Tanzania: makao ya wanyama wasiopatikana kirahisi duniani

October 29, 2019 3:13 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Chura wa kihansi ambao wamefungamana na bonde la Kihansi ni sehemu tu ya upekee wa Tanzania
  • Kisukuku, nguva na papa potwe huyapamba maji ya Tanzania kwa misimu tofauti.
  • Wanyama hao wamekuwa kivutio kikubwa cha utalii na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

Dar es Salaam. Baada ya kukuletea wanyama adimu wa mbugani juma lililopita, Nukta Safari inakusafirisha kukutoa kwenye viumbe vya ardhi hadi viumbe vya majini.

Huenda ni kawaida kwako kumuona pweza akiteleza kwenye mapango ya bahari ya Hindi au ngadu akikimbia upande upande lakini, inaweza ikawa ni nje ya matarajio kufahamu kuwa Tanzania ni makazi ya viumbe ambavyo huenda hujawahi kufikiri kama vinaishi?

Kabla ya kupiga mbizi na kuingia baharini, wafahamu viumbe hawa wa majini kwa upekee wake.

Chura wa kihansi (Kihansi spray toad)

Chura huyo amefungamana na mazingira ya bonde la Kihansi nchini Tanzania ambapo hali ya mvuke unaotokana na kutiririka maji kwenye bonde hilo inamfanya kuishi kwenye mazingira hayo tu huku akiipamba ardhi hiyo na rangi ya njano na kahawia.

Udogo wa chura huyu huenda ukawafanya watu wanaoogopa wadudu na viumbe wadogo kuondokana na hofu hiyo kwani chura dume hukua hadi sentimita 1.9 na jike kwa sentimita 2.9.

Chura wa kihansi hukaa na mayai yake tumboni na yakishaanguliwa, huwatoa watoto wake kana kwamba anazaa. Picha| Mtandao.

Tofauti na chura wengine, chura wa kike wa jamii hii hukaa na mayai yake tumboni na yakishaanguliwa, huwatoa watoto wake kana kwamba anazaa. Kamwe,huwezi kuyaona mayai yake na hauna haja kwani upekee wa miguu yake utakuondolea hata wazo la kuyatafuta.


Fahamu: 

  • Chura wa jamii nyingine hutaga mayai na kisha kuyaacha majini ambapo huanguliwa pale muda unapofika.
  • Chura huyo amewekwa kwenye kundi la viumbe wanaotoweka na Shirika la Kimataifa la Utunzaji wa Mazingira (IUCN) 

Wakati ukitafakari hayo, umewahi waza kuwa maji ya mipaka ya Tanzania pia yana uhifadhi wa viumbe adimu na hata ambavyo vilidhaniwa kuwa vimetoweka? Basi bado wapo Tanzania

Silikanti (Coelacanch)

Akieleza juu ya kiumbe huyu, Lydia Mwakanema ambaye ni Afisa Programu za viumbe maji kutoka Mfuko wa Wanyamapori Duniani (WWF) amesema “katika orodha ya viumbe waliopotea duniani walikuwa wameorodheshwa kwamba hao viumbe ni distinct (wametoweka).”

Lakini ajabu ni kwamba wavuvi nchini Tanzania walivua samaki wasio muelewa na hivyo kumpeleka kwenye ofisi za mamlaka hiyo na baada ya mawasiliano kufanyika na watafiti wengine, mshangao ulitawala kumuona samaki huyo aliyeaminika kutoweka kwamba bado anaishi. 

Kwa Tanzania, Silikanti au kisukuku anapatikana kwenye bahari ya hindi hasa  mkoa wa Tanga. 

Kwa mujibu wa Mwakanema, samaki huyo hupenda kukaa kwenye maji ya kina kirefu hivyo huihitaji mitambo mingi ikiwemo kamera, tochi na vifaa vya kuogelea kumtazama. 


Zinazohusiana


Papa potwe (Whale shark)

Papa huyu ambaye kwa sifa za jamii yake ana tabia ya kuhama hama. Amewasahihisha waliompatia sifa hiyo kwani anapatikana katika visiwa vya Mafia vilivyopo mkoa wa Pwani huku ndiyo nyumbani kwake. 

Licha ya ukubwa wa bahari ya Hindi, Potwe ambaye kawaida ana ukubwa wa mita 13 hadi 18, hajawahi kuonekana popote zaidi ya Mafia.

Mwakanema anaeleza kuwa papa huyo ni kivutio cha utalii ambacho kinaonekana kwa wingi na kuipamba bahari ya Mafia msimu ambao maji huwa na vuguvugu na pale yanapokuwa ya baridi, hutokeza lakini siyo kwa wingi sana.

“Kuna msimu hata ukikaa tu pale pwani Mafia unawaona. Kimekuwa ni kivutio cha utalii hasa kwenye kisiwa cha Mafia. Amekuwa chanzo kikubwa cha kipato hasa kwenye wilaya ya Mafia,” amesema Mwakanema

Nguva (Dugong)

Ndiyo! hata mimi sikuwa na picha ya samaki huyu kama nguva. Mbali na taswira ya nguva iliyojengeka kwenye vichwa vya watu wengi, hiyo ndiyo taswira halisia kwani usitegemee nywele ndefu na nusu ya kiwiliwili chake kuwa kama binadamu.

Samaki huyu anapatikana kwenye maji ya kisiwa cha Mafia pia kwa Tanzania ambapo aliwahi kuvuliwa na wavuvi ambao walimpeleka pwani.

“Nguva akionekana inakuwa ni stori kubwa” amesema Mwakanema ambaye amethibitisha kuonekana kwa samaki huyu siyo kwa urahisi.

Nguva akionekana inakuwa ni stori kubwa” amesema Mwakanema. Picha| mtandao.

Mbali na rangi yake ya kijivu, nguva anaweza kufikia uzito wa  hadi kilogramu 400 huku wakipenda kukaa kwenye maji ya kina kirefu kwa sababu chakula chao kinapatikana kwenye sakafu ya bahari.

Serikali na taasisi za kimataifa zinafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Tanzania inahifadhi urithi wake asilia ambapo wamefanya uhifadhi wa wanyama mbalimbali akiwemo kutenga maeneo tengefu yanayolindwa ili kuhakikisha wanyama hao wanakuwa salama.

Kama una mpango wa kuwaona wanyama hao, basi tembelea kisiwa cha Mafia ili kujionea fahari hiyo ya Tanzania.

Enable Notifications OK No thanks