mwanza amesema hawezi kumwamini sana Rais mpya ingawa anampa muda kuona utendaji wake, huenda namna anavyofikiria inaweza kuwa tofauti. 


Soma zaidi:


“Tumwamini, akishirikiana vizuri na watendaji wa ngazi ya chini tutafika kule ambako Rais Magufuli alipotaka kwenda, wote tumeshuhudia uongozi wake ulivyokuwa thabiti hivyo kwa kuwa amepita kwenye mikono yake hatuna mashaka naye,” amesema Jaquline Mathias akitofautiana na Mayaya akimtathmini Rais Samia kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kiongozi kwani una uzoefu wa muda mrefu. 

Wakazi Dar nao watoa ya moyoni

Kuapishwa kwa Rais Samia imekuwa ni furaha kwa wanafunzi na kizazi cha wasichana ambao wanasema kiongozi huyo atakuwa kioo kwao katika kutimiza malengo ya kielemu kwa sababu ana uwezekano mkubwa wa kufungua fursa za wao kufanikiwa kimaisha. 

Kwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Caroline Henry, furaha yake ni kumpata Rais wa kwanza mwanamke na anaamini ataboresha zaidi miundombinu na uongozi wake utakuwa chachu kwa wasichana wengi.

“Naamini ataenda kufanya kazi. Mama Suluhu ni mchapa kazi. Malkia wa nguvu na anajua wananchi ni nini tunakitaka. Atainua wananchi na maendeleo ya nchi kiujumla,” amesema Caroline. 

Caroline anaamini kwa kazi zilizokuwa zinaendelea ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na mradi wa umeme wa mto Rufiji ataiendeleza na kufanya mambo mengine makubwa kuboresha maisha ya Watanzania hasa wanyonge.


TANGAZO:


Baadhi ya wajasiriamali mkoani hapa wamesema wanaamini mazingira ya biashara yataboreshwa zaidi ili kuwawezesha kufanya biashara kwa uhuru na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. 

Theresiah Venance ambaye ni mjasiriamali wa vifaa vya plastiki mkoani Dar es Salaam amesema kwake anatarajia uongozi bora utakaoleta mabadiliko hasa katika sekta ya biashara. 

“Kuna vitu ambavyo kama wanawake tulikuwa hatuvipati. Fursa zikiwemo ajira, naamini zitaachia,” amesema Theresia.

Binti huyo ambaye sauti yake ilielezea furaha aliyonayo amesema anaamini Rais Samia atawekeza katika vipaji, ujasirimali kwani wanawake wengi nchini walipitwa na fursa ya elimu rasmi. 

Naye Mchungaji wa kanisa la Greater Light of Glory, Daimon Nathani amesema ana imani na Rais Samia kwani maono ya Rais Magufuli ni maono yake pia.

Kwa kiongozi huyo wa dini, Rais Samia ni kiongozi ambaye amekuwa serikalini kwa muda mrefu jambo ambalo linamfanya kuwa kiongozi aliye na misingi thabiti.

“Nina amini kuwa atayabeba maono ya Hayati Rais Magufuli kwa sababu Dk Magufuli aliweka alama katika uongozi na Rais Samia hawezi kurudi nyuma ya alama hiyo,” amesema Mchungaji Nathani.

Wewe unatarajia nini kutoka kwa Serikali itakayoingoza Mama Samia ambaye leo amekabidhiwa rasmi jukumu la kuongoza nchi ya Tanzania na watu wake?

Habari hii imeandikwa na Daniel Samson, Rodgers George na Mariam John

Enable Notifications OK No thanks