RC Makalla ataja sababu mgao wa maji kuisha Dar
- Ni baada ya kuanza kunyesha mvua na uzalishaji kuanza Ruvu Chini na Ruvu Juu.
- Asema wamewaondoa watu pembezoni mwa vyanzo hivyo.
- Dawasa watakiwa kuimarisha miundombinu ya maji.
Dar es Salaam. Huenda wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakapata ahueni baada ya Serikali kutangaza kumalizika kwa mgao wa maji kutokana na chanzo cha maji cha Ruvu Chini mkoani Pwani kuanza kufanya kazi.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja, wakazi wa jiji hilo wamekuwa wakitaabika na uhaba wa maji baada ya kuchelewa kwa mvua za msimu na hivyo kusababisha kupata maji kwa mgao na wengine kukosa kabisa, jambo lililoathiri shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, maji katika chanzo hicho yamerejea kama kawaida baada ya kuanza kunyesha kwa mvua na kutitirika kwenye mto Ruvu ambao ndiyo chanzo kikubwa cha maji.
“Maji yamerejea katika ujazo wake wa kawaida na zaidi na kama mnavyojua vyanzo vya maji vinavyotegemewa ni Ruvu Juu inayochangia lita milioni 196 na hapa Ruvu Chini inachangia maji lita milioni 270 na kufanya jumla kuwa lita za ujazo 466 miioni na sasa tuna maji ya kutosha,” Makalla amenukuliwa na gazeti la Mwananchi.
Mapema leo Novemba 25, 2022, Makalla na timu ya wataalam walitembelea chanzo cha maji Ruvu Chini, huku akitangaza kuisha kwa mgao baada ya kuona ujazo wake umerejea kwenye hali yake ya kawaida.
Mambo yaliyosaidia kumaliza mgao
Makalla amesema awali maji katika vyanzo hivyo yalikauka kabisa lakini walichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwatoa watu wanaofanya shughuli zao karibu na mto Ruvu kuanzia milima ya Uruguru mkoani Morogoro hadi Pwani.
Pia Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) walichukua hatua ya kufukua visima 20 katika Mkoa wa Dar es Salaam na kufanya jumla ya visima vinavyotoa huduma kufikia 169. Visima hivi vinazalisha lita milioni 31.9 kwa siku na kuingiza kwenye mfumo wa maji katika jiji hilo.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alitoa Sh24 bilioni kwa ajili ya mradi wa visima vya Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni unaozalisha lita za ujazo milioni 70 ambao umesaidia kupunguza makali ya mgao wa bidhaa hiyo muhimu.
Makalla amewashukuru wakazi wa jiji hilo linalokua kwa kasi Afrika kwa uvumilivu katika kipindi chote cha hali ngumu ya mgao wa maji walichopitia.
Soma zaidi:
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mgao huo uliwaweka katika wakati mgumu kwa sababu walikuwa wakipata maoni tofauti kutoka kwa wananchi.
“Wateja wote wa kwetu na kama hawapati maji wanatafuta majibu kulikuwa kipindi kigumu kama cha wiki tatu hivi, Lakini nawashukuru viongozi wa dini kilichofanyika kama miujiza mvua zimeanza kunyeesha na maji yamejaa,” amenukuliwa Mhandisi Luhemeja na gazeti la Mwananchi na kueleza kuwa,
“Ukichukua maji ya Ruvu juu, Ruvu Chini, Wami na Kigamboni ni kama jumla ya lita 590 milioni wakati mikoa hiyo mahitaji yake ni Lita 544 milioni.”
Hata hivyo, changamoto iliyobaki ni uchakavu wa miundombinu ambapo amesema wataendelea kuboresha ili kuimarisha upatikanaji wa maji.