Mambo ya kujifunza baada ya mgao wa maji kupungua Dar

December 14, 2022 6:09 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni umuhimu wa kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadaye.
  • Kuchimba visima na mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua.
  • Kujenga tabia za matumizi bora ya maji na utunzaji wa mazingira.

Dar es Salaam. Kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja uliopita, hali ilikuwa siyo shwari Dar es Salaam, jiji lililopo mashariki mwa Tanzania.

Ilikuwa ni kelele, manung’uniko na lawama za watu wanaoishi katika jiji hilo linalokuwa kwa kasi Afrika na duniani. Walikuwa wakilalamikia mgao wa maji katika nyumba zao na maeneo ya uzalishaji.

Baadhi yao walilazimika kuikosa kabisa huduma hiyo kwa siku hadi wiki kadhaa, jambo lililowaweka katika wakati mgumu wa kujisitiri, usafi binafsi na afya zao. 

Tabu hiyo ya maji ambayo ilimgusa karibu kila mtu jijini hapa wakiwemo viongozi waliokuwa wakihaha huku na kule kutafuta suluhu, ilisababishwa na kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua za vuli katika mikoa inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Kwa kawaida mvua hizo huanza kunyesha mapema, Oktoba. Hata hivyo, mwaka huu zilichelewa, jambo lililosababisha kina cha maji cha Mto Ruvu kupungua na kushindwa kupeleka maji katika vyanzo vya Ruvu Chini na Ruvu Juu. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), uzalishaji wa maji kwa jiji hilo ulipungua kwa takriban nusu hadi lita milioni 300 kwa siku ikilinganishwa na uzalishaji wa kawaida wa zaidi ya lita milioni 500.

Kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuchimba na kufufua visima vya maji ili kuwapunguzia wananchi makali ya ukosefu wa bidhaa hiyo muhimu kwa uhai wa binadamu na viumbe wengine. 

Licha ya kuwa Serikali imetangaza kuisha kwa mgao wa maji jijini hapa baada ya mvua kuanza kunyesha, wakazi wake wana la kujifunza hasa kuweka mifumo itakayowasaidia kutunza maji yatakayowasaidia wakati bidhaa hiyo inapoadimika ikizingatiwa kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zitaendelea kujitokeza.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), takribani watu bilioni 4 duniani kote wanakutana na uhaba wa maji angalau mara moja kila mwaka.

Hiyo ni sawa na kusema asilimia 33 ya watu wote duniani wanaishi kwenye ukanda wenye uhaba wa maji.

Kutokana na kuchelewa kwa mvua za vuli, wakazi wa Dar es Salaam walilazimika kupata maji kwa mgao na wengine kukosa kabisa kwa siku kadhaa. Picha | Dar24.

UNICEF inasema moja ya suluhisho ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji ni utunzaji wa maji kwenye visima pamoja na uvunaji wa maji ya mvua.

Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu ambao wanatamani kuanza jitihada za utunzaji wa maji zifuatazo ni mbinu zinaweza kukusaidia:


1. Uvunaji wa maji ya mvua

Kwa mujibu wa UNICEF, uhifadhi wa maji ya mvua unaweza kusaidia maeneo yenye ukame au kusaidia wakati ambapo nchi au mji unapitia uhaba au upungufu wa maji.

Khalid Juma, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam anasema utunzaji wa maji ya mvua unaweza pia kurahisisha shughuli za nyumbani wakati wa uhaba wa maji pia kwa shughuli nyingine kama umwagiliaji wa bustani.

“Kama ningevuna maji ya mvua bustani yangu isingekauka kutokana na uhaba wa maji tuliopitia ndani ya miezi hii michache,” anasema Khalid.

Tayari Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa mradi wa bwawa la Kidunda mkoani Morogoro litakalotumika kuvuna maji ya mvua. 

Ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 mpaka 2025 na utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika Mkoa wa Pwani pamoja na jiji la Dar es Salaam kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wote mwaka mzima.

Wananchi pia wanashauriwa kuchimba mabwawa au kujenga matanki katika nyumba zao na kuhifadhi maji ya mvua kuwasaidia wakati wa kiangazi bila kuisubiri Serikali. 


Soma zaidi:


2. Uchimbaji wa visima

Kwa wakazi wa Dar es Salaam wenye visima changamoto ya uhaba wa maji haukuwapata kabisa, huku wegine wakiingiza pesa kama anavyokiri Bernard Hinza, muuza maji maarufu mitaa ya Kijitonyama Kisiwani jijini Dar es Salaam.

“Kipindi cha mgao nimeingiza sana pesa kwa siku sikosi Sh30,000 ila kilichosaidia ni uwepo wa kisima kwa mama mmoja anaitwa mama Koroshu, sisi tulikuwa tunanunua Sh100 kwa  dumu la lita 20 tunakuja kuliuza Sh500 mpaka Sh1,000,” anasema Hinza.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maji na Usafi wa Mazingira (UN Water) limetaja uchimbaji wa visima kama moja ya suluhisho la kupambana na ukame unaosababisha uhaba wa maji.

“Kulinda na kutumia maji ya ardhini kwa njia endelevu kutakuwa msingi wa kuishi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka,” limesema shirika hilo.

Visima hivi vinaweza kuchimbwa kwa ushirikiano wa kaya kadhaa na kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. 

3.Ununuzi wa vyombo vya kuhifadhia maji

Mbinu nyingine inayoweza kusaidia wakazi wa jiji hilo kupambana na uhaba wa maji utakapotokea ni kununua vyombo vikubwa vya kuhifadhia maji vyenye uwezo wa kutunza maji kwa muda mrefu.

Anerth Kiwia maarufu kama mama Kiwia, mkazi wa Kunduchi Jijini Dar es Salaam anamiliki matenki makubwa ya maji. Kwa kipindi chote cha mgao wa maji yeye na familia yake hawakupata kabisa uhaba huo.

“Matenki haya yana miaka zaidi ya 10 hapa kwangu niliyanunua kipindi mji huu ulipokuwa na changamoto ya maji kabla ya mabomba ya maji ya Dawasa hayatufikia, yamenisaidia sana kipindi hiki cha mgao wa maji,” anasema mama huyo.


4. Matumizi ya wastani nyumbani

Shughuli za nyumbani kama kupika, kufua, kuosha vyombo huwa zinahitaji maji mengi, wakati wa uhaba wa maji au mgao wa maji baadhi ya shughuli hizi husitishwa au kufanyika kwa kiwango kidogo.

“Ikiwa unataka kuhifadhi maji wakati wa kufanya shughuli za nyumbani kama kuosha vyombo ni vyema kuviosha kwa pamoja kuliko kuosha kimoja kimoja,” imesema tovuti ya Pinkvilla.

Shughuli nyingine kama kufua na usafi wa nyumba tovuti hiyo inashauri ni vyema kutumia tena maji yaliyotumika kwenye shughuli hizo (reuse).

“Maji yanayotumika kwenye kufua, yanaweza kutumika tena kwa ajili ya kufanya usafi wa nyumba, bafu pamoja na kumwagilia bustani,” imeeleza tovuti hiyo.

Hiyo siyo itasaidia kupunguza matumizi makubwa ya maji bali, bili utakayopata kila mwezi itakuwa himilivu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Oktoba 10, 2022 alikagua visima vya dharura mkoani Dar es Salaam vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.

5. Kurejeleza maji 

Mbinu nyingine inayoweza kusaidia uhifadhi wa maji ni kurejeleza maji yaliyokwisha kutumika. Kwa mujibu wa tovuti ya i control pollution, urejelezaji wa maji ni  kitendo cha kutumia tena maji machafu yaliyosafishwa kwa madhumuni ya manufaa kama vile umwagiliaji wa kilimo na mazingira na michakato ya viwandani.

Urejezaji huu wa maji unaweza kufanywa nyumbani kwa kutumia mashine maalum na kusaidia kutunza maji endapo uhaba wa maji ukitokea tena. Hata hivyo, inashauriwa maji haya yasitumike kwa ajili ya kunywa.

“Maji yaliyorejelezwa  mara nyingi hutumika kwa shughuli mbalimbali  (sio kwa ajili ya kunywa), kama vile kilimo, mandhari, mbuga za umma, na matumizi mengine,” imeeleza tovuti hiyo.

Enable Notifications OK No thanks