Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano ya Disemba 9

December 5, 2025 6:31 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema maandamano hayo hayajakidhi matakwa ya kisheria na yanaashiria mipango hatarishi inayoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyotangazwa kufanyika Desemba 9, 2025, likiweka bayana kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria na yanaashiria mipango hatarishi kwa usalama wa Taifa.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime, iliyotolewa leo Disemba 5, 2025 imebainisha kuwa maandamano hayo yanayopigiwa chapuo na baadhi ya watu mtandaoni ni kinyume cha sheria ya Tanzania.

“Kuna uhalifu unaoendela kupangwa katika mitandao ya kijamii, na kwenye makundi ya baadhi ya watu wakihamasisha kile wananchokiita maandamano ya amani na yasiyo na kikomo kuanzia tarehe 9 Oktoba 2025…

…Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano hayo yaliyopewa jina la maandamano ya amani yasiyo na kikomo yasifanyike,” imesema taarifa ya Misime.

Taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi ni mfululizo wa tahadhari inayoendelea kutolewa na viongozi wa juu Serikalini kwa wananchi kutoshiriki maandamano hayo yaliyoitishwa nchi nzima.

Maandamano hayo yanaitishwa kwa mara ya pili baada ya yale ya awali kuacha alama kubwa katika maisha ya Watanzania yakisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, mali na vifo vya watu ambao mpaka sasa Serikali haijabainisha rasmi idadi kamili.

Jeshi la Polisi linabainisha kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322, inayomtaka mtu yeyote anayetaka kufanya mkusanyiko au maandamano kuwasilisha notisi ya maandishi kwa Afisa Polisi Msimamizi sharti ambalo bado halijatimizwa.

Pamoja na maandamano hayo, Misime amesema kuwa wamebaini mikakati mbalimbali hatarishi ikiwemo wito kwa watu waliopata mafunzo ya silaha kuzitumia siku hiyo, kusimamisha shughuli za kawaida, kuchoma minara ya mawasiliano, kufunga kwa barabara za kuelekea na kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kufunga kwa mipaka ya nchi.

“Imebainika kuwepo kwa miito ya kupora mali za watu kwa kisingizio cha njaa, kuzuia huduma hospitalini, kuwadhuru watumishi wa Serikali, kutoa vitisho vya kuuawa kwa wanaoweza kuonekana mitaani, pamoja na wito wa kubeba petroli kwenye chupa,” ameeleza Kamanda Misime.

Kwa mujibu wa Misime, mipango hiyo ni viashiria vya wazi vya uvunjifu wa amani, kuhatarisha maisha ya wananchi, kuathiri uchumi, na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi. 

Jeshi hilo limesema linaendelea kufanya uchunguzi likiwataka Wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kulinda amani na utulivu wa Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks