Haya ndiyo matumizi sahihi ya mashine za kuoshea magari

March 17, 2020 9:19 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Matumizi ya mashine hizo zinazotumia pampu za maji yanatakiwa yaendane na aina ya uchafu uliopo kwenye gari. 
  • Kila kifaa cha kwenye mashine hizo kina kazi yake, kikitumika visivyo kitaleta madhara kwenye gari.

Dar es Salaam. Hakuna ambaye hafurahii mng’ao wa gari lake pale linapotoka kuoshwa. Hisia hiyo hakika hukupatia amani ya moyo hasa pale gari lako linapokuwa “limekogeka” kisawa sawa.

Hata hivyo, wakati teknolojia ya kuosha gari kwa kutumia mashine zinazosukuma maji kwa pampu maarufu kama “High Pressure Washer Machine” zikiwa zinatumika katika maeneo mbalimbali, yapo mambo ambayo unahitaji kuyafahamu kwani huenda umekuwa ukiyafanya pasipo kujua kuwa unakosea.

Kwa kuzingatia mambo hayo muhimu utaliweka gari lako salama zaidi na kulifanya lidumu muda mrefu ujao. 

Jambo la kwanza ni matumizi ya vifaa vya kuseti mwelekeo wa maji. Vifaa hivi vinajulikana kama “Nozzle” ambavyo viko vya aina tano na vinatofautishwa na rangi yaani nyeusi, nyeupe, njano, kijani na nyekundu vikiwa vimefungwa kwenye mashine.

Wakati kila rangi ikiwa na maana yake, huenda hujafahamu matumizi ya kila rangi jambo linaliweka gari yako katika hatari ya kuharibika ikiwemo kuchubuka rangi.

Kama unaosha gari epuka kutumizi nozzle nyekundu kwa sababu  inatumika kuondoa uchafu sehemu ngumu kama zege na chuma. Gari yako haiwezi kustahimili nguvu hiyo ya maji.

Matumizi sahihi ni kutumia nozzle ya njano au ya kijani kwaajili ya kuondoa matope kwenye gari lako na nozzle nyeusi itakusaidia kupaka sabuni gari lako.

Sugua gari lako mara baada ya kupaka sabuni kwa kutumia kitambaa ili kuondoa uchafu wote kisha malizia kwa maji safi ili kupata mg’ao mzuri.Hapa utatumia nozzle nyeupe ambayo inatoa maji kutakatisha gari yako.


Zinazohusiana


Kingine cha kuzingatia ni mavazi yako wakati ukiosha gari. Kwa mashine hii, epuka kufanya kazi ukiwa umevaa ndala au kanda mbili na kiatu chochote chenye kuacha miguu yako wazi.

Endapo maji yatakuwa na presha kubwa sana unaweza ukaumia kutokana na msukumowake endapo utakutana moja kwa moja na ngozi ya mguu ama eneo lolote.

Hakikisha mashine yako inasukuma maji kwa nguvu ya kawaida. Ukitumia nguvu kubwa unaweza kudhuru gari lako ikiwemo kupasuka kwa vioo na kuchubuka kwa rangi na kukuongezea gharama za kupaka nyingine.

Lengo ni kuosha gari ili liwe safi. Matumizi sahihi ya mashine hizo yakusaidie gari lako lidumu muda mrefu. Hata kama umepeleka kuosha kwa mtu, unatakiwa uwe makini.

Enable Notifications OK No thanks