MSD yashauri vituo vya afya kununua mfuko maalum kwa wajawazito

Zahara Tunda 0543Hrs   Agosti 24, 2018 Habari
  • Mfuko huo unahusisha vifaa vyote muhimu vya kujifungulia.
  • Ni wakati wa vituo vya afya vya serikali kununua kifurushi cha vifaa vya kujifungulia kurahisisha huduma.
  • Wadau waipongeza serikali kwa kugawa vifaa vya kujifungulia bure.

Dar es Salaam.   Katika kuhahakisha vifo vya wajawazito na vichanga vinapungua nchini, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imevitaka vituo vya afya kuhakikisha vinaagiza na kununua mifuko ya vifaa vya kujifungulia kwa wakati kulingana na upatikanaji wa bajeti ya afya. 

Kauli hiyo imekuja miezi mitano baada ya Boharia ya Dawa kuzindua mfuko maalum wa vifaa vya kujifungulia kwa wajawazito vinavyopatikana bure katika vituo vya afya. 

Akizungumza na Nukta, Afisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka amesema kazi yao ni kusambaza mifuko hiyo na vituo vya afya vina jukumu la kuagiza na kununua kwa kutumia utaratibu uliopo ili kuhakikisha mifuko hiyo inapatikana wakati wote.

“Ili mifuko ya vifaa vya kujifungulia vipatikane ni wajibu wa kituo cha afya husika kununua vifaa hivyo au kuagiza kulingana na bajeti na mahitaji yao,” amesema Kusiluka.

Kulingana na mwongozo wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wanawake wanaoenda kujifungua kwenye vituo vya afya wanapaswa kupewa huduma zote bila malipo ikiwemo vifaa vya kujifungulia.

Mfuko huo hujumuisha vifaa 12 ikiwemo mipira ya mikono, taulo ya kike ya wazi, pamba kubwa, nguo ya mtoto, vibana kitovu, mpira wa kuzuia uchafu, nyembe za kujifungulia, nyuzi za kushonea, bomba la sindano na dawa ya kuongeza uchungu.

Wakati mwingine vituo vya afya vinachelewa kuagiza vifaa hivyo kutokana na ufinyu wa bajeti na matokeo yake wajawazito wanalazimika kununua vifaa hivyo kwenye maduka ya watu binafsi ambapo huleta usumbufu na hatari ya mama mjamzito na mtoto kufariki kwasababu ya kukosa huduma. 

“Mifuko inapatikana kwa kutoa oda na tutaendelea kuagiza ili kufuata sera ya serikali kuhusu kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga,” amesema Kusiluka.

 Kwa mujibu wa MSD, mfuko huo hauuzwi kwa mtu mmoja mmoja bali hupatikana katika vituo vya afya vya umma na hospitali maalumu zilizopewa kibali na Wizara ya Afya.

Mpaka sasa mifuko 500,000 imesambazwa na MSD katika maeneo mbalimbali nchini ambapo mifuko mingine 1.5 milioni inatarajiwa kuagizwa ili kuwaondolea vituo vya afya vya umma usumbufu wa kununua mifuko hiyo.

 “Zanzibar walianza kuagiza mifuko ya vifaa vya kujifungulia 100,000 na wameongeza tena 50,000, hivyo lengo la kuviweka hivi vifaa pamoja na kwa bei ya Sh 21,000 ni kila kituo cha Afya umma wanunue,” anafafanua Kusiluka.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa MSD, Neema Mwela, akimkabidhi  Mfuko wa vifaa vya kujifungulia Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk Amani Malima. Picha| habari24.blogspot.com.


Wadau waifagilia mifuko hiyo

Wadau wa masuala ya afya wamesema ujio wa mifuko hiyo yenye vifaa vyote vya kujifungulia utapunguza uhaba wa vifaa hospitalini na kuwawezesha akina mama wajawazito kujifungua bila vipangamizi.

 “Mifuko tunayo na tunatoa bure hapa hospitalini, imerahisisha sana kuliko ilivyokuwa mwanzo ambapo ilimlazimu mtu kununua kitu kimoja kimoja ,” anasema Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dk Amani Malima.

Baadhi ya akina mama wameiambia Nukta kuwa mifuko hiyo huenda ikapunguza gharama za vifaa vya kujifungulia kwasababu wamekuwa wakitozwa fedha kila wanapoenda kujifungua katika vituo hivyo licha ya Serikali kuagiza vitolewe bure.

“Wakati naenda kujifungua, nilinunua vifaa vyangu katika duka la dawa la jumla kwa Sh 23,500, huku katika maduka mengine ya rejareja unaweza kununua hadi Sh 37,000, hivyo ni jambo zuri kwa kupatikana kwa vifaa hivyo bure,” anasema Sakina Dotto mkazi wa Mabibo ambaye amejifungua mtoto siku za hivi karibuni katika moja ya kituo cha afya jijini Dar es Salaam.

Seti hiyo ya vifaa vya kujifungulia mtaani huuzwa kati ya Sh 50,000 hadi 60,000.

Mdau mwingine wa afya, Dk Elirehema Mfinanga anasema utaratibu huo wa Serikali utapunguza vifo vya akina mama wajawazito na vichanga muda mfupi kabla ya kujifungua.

Kwa mujibu wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), kila mwaka akina mama 8,000 nchini Tanzania hufariki wakati wa kujifungua na watoto 47,000 hufa kabla ya kuzaliwa.

UNICEF inafafanua kuwa siyo vifo vyote vya watoto vinavyotokea vinashindikana kuzuiliwa kabla ya kutokea kwake, bali vingine vinasababishwa na sababu ambazo zinaweza kuzuilika kwa wakati.

Sababu kubwa ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua ni kukosekana kwa huduma muhimu katika vituo vya afya vikiwemo vifaa vya kujifunguliwa. 


Related Post