Wafahamu zaidi wanyama hawa adimu Tanzania

October 23, 2019 2:27 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanyama hawa baadhi yao wapo kwenye kundi la wanyama wanaotoweka.
  • Kati ya wanyama hao yupo Mbwa mwitu.

Dar es Salaam. Kuna mambo mengi ambayo mtalii yeyote anatarajia wakati akitembelea mbuga za wanyama na hata vivutio vingine.

Moja kati ya mambo hayo ni kuona vitu vya kipekee ambavyo hajawahi kuviona au hata kusikia kama vipo. 

Kwa kutembelea mbuga za wanyama mbalimbali nchini Tanzania, wapo wanyama ambao watakusahaulisha upekee wa Simba, urefu na maringo ya twiga, ukubwa na uzito wa tembo na hata miruzi na nyimbo za ndege.

Hawa ndio wanyama wa kipekee utakao waona pale utembeleapo mbuga za wanyama za Tanzania.

Wanyama waliohadimika zaidi katika mbuga za wanyama Tanzania. Picha | Mtandao.

1. Mbwa mwitu (African wild dog)

Ukimwangalia kwa haraka, unaweza kumfananisha na fisi lakini ukubwa wa masikio yake na mabaka yake yanaweza kumtofautisha.

Mbwa miwitu anaonekana kwa msimu wa ukame kwenye mbuga ya Tarangire huku takwimu za Mfuko wa Dunia wa kulinda viumbe vya asili (WWF) zikimtaja mnyama huyu kama mmoja wa wanyama walio hatarini kutoweka.

Hadi sasa WWF 2019 inaainisha wanyama hao wamebaki 1,409 huku Tanzania ikitajwa kuwa makazi ya mnyama huyu kati ya nchi chache duniani zikiwemo Msumbiji na Afrika Kusini.

2. Caracal

Tanzania ni miongoni mwa nchi 41 kati ya nchi 54 barani Afrika ambazo zina makazi ya mnyama huyu.

Unaweza kumuita paka kwani miguu yake, masikio yake na hata macho yanasadifu jina lake. Manyoya yake yenye rangi kama ya simba na masikio yake yaliyopambwa na manyoya ya ziada ni sehemu tu ya vitu vidogo vitakavyo kuacha ukitaka kumtazama tena na tena.

3. Fisi mwenye michirizi

Kwanza kabisa mnyama huyu ana mionekano miwili kwa mwaka. Wakati wa joto, fisi huyu huwa na manyoya mafupi na manyoya hayo huongezeka urefu wakati wa baridi.

Kumuona mnyama huyu, unahitaji kuweka kambi usiku kwani aibu zake humfanya kutembea wakati wa giza tuu. 

Fisi huyu ambaye anaweza kuishi kwa miaka 12 anapatikana Kaskazini na kusini mwa Afrika pekee.

4. Tumbili Colobus (Black and White Colobus Monkey)

Tumbili huyo mwenye rangi mbili yaani nyeupe na nyeusi atakustaajabisha na nywele zake za singasinga.

Ajabu zaidi, nywele hizo hazipo kichwani bali kwenye mgongo wake. Mnyama huyu huonekana kwa nadra kwani hujificha kwenye msitu mnene lakini unaweza kumbahatisha kandokando ya Mto Grumeti kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Michezo ya mnyama huyu itakufanya uzidi kumstaajabu na kujikuta badala ya kumaliza safari nzima unaweza kutamani umtizame akicheza na wenzake hadi pale jua lizamapo. 

5. Digidigi

Tofauti na wanyama wengine, digidigi jike ni mkubwa kuliko dume. Mnyama huyu ambaye uzito wake ni kuanzia kilo tatu hadi sita anapatikana zaidi Afrika Mashariki hasa nchini Tanzania na Somalia. Pia, anaweza kupatikana Namibia na Angola.

Huku wengi wakimfananisha na swala, tofauti yake na swala ni udogo wake na sauti ya ziki-zik au dik-dik anazozitoa kwenye pua zake akiwa anakimbia.

Jina lake linatokana na sauti hiyo na kasi yake ni kilometa  67.5 kwa saa na kati ya nchi 54 barani Afrika, digidigi anapatikana kwenye nchi sita tu na Tanzania ikiwemo.


Zinazohusiana:


Orodha bado inaendelea. Nukta.co.tz itaendelea kukujuza zaidi.

Enable Notifications OK No thanks