Makosa dhidi ya binadamu yaongezeka kwa asilimia 26 Tanzania

Lucy Samson 0246Hrs   Februari 20, 2024 Habari
  • Yafikia 12,790 kwa mwaka 2023.
  • Makosa hayo ni pamoja na mauaji, ubakaji, ulawiti, wizi wa watoto, kutupa watoto na usafirishaji haramu wa binadamu.
  • Bunge lashauri kutolewa kwa elimu kwa jamii kupitia viongozi wa dini ili kupunguza makosa hayo.

Dar es Salaam. Huenda Jeshi la Polisi na vikosi vya ulinzi na usalama vitakatakiwa kuongeza nguvu ya kukabiliana na makosa dhidi ya binadamu yaliyoongezeka kwa asilimia 26 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Bunge, makosa dhidi ya binadamu yanahusisha mauaji, ubakaji, ulawiti, wizi wa watoto, kutupa watoto pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu.

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) iliyosomwa hivi karibuni bungeni jijini Dodoma, inabainisha kuwa mwaka 2023 makosa 12,790 dhidi ya binadamu yaliyoripotiwa. 

Idadi hiyo imeongezeka kwa kwa asilimia 26 kutoka makosa 10,130 yaliyoripotiwa mwaka 2022 jambo linalowazuia raia kutekeleza shughuli zao kwa uhuru. 

“Tathmini zaidi zinaonyesha kuwepo kwa malalamiko ya wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika wamekuwa wakiporwa mali na rasilimali zao…

…wanapotekeleza shughuli zao za uvuvi, kamati inatoa rai kwa Jeshi la Polisi kuimarisha doria katika maeneo hayo,” amesema Vita Kawawa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Februari 9, 2024 bungeni Dodoma.


Soma zaidi: Watuhumiwa 13 wakamatwa kwa matukio ya uhalifu Mwanza


Aidha, kamati hiyo imebaini kuongezeka kwa makosa mengine ikiwemo ya kuwania mali kwa asilimia 8.3, uhalifu wa kifedha kwa asilimia 6.4 huku makosa dhidi ya jamii yakipungua kwa asilimia 24.1.

Makosa hayo ni yale yanayohusisha kutumia silaha, uvunjaji, wizi, kuchoma moto mali, dawa za kulevya, nyara za Serikali, pombe na rushwa.

Mengine ni pamoja na yale yanayohusisha kughushi, noti bandia, wizi wa benki, wizi wa mashirika ya umma na Serikali kuu. 

Ili kupunguza idadi hiyo, Bunge liliitaka Serikali kuanzisha jitihada mbalimbali ikiwemo kushirikisha viongozi wa dini kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya makosa hayo.

“Kwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga jamii yenye maadili isiyo na visasi na tamaa za mali,” amesema Kawawa.

Baaadhi ya vitu vilivyokamatwa wakati wa doria ya polisi iliyofanyika mwezi Desemba mkoani Mwanza.Picha|Mariam John

Mchungaji Imani Mwakanyamale kutoka kanisa la Building the Temple of God (BTG) iliyopo jijini Dar es Salaam, ameiambia Nukta Habari kuwa kanisa ndio suluhisho la mwisho katika kutokomeza uhalifu nchini wakati ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa.

“Imani inabakia kwa msingi wa mwisho wa kubadilisha mtu, sisi kama watu wa imani tunajitahidi kuwafikia watu ili asili yao ya ubinadamu ifikiwe na sauti ya Mungu wabadilike na kuwa watu wema,” amesema Mchungaji Mwakanyamale.

Pia, kamati hiyo imeitaka Serikali itafakari suala la kuanzisha utaratibu wakuwa na viongozi wa nyumba kumi ndani ya mfumo wa serikali za mitaa.

Suala hilo litarahisisha uratibu wa masuala mbalimbali katika jamii ikiwemo ya ulinzi na usalama na majirani kutambuana katika ngazi ya kaya.

Related Post