Maarufu Muyaga: Kutoka kuuza sabuni hadi kuibuka na app ya kurahisisha sherehe Tanzania

February 2, 2021 8:43 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupitia changamoto lukuki wakati wa kufunga ndoa yake miaka miwili iliyopita.
  • Programu hiyo (App)  imekusanya watoa huduma wanaohusika na shughuli za sherehe ikiwemo harusi.
  • Wadau wamesema itarahisisha upatikanaji wa watoa huduma wakati wa sherehe. 

Dar es Salaam. Iwe “kitchen party”, sherehe ya kumuaga mwali (send off) na hata harusi, watu wengi huumiza kichwa kuwapata watu watakaosimamia sherehe hizo na kuhakikisha mahitaji yote yanapatikana.

Kuanzia chakula kizuri, vinywaji, mapambo, wapiga picha, keki, mshereheshaji, ukumbi na mengine mengi ni vitu muhimu katika sherehe za kitanzania na endapo wenye sherehe watabeba jukumu la kusimamia kila kitu, basi wataishia kuumwa vichwa katika siku ya tukio.

Kuitambua changamoto hiyo, Mtanzania Maarufu Muyaga ameibuka na programu tumishi ya simu (App) ambayo inawasaidia waandaaji wa sherehe kupata huduma zote katika viganja vya mikono yao. 

Programu hiyo inayojulikana kama Nderemo inasaidia inakusogezea karibu watoa huduma mbalimbali wa sherehe wakiwemo wapishi, wapambaji na hata washehereshaji. 

Hivyo ni kusema hautakiwi kuumiza kichwa kufanikisha sherehe yako, zaidi kuingia kwenye programu hiyo ambayo unaweza kuipate kwenye simu janja na kupata kila kitu unachokihitaji kulingana na bajeti ya sherehe yako

Muayaga alianza safari ya kutafuta suluhu hiyo kiteknolojia baada ya kupata changamoto wakati anafunga ndoa yake mwaka April 2019.

“Kipindi nataka kuoa, nilipata tabu sana kuwapata watoa huduma. Mtu wa mapambo nilimfuata Temeke kwa Aziz Ally na wa chakula nilimfuata hadi Kigamboni kwa ajili ya kufanya mazungumzo,” amesema Muyaga ambaye kipindi hicho alikua akiishi Magomeni jijini Dar es Salaam.

Haikuishia hapo Muyaga aliendelea na safari ya kutafuta washereheshaji kupitia mtandao wa Instagram huku akitumia gharama kubwa za mawasiliano na usafiri kuwapata watoa huduma hao.

“Haikuwa rahisi,” amesema Muyaga wakati akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuhusu utendaji wa app ya Nderemo. 

Changamoto hii siyo kwa Muyaga pekee imeenda hadi kwa Lucy Protas ambaye alikuwa na sherehe yake mwishoni mwa mwaka 2020 ambapo alitumia gharama kubwa kufanikisha sherehe yake kwa sababu hakuwa na njia mbadala ya kuwapata watoa huduma. 

“Gauni la kawaida tu ambalo malighafi yake yanaweza gharimu Sh150,000 watakutengenezea kwa gharama ya hadi Sh800,000 hadi Sh1.5 milioni,” amesema Lucy ambaye ni mwanzilishi wa jukwaa ‘Sport for Change’.

Changamoto hizo wakati wa sherehe siyo tu zimewapata Lucy na Muyaga, bali zinaendelea kuwapata Watanzania ambao maono yao ni kuona sherehe zao zinajawa na furaha. 

Lakini sasa wamepata suluhisho katika viganja vya mikono yao.

App ya Nderemo hadi sasa imepakuliwa na watu zaidi ya 100 huku ikiwa na watoa huduma zaidi ya 150 waliojisajiri katika apphiyo. Picha| Maarufu Muyaga.

Mwanzo wa safari ya suluhisho

Akishirikiana na wenzake ambao ni Amrani Nyamwita, Buliba Magambo na Musa Kambe, Muyaga alianza mchakato wa kutengeneza programu ya Nderemo mwishoni mwa mwezi Septemba, 2020. 

Kwa timu ya watu hao wanne na michango ya ndugu,  jamaa na marafiki, Nderemo iliweza kuzinduliwa rasmi Disemba 15, 2020 kwa ajili ya majaribio.

“Ujumbe kuhusu kuzinduliwa kwa app yetu tuliutuma kupitia WhatsApp status ili kupata maoni kutoka kwa watu wa karibu yetu. Ndani ya siku tano, App ilipakuliwa na watu zaidi ya 100,” amesema Muyaga.


Nini kipya katika app ya Nderemo?

Kwa Tanzania, hii ni app ya kwanza kutoa huduma za sherehe mtandaoni ambayo inapatikana katika duka la mtandaoni la “Play Store linalomilikiwa na kampuni ya Google ya Marekani. Hapo anaweza kuipakua na kuitumia muda wowote.

Tofauti na app zingine, app hii haihitaji taarifa zako kama mteja lakini kama mtoa huduma, utahitajika kutoa taarifa zako ili wateja wafahamu taarifa zako zikiwemo namba ya simu, jina la biashara na picha za kazi zako.

“Tunajaribu kumuondolea mteja vikwazo katika kutumia app. Tofauti na app zingine zinazohusisha mtoa huduma na mteja, app ya Nderemo ni hiyo hiyo, hivyo mtu akiwa mteja ataitumia kama mteja na mtu akiwa mtoa huduma atatumia app hiyo hiyo kama mtoa huduma.

“Na hata pale mtoa huduma atakapohitaji huduma kutoka kwa mtu mwingine, anaweza kuitumia app hiyo hiyo kama mteja,” amefafanua Muyaga

Baada ya kufungua app ya Nderemo, utakutana na vipengele vikiwemo washereheshaji, wapiga picha, watengeneza keki, wapambaji na watu wote wanaohusika na huduma za sherehe.


Uwezo wa kuchanganuliwa bajeti yako

Katika app ya Nderemo, unaweza kuweka bajeti yako na huduma ambazo utazihitaji kukamilisha sherehe yako kisha app ikakuchanganulia watoa huduma ambao wataendana na bajeti yako.

Mfano endapo bajeti ya harusi yako ni Sh10 milioni, utaandika bajeti hiyo kwenye kipengele cha bajeti na kisha kuchagua huduma ambazo utazihitaji mfano chakula, keki, ukumbi na mapambo.

App hiyo itakuonyesha watoa huduma wote ambao wanaweza kuendana na bajeti yako. Na hivyo kukuondolea usumbufu wa kuanza kuwatafuta  watoa huduma ambao hauwezi kuwalipa.

Kipengele hicho kimerahisisha mahesabu kwa mwenye sherehe huku kikiokoa muda.

Faida zinazoambatana na programu hiyo

App hiyo ambayo hadi sasa imepakuliwa na zaidi ya watu 100 inampatia mteja mawasiliano ya watoa huduma ikiwemo namba za simu na imeunganishwa na mtandao wa WhatApp endapo mteja atahitaji mazungumzo na mtoa huduma.

Baadhi ya watu walioanz akutumia app hiyo akiwemo Shebby Sk wamesema ni programu nzuri kwa sababu inaokoa gharama na inamuwezesha mtu kukamilisha sherehe yake kwenye simu. 

“Ni app nzuri sana na inatoa msaada wa kuwapata watoa huduma tena wenye bei nafuu,” amesema Sk akitoa maoni yake kuhusu programu hiyo. 

Hata hivyo, waanzilishi wa app hiyo watakua na kibarua cha kuhakikisha inatumika katika simu zote ili kuwafikia watu wengi katika maeneo mbalimbali Tanzania. 


Hadi sasa Nderemo imefikia wapi?

Safari ya matumaini ya app ya Nderemo imeendelea kuwatia moyo Muyaga na wenzie hasa baada ya watoa huduma zaidi ya 150 wa jijini Dar es Salaam na mikoa mingine kujiunga na mfumo huo ndani ya takriban miezi miwili tu tangu uzinduzi rasmi wa app hiyo.

“Ninamshukuru Mungu kuwa tunakua kila siku. Kwa sasa app hii ipo Tanzania pekee licha ya kuwepo wadau wengine nchi za jirani wanaohitaji kuitumia,” ameeleza Muyaga wakati akiongea na Nukta Habari.

Hadi sasa Nderemo imetoa ajira kwa watu watano akiwemo Muyaga ambaye ndiyo Mkurugenzi na wenzake wanne huku wakitaka kuiona app hiyo ikiwafikia watu wengi ndani na nje ya nchi.


Soma zaidi:


Bado haijaanza kuingiza fedha

Kila mtu anayeanzisha biashara, kampuni na huduma ana matazamio ya kitu hicho kukua, kufahamika na kusaidia watu wengi iwezekanavyo kwani hayo ndiyo mafanikio.

Kwa Nderemo, Muyaga amesema licha ya kuwa imemgharimu takriban Sh10 milioni kufikia hapo ilipo, bado haijaanza kumuingizia faida lakini anaamini ni kitambo tu yote hayo yatawezekana.

“Kwa sasa ndiyo tunaanza na sisi tunaamini fedha zipo kwa watu. Kwa sasa umakini wetu upo katika kulikuza jina la Nderemo na tunajua ndani ya muda mfupi pesa zitaanza kuja,” amesema Muyaga.

Kijana huyo ametoa wito kwa vijana kuacha kuchagua kazi, kujituma na kuamini kuwa maisha siyo rahisi kama kuchukua pipi kutoka kwa mtoto.

Amesema licha ya kuwa ana na shahada ya manunuzi na usafirishaji lakini safari yake ya kutengeneza app hiyo haikua rahisi kwa sababu alianza kuuza sabuni, gesi na kufanya shughuli ndogo ndogo za kumuingizia kipato.

Enable Notifications OK No thanks