Jilinde dhidi ya ongezeko la mafuta mwilini kuepuka gharama kubwa za matibabu
- Sio kila mafuta yaliyopo mwilini ni mabaya.
- Mtindo wa maisha una mchango katika kuwa na lehemu nzuri au mbaya mwilini.
- Ufanyaji mazoezi na ulaji wa chakula kizuri husaidia kuongeza kiwango cha lehemu nzuri mwilini.
Dar es Salaam. Kati ya mambo ambayo yamekua yakiendelea kuwasumbua binadamu kwa magonjwa na gharama zisizo za lazima ni pamoja na mtindo maisha. Ulaji wa mtu pamoja na ufanyaji mazoezi unaweza kuchangia kwenye ongezeko la lehemu ama kupunguza lehemu hiyo mwilini na hivyo kuathiri afya yake.
Lehemu (Chorestral) ni aina ya mafuta yapatikanayo ndani ya mwili wa binadamu katika seli hai zote za mwili.
Hata hivyo, wingi na usawa wa lehemu kwenye mwili una maana kwani mwili wa binadamu unahitaji kiwango fulani cha lehemu ili kutengeneza vitu kama homoni, vitamini D na baadhi ya vitu vinavyosaidia katika mmen’genyo wa chakula.
Kutokana na mtindo maisha, baadhi ya watu hujikuta na ongezeko kubwa la lehemu mwilini na hivyo kuingia kwenye matatizo ikiwemo magonjwa ya moyo pamoja na kiharusi.
Mfiziotherapia, Dk Joshua Sultan ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Tiba na Afya cha KCMC Mosh anasema kuna lehemu nzuri na lehemu mbaya na leo anazungumzia lehemu nzuri na kisha kukuletea sehemu ya pili itakayoongelea lehemu mbaya na jinsi ya kujilinda nayo.
Chakula kizuri kama mboga za majani, korosho, karanga, mboga jamii ya kunde na hata mboga za mimea husaidia kuongeza kiwango cha lehemu nzuri mwilini. Picha| Mtandao
Je, Lehemu nzuri ni ipi?
Sultan anasema lehemu nzuri (High Density Lipoproteins) hupatikana kwenye mwili wowote wa binadamu na yenyewe huzunguka kila wakati ikizitafuta lehemu mbaya. Faida ya lehemu nzuri ni pamoja na kun’gamua lehemu mbaya, kisha ikajifunga nazo na kuzipeleka kwenye ini ambapo huchujwa na kuondoa madhara katika mwili.
Uwepo wa lehemu nzuri mwilini ni kitu kizuri kwani itasaidia kumuepusha mtu na magonjwa ambayo yanatokana na uwepo wa lehemu mbaya mwilini.
“Ukiwa na kiwango kikubwa cha aina hii ni vizuri, kwani unapokuwa na kiwango kidogo unajiweka katika hatari ya kupata matatizo maana lehemu mbaya huzidi,” amesema Joshua.
Kuwa na aina hii ya lehemu ni rahisi kwani mtindo wa maisha wa binadamu yeyote kama ukiwa sawa basi ana uwezo wa kuwa na aina hii ya mafuta mwilini.
Zinazohusiana:
- MSD yashauri vituo vya afya kununua mfuko maalum kwa wajawazito
-
Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
-
Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani
Sultan amesema ufanyaji mazoezi ya japo dakika 30 kila siku na ulaji wa chakula kizuri kama mboga za majani, korosho, karanga, mboga jamii ya kunde na hata mboga za mimea husaidia kuongeza kiwango cha lehemu nzuri mwilini.
“Kiwango cha lehemu hii hutakiwa kua katika kiwango maalumu cha kawaida kwani lehemu inapozidi katika mwili huleta madhara anuai,” amesema Sultan na kuongeza kuwa hamna dalili za wazi za kuonyesha au kuashiria ongezeko la lehemu mwilini na hivyo ni vizuri mtu kujiwekea ratiba ya kufanya vipimo vya lehemu kwani jinsi ya kujua kiasi cha lehemu mwilini ni kwa njia ya vipimo pekee.
Je lehemu mbaya ni ipi?, ina madhara gani? Fuatilia mwendelezo huu kupitia www.nukta.co.tz katika makala ijayo.