Viwanda 3 vya kuchakata mbaazi kufufua matumaini ya soko kwa wakulima Tanzania

October 9, 2018 7:01 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatua hiyo ni kujibu kero ya muda mrefu ya wakulima wa mazao ya mbaazi na choroko kukosa soko la uhakika kwa kuongeza thamani ya mazao hayo hapa nchini.
  • Vinajengwa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro kwaajili ya kutengeneza bidha mbalimbali  zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Huenda wakulima wa Mbaazi na Choroko wakaondokana na kilio cha muda mrefu cha mazao yao kukosa soko, baada ya wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao hayo nchini.

Viwanda hivyo vinatarajiwa kujengwa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro. vitatumia mbaazi na choroko kutoka kwa wakulima kwaajili ya kutengeneza bidha mbalimbali  zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.

Matumaini hayo kwa wakulima yametolewa leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, ambapo amesema kilimo kinategemewa na watanzania wengi na juhudi za kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mbaazi ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda.  

“Kilimo kinategemewa na zaidi ya asilimia 65 ya watanzania, lakini zao la mbaazi limekuwa na matatizo ya soko ndiyo maana Serikali imeamua kuchukua hatua kwa kuwahamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya kusindika mazao hayo hapa hapa nchini, jambo ambalo limeanza kutekelezwa,” amesema Mgumba.

Amebainisha kuwa hatua hiyo ni kujibu kero ya muda mrefu ya wakulima wa mazao hayo katika mikoa ya Manyara, Arusha, Dodoma na maeneo mengine kukosa soko la uhakika kwa kuongeza thamani ya mazao hayo hapa nchini.

“Ukiongeza thamani ya hizi mbaazi unapanua soko katika dunia badala ya kutegemea soko moja tu la nchini India, ambapo sasa mbaazi zitauzwa nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Kiarabu, Ulaya na Marekani” amesisitiza Mgumba.

Amesema hivi sasa viwanda vitatu vya  kuchakata mbaazi vinajengwa mkoani Arusha, Dar es Salaam na Morogoro katika eneo la Mtego wa Simba, huku kiwanda kimoja cha kusindika choroko kikijengwa mkoani Dodoma.


Zinazohusiana:


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dk Ashatu Kijaji amesema Wilaya ya Kondoa ina wakulima wengi ambao wanahitaji kuboreshewa mazingira yao ya kilimo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika pato la Taifa.

“Watu wanasema Kondoa ni vijijini kwa asilimia 100 lakini kwa kasi tunayokwenda nayo, baada ya miaka 5 Jimbo hili litakuwa miji mitupu katika kata zote 21 na kitakachotuvusha kwenda kwenye miji hiyo ni kilimo,” amesema Dk Kijaji.

Bei ya Mbaazi iliimarika katika msimu wa mwaka 2015 ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,800 hadi 3,000 (sawa na 280,000-300,000 kwa gunia la kilo 100) ambapo ilikuwa neema kwa wakulima na msimu uliofuata wa 2016 uzalishaji uliongezeka zaidi lakini matatizo ya soko yakaanza kujitokeza.

Mpaka kufikia msimu wa 2017, inasemekana bei ilishuka hadi Sh150 kwa kilo kutokana na mabadiliko ya bei ya kimataifa na kuathiri wakulima wengi wao zao hilo nchini. Baadhi ya wakulima wamehifadhi shehena ya zao hilo kwenye maghala wakisubiri kupanda kwa bei.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zinazozalisha kwa wingi mbaazi, ambapo asilimia 95 ya zao hilo ilikuwa inauzwa nchini India na sehemu ndogo iliyobaki inatumika kwa chakula.

Enable Notifications OK No thanks