Kwanini makosa ya ubakaji yanaongezeka Tanzania?

Rodgers George 0114Hrs   Agosti 06, 2020 Ripoti Maalum
  • Makosa ya ubakaji yameongezeka kwa takriban asilimia 3 ndani ya mwaka mmoja.
  • Ukosefu wa maadili, mitandao ya kijamii vyachangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.
  • Jamii yatakiwa kuwalinda watoto wa kike. 

Dar es Salaam. “Ninamfahamu binamu yangu mwenye miaka saba ambaye alibakwa na binamu yetu mwingine mwenye miaka 20,” Sikuzani* mkazi wa Dar es Salaam anasimulia namna ambavyo binadamu yake alivyobakwa nyumbani na ndugu yake mwingine wa karibu. 

Sikuzani, ambaye si jina lake halisi akihofia kusumbuliwa na ndugu, ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa binamu yake wa kiume mara nyingi alikuwa akimuita binamu yake wa kike mwenye miaka saba chumbani wakati hakuna watu wengine.

Wakiwa chumbani, anasimulia kuwa kijana huyo alikuwa akimlazimisha binti huyo kumkanda (massage) na kisha alikuwa akimbaka na kumuacha na binamu yake mwingine mwenye umri unaokaribiana na ule wa mtoto huyo wa kike. 

“Haikuwa mara moja...msichana wa kazi alikuwa akifua chupi za mtoto na kuzikuta na damu mara nyingi tu naye alionekana kuwa mwathirika kwani bila kuambiwa ni nini kilimkuta, alimuambia asipende kwenda chumbani kwa yule kijana,” anasema Sikuzani.

Kwa mujibu wa Sikuzani, wazazi wa familia hiyo hawakuwahi kufahamu lolote linaloendelea nyumbani pale wanapokuwa hawapo kwani hata mfanyakazi hakuwaambia waajiri wake na badala yake aliamua kuwashirikisha majirani.

“Majirani ndio walitoa taarifa ustawi wa jamii ambao walimfuata mtoto shule na kumpeleka hospitali. Majibu yalithibitisha vitendo vya ubakaji na mtoto tayari alikuwa amepata fangasi kwenye sehemu zake za siri...alikuwa akilalamika kuumia,” anaelezea Sikuzani.

Kinachomuumiza zaidi Sikuzani ni kuwa mtuhumiwa wa vitendo hivyo alifikishwa kwenye kituo cha polisi lakini baada ya siku 14, alirejea nyumbani huku kesi ikiwa haijafika hata mahakamani.

“Nasikia familia yake ilimhamishia Arusha. Sasa hivi shangazi zangu wote hawaongeleshani. Mama wa mtoto alisema amemuachia Mungu,” anasema Sikuzani huku akionyesha kugadhabishwa na jambo hilo lililotokea mwaka mmoja uliopita.

Ubakaji unaongoza kwa kuwa na makosa mengi zaidi dhidi ya mtu (offenses against person) ukiacha nyuma makosa ya mauaji yaliyoripotiwa ndani ya miaka mitano (2015-2019). Picha| Noi polls.

Mtoto huyo wa miaka saba ni miongoni mwa wasichana na wanawake wanaofanyiwa ukatili huo wa kijinsia Tanzania ambao baadhi ya makosa yake huripotiwa katika vyombo vya dola na mengine humalizwa kifamilia kama tukio hilo. Makosa ya aina hiyo yanaendelea kushamiri. 

Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania mwaka 2019 (Tanzania in Figures 2019) ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inaeleza kuwa makosa ya ubakaji yaliyoripotiwa nchini yameongezeka kwa asilimia 2.8 hadi 7,837 mwaka jana kutoka 7,617 mwaka 2018. 

Hii ni sawa na kusema kuwa wastani wa makosa 21 ya ubakaji yaliripotiwa kwa siku Tanzania mwaka 2019. Wanaofanyiwa vitendo hivyo si takwimu tu kama ambavyo baadhi hunukuu bali ni watoto, dada, shangazi au mama zetu. 

Licha ya kuwa makosa ya ubakaji kuongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, makosa hayo yamekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka kwa miaka mitano iliyopita, jambo linalowawia vigumu baadhi ya wachambuzi kutabiri iwapo yatashuka hivi karibuni au la. 

Katika kipindi hicho, mwaka 2017 ndiyo kulikuwa na kiwango cha juu zaidi cha makosa ya ubakaji baada ya kurekodiwa makosa 8,039. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mwezi Juni mwaka huu na NBS, ubakaji unaongoza kwa kuwa na makosa mengi zaidi dhidi ya mtu (offenses against person). 

Mfano, mwaka 2019 mamlaka zilirekodi makosa mengi zaidi ya ubakaji kuliko mengine yakifuatiwa na makosa ya mauaji huku usafirishaji binadamu ukirekodi matukio machache zaidi. Katika mwaka huo, makosa sita kati ya 10 (asilimia 64) dhidi ya mtu yalikuwa ni ya ubakaji kati ya jumla ya makosa 12,223. 

Kanuni ya Adhabu (Penal Code) ya mwaka 2002 na Sheria ya Makosa ya Kujamiana ya mwaka 1998 zinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye mahakama itamtia hatiani kwa ubakaji atafungwa jela maisha. 

Iwapo mahakama itaona vyema kutoa adhabu ya kifungo basi kifungo hicho kisiwe chini ya miaka 30 na mkosaji atatakiwa kupewa adhabu kali na kutoa fidia kwa mtu aliyembaka (muathirika) katika kiwango kitakachoamuriwa na mahakama kulingana na athari alizozipata aliyebakwa.

Pamoja na adhabu hizo kali bado makosa ya ubakaji yanaongezeka.  


Kwanini matukio ya ubakaji yanaongezeka? 

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa amesema kuongezeka kwa makosa ya ubakaji, haina maana ya kuwa mamlaka hazichukui hatua dhidi ya vitendo hivyo.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu amesema ongezeko hilo linasababishwa na vyombo vya habari kuzipa kipaumbele habari hizo na watu wamekuwa na mwamko wa kutoa taarifa za ubakaji katika vyombo vya dola.

“Huenda sasa hivi utoaji taarifa dhidi ya vitendo hivyo ni mkubwa kuliko zamani. Siyo ajabu ukakuta zamani watu walikuwa wakibakwa sana kuliko hata sasa,” amesema Ole Ngurumwa.

Baadhi ya tafiti zinaeleza kuwa mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, wazazi/ walezi kukosa muda wa kutosha wa kukaa na watoto kuwafundisha maadili mema na mila potofu kwa baadhi ya makabila kuona kuwa mwanamke ni chombo kinachoweza kutumika kwa namna yeyote ile ni baadhi ya vitu vinavyochochea ubakaji.

Wanaofanyiwa vitendo hivyo si takwimu tu kama ambavyo baadhi hunukuu bali ni watoto, dada, shangazi au mama zetu. Picha| The Guardian Nigeria. 

Ritha Tarimo, mwanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia, ameiambia Nukta (www. nukta.co.tz) kuwa idadi hiyo ya makosa ya ubakaji inaweza kuwa ndogo kwa sababu yapo matukio ya ubakaji ambayo hayaripotiwi polisi, jambo linalowafanya waathirika kukosa msaada na kuendelea kuteswa.

“Ninafahamu kuwa kuna idadi kubwa ya kesi ambazo haziripotiwi kama ilivyo. Ninafikiri vitu hivi vinaanzia ngazi ya familia. Watoto wanateseka mikononi mwa wazazi wao,” amesema Ritha ambaye pia ni mmiliki mwenza wa shule ya awali na msingi ya Stars ya jijini Arusha. 

Amesema kutokana na baadhi ya watu kuogopa kuchekwa au kuharibu uhusiano na marafiki na hata ndugu zao, hufumbia macho vitendo vya ubakaji kwa kumaliza kesi hizo kwa mashauriano. 

“Watoto wanabakwa majumbani kwao lakini huwezi kulisikia. Wanaambiwa kuficha, wasilijadili na yeyote,” amesema Ritha.

Ubakaji wamkwaza kila mtu

Wengi wanaelewa madhara na maumivu yanayowapata waathirika wa ubakaji lakini ni wachache hupata ushujaa wa kuripoti matukio hayo kwa vyombo vya dola licha ya kukwazika, tabia inayorudisha nyuma vita ya kutokomeza vitendo hivyo.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam Shinuni Masoud anasema anafahamu kuwa ubakaji ni kumuingilia kimwili kwa nguvu mwanamke, ukatiri ambao huacha majeraha kwa waathirika. 

“Uwii! Uwi! huwa najisikia vibaya sana nikisikia mwanamke au msichana amefanyiwa hivyo. Sipendi yamkute mtu yeyote,” amesema Shinuni huku akionyesha kutopendezwa na vitendo hivyo. 


Zinazohusiana:


Si wote wanaamini ubakaji ni matokeo ya hulka za mhalifu. 

Taurus Mangi mkazi wa Dar es Salaam ameiambia Nukta kuwa mtazamo wake ni kwamba miongoni mwa sababu za ubakaji ni imani za kishirikina na tamaa za watu.

“Ubakaji unaotokana na tamaa hufanyika majumbani na watoto wanafanyiwa vitendo hivyo na ndugu wa karibu sana. Hapa ninachoweza kusema ni kwamba kukaa nyumbani na kufuga ndugu wasio na kazi ni kuhatarisha maisha ya watoto wako,” amesema Mangi. 

Hofu ya Taurus kuhusu kuhusika kwa baadhi ya ndugu wa karibu katika matukio hayo ya ubakaji na mengine ya ukatili wa kijinsia kwa watoto huenda ina mashiko. 

Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa zaidi ya robo tatu au asilimia 85 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalikuwa ni ya ukatili wa kingono, hasa ubakaji na ulawiti. 

Waathirika wengi wa ukatili huo walikuwa ni watoto wa shule za msingi wenye umri wa kati ya miaka saba hadi 14. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, katika mwaka huo, mmoja wa watoto waliobakwa alikuwa ana umri wa miaka miwili.

“LHRC ilikusanya matukio matatu ya watoto ambao walibakwa na baba zao! Matukio saba kati ya matukio ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto yaliyokusanywa na LHRC yalihusu ubakaji na ulawiti wa watoto wenye umri wa mwaka mmoja hadi sita,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya LHRC

Usikose kusoma sehemu ya pili na ya mwisho ya makala haya. Katika sehemu ya pili tutaangazia athari za ubakaji na hatua zinazochukuliwa na mamlaka ikiwemo mikakati ya Jeshi la polisi kutokomeza vitendo hivyo. Maoni tuandikie kupitia maoni@nukta.co.tz 

Related Post