Majaliwa atua Njombe, atoa maagizo mazito minada ya chai Tanzania
- Aagiza minada ifanyika katika kanda zinazolisha zao hilo na siyo nje ya nchi.
- Wizara ya kilimo yasema itafungua mnada wa chai mkoani Dar es Saalam.
- Majaliwa yuko mkoani humo katika ziara ya kikazi ya siku tatu.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe minada ya kuuza zao la chai katika ukanda wa maeneo yanayozalisha zao hilo ili kuwarahishia wakulima kupata soko la uhakika na kuacha kutegemea minada ya nje ya nchi.
Amesema Serikali itasimamia kikamilifu zao hilo na kuhakikisha wahusika wananufaika kwa kupata soko la uhakika ikiwemo minada ya chai yenye manufaa kwa wakulima.
Wastani wa asilimia 80 ya chai yote inayozalishwa nchini huuzwa kwenye masoko ya nje.
Kati ya hizo wastani wa asilimia 40 huuzwa kupitia soko la mnada wa chai Mombasa nchini Kenya na zilizobaki huuzwa moja kwa moja kwa wanunuzi katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Ujerumani, Pakistani, Falme za Kiarabu, Urusi na Marekani.
“Zao la chai ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao hili huliingizia Taifa zaidi ya Dola za Marekani milioni 60 (zaidi ya Sh139 bilioni) kwa mwaka. Tukiboresha mikakati yetu litatuongezea fedha nyingi zaidi,” amesisitiza Majaliwa leo Machi 10 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe.
Maagizo kwa Mkoa wa Njombe
Aidha, mtendaji huyo mkuu wa Serikali amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie na kuchukua hatua kwa baadhi ya viwanda vya chai vinavyonunua majani mabichi ya chai ambavyo vimekuwa vikichelewesha malipo ya wakulima ahakikishe vinawalipa kwa wakati.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuona zao hilo linapata mafanikio, hivyo amewataka watendaji wafuatilie kuhakikisha wakulima wote wananufaika na zao hilo.
”Lazima wakulima walipwe fedha zao kwa wakati ili waweze kuhudumia mashamba yao na kukidhi mahitaji yao,” amesema Majaliwa.
Kuhusu kuwepo kwa minada ya chai nchini, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es Salaam hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.
Soma zaidi:
- TADB yakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata chai Iringa
- Viwanda vya kuchakata mbaazi kufufua matumaini ya soko kwa wakulima Tanzania
Amesema zao la chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati hapa nchini na kwamba Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili liendelee kuwa na tija kwa wakulima, wenye viwanda na Taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, zao la chai limechangia kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu zaidi ya 50,000 wameajiriwa viwandani na mashambani.
Pia limetoa takribani ajira milioni 2 zisizo za moja kwa moja huku akisema “Idadi hii haitoshi kulingana na ardhi nzuri tuliyonayo.”
Waziri mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji waje nchini kujenga viwanda vya kuchakata zao la chai kwa kuwa nchi ina mazingira mazuri ya uwekezaji na malighafi ya kutosha pamoja na nishati ya uhakika.
Zao la chai kwa hivi sasa linalimwa katika wilaya 12 zilizopo kwenye mikoa sita ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro.
Jumla ya eneo lililopandwa chai ni hekta 22,721 ambapo wakulima wakubwa wana hekta 11,272 na wakulima wadogo hekta 11,449.