Sasa utaweza kujitoa makundi ya Whatsapp bila kujulikana

David Mselewa 0808Hrs   Agosti 10, 2022 Teknolojia
  • Ni baada ya mtandao huo kufanya mabadiliko ili kuimarisha faragha za watumiaji wake.
  • Wenzako katika kundi hawatajua kama umejitoa.

Dar es Salaam. Umechoshwa kuulizwa kwa nini utajiondoa katika baadhi ya makundi ya WhatsApp? Basi ondoa shaka kwa sababu hutaulizwa tena.

Kampuni ya Meta inayomiliki Whatsapp imesema kutakuwa na mabadiliko ya faragha kwa watumiaji wake yatakayowawezesha kujitoa kwenye makundi ya mtandao huo bila kujulikana kama wamejiondoa.

Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo akizungumza wiki hii, Mark Zuckerberg amesema mabadiliko hayo yatasaidia kulinda na kutunza faragha za mtumiaji.

Hivi sasa katika mtandao huo endapo mtumiaji atajitoa katika kikundi alichopo wanakikundi wote watajua kama kuna mtu amejitoa na hivyo kila mmoja kumtafsiri kivyake.

Kwa mabadiliko hayo ya Meta, endapo mtumiaji atajitoa kwenye kikundi ni kiongozi au viongozi wa kikundi hicho cha Whatsapp ndiyo watakaojulishwa kuwa kuna mwanakikundi amejitoa.

Mkuu wa kitengo cha bidhaa wa Meta,  Ami Vora amebainisha kuwa mtandao huo wa mawasiliano unalenga kumpatia mtumiaji uwezo wa kudhibiti faragha zake anapotumia mtandao huo.

Mbali na mabadiliko hayo yanayotarajiwa hivi karibuni,  mabadiliko mengine ni mtumiaji kuruhusu namba ambazo zinaweza kumuona pale anapokuwa hewani kuliko hivi sasa ambapo mtu yeyote anaweza kukuona kupitia simu yake kama upo hewani.

Related Post