10 bora kidato cha nne, sita shule za Serikali inavyofikirisha

Daniel Mwingira 0757Hrs   Machi 01, 2019 Ripoti Maalum
  • Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, Serikali haikufanikiwa kuingiza hata shule moja katika 10 bora matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. 
  • Mchuano mkali wa kuingia  kwenye 10 bora umekuwa ukishuhudiwa katika matokeo ya kidato cha sita kati ya shule za Serikali na binafsi kila upande ukijaribu kuhimili ushindani.
  • Kutokana na ushindani mkali, idadi ya shule za Serikali katika kundi la 10 bora kidato cha sita inapungua kila mwaka. 
  • Wadau wa elimu wamesema hali hiyo inatokana na tofauti ya uwekezaji, mazingira ya kusomea na kujitambua kwa wanafunzi. 

Dar es Salaam. Licha ya shule za Serikali kukimbizwa na shule binafsi katika 10 bora ya matokeo ya kidato cha nne kwa miaka saba iliyopita, zimeanza kuchukua mkondo huo pia katika matokeo ya kidato cha sita, jambo ambalo wadau wa elimu wamesema linatakiwa liangaliwe upya kuziokoa shule hizo na anguko la elimu.

Uchambuzi wa matokeo ya mitihani yanayotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kila mwaka uliofanywa na nukta.co.tz unaonyesha kuwa kwa miaka saba mfululizo yaani kuanzia 2012 hadi 2018 hakuna hata shule moja ya Serikali iliyofanikiwa kuingia 10 bora ya matokeo ya kitaifa ya mtihani wa kidato cha nne.
 
Hali hiyo imekuwa ikiibua maswali mengi juu ya elimu inayotolewa katika shule za Serikali kuwawezesha wanafunzi kujibu mtihani vizuri.
 
Wakati 10 bora ya kidato cha nne ikitawaliwa na shule binafsi, hali ni tofauti kwa matokeo ya kidato cha sita ambapo shule za Serikali na binafsi  zimekuwa zikichuana vikali kuingia katika orodha hiyo ya dhahabu.
 
Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, Serikali imefanikiwa kuingiza shule zake 17 katika 10 bora kati ya 28 zilizofanikiwa kuonja orodha hiyo ya shule bora zaidi nchini huku taasisi binafsi na mashirika ya dini zikinyang’anyana nafasi zilizosalia.
 
Mathalani kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, shule za Serikali zilitawala zaidi kwenye 10 bora ambapo kila mwaka katika kipindi hicho ziliingia shule sita na kuzipiku shule binafsi ambazo ziliingiza shule nne tu.

 Mwaka 2015 shule binafsi zilikaza kidogo na kufanikiwa kugawana nusu kwa nusu ya 10 bora kwa kuingiza shule tano kila upande, kabla ya kuangushwa tena mwaka uliofuata wa 2016 ambapo Serikali ikarudi katika nafasi ya juu na kuingiza shule sita.  
 
Lakini mambo yalibadilika mwaka 2017, shule za Serikali ziliporomoka katika kundi hilo la 10 bora na zikaingiza shule nne tu za Kisimiri, Mzumbe, Tabora Boys na Kibaha ambapo mwaka jana pia ziliporomoka zaidi hadi zikabaki shule tatu tu. 


Hali hiyo inasababishwa na nini?

Baadhi ya wadau wa masuala ya elimu wameiambia Nukta kuwa utofauti unaojitokeza katika ufaulu wa shule za Serikali katika mitihani ya kidato cha nne na sita unatokana na uwekezaji na mazingira ya kusomea ambayo yana mchango mkubwa kwa mwanafunzi kufaulu au kufeli. 

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa anasema taasisi binafsi zimefanya uwekezaji mkubwa kwenye shule za kidato cha nne kuliko kidato tano na sita, jambo linalotoa nafasi kwa shule za Serikali kutamba 10 bora japo zimeanza kupungua kutokana na ushindani uliopo.

“Kuwa na shule ya kidato cha tano na sita ni ‘so demanding’ (gharama) kutokana na kuwa wanafunzi wachache ukilinganisha na wale wa kidato cha nne, hali hiyo inapelekea wawekezaji binafsi kwenye sekta ya elimu kutowekeza huko,” amesema Dk Mkonongwa.


Zinazohusiana: 


Hali hiyo pia inatokana na ukweli kuwa, wanafunzi wa kidato cha tano na sita ni wachache ukilinganisha na ngazi za chini ambapo huwapa ahueni walimu kuwafundisha vizuri na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mitihani ya mwisho.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo ameiambia Nukta kuwa matokeo hayo ya kidato cha sita siyo ya kushangaza sana kwa sababu wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanajitambua na hupita katika mchujo mpaka kufika hatua ya juu, jambo linalowasaidia kufanya vizuri.

“Wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanajitambua na wako tayari kujifunza ukilinganisha na wale wa kidato cha nne hata wale wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanajitambua wanafanya vizuri hata kutoka shule za kata,” anasema Dk Akwilapo.

Pamoja na hayo, amesema ili mwanafunzi achangie ufaulu wa shule ni lazima vitu vitatu vitokee; jitihada za  mwanafunzi wenyewe, familia na wazazi wafanye wajibu wao na shule husika kuwekeza katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Kibaha Boys wakiwa katika moja ya mitihani ya kurudisha hadhi ya shule baada ya matokeo mabovu yaliotangazwa mwaka 2015. Picha|Mtandao.

Katika kutoa suluhisho, Dk Mkonongwa anasema inahitajika mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu ikiwemo wanafunzi kusaidiana katika masomo ili kuziwezesha shule zao kufanya vizuri na kuondoa aibu ya shule za Serikali kukosekana katika 10 bora kitaifa.  

“Inatakiwa mwanafunzi wa kidato cha tano na sita amsaidie mwanafunzi wa kidato cha nne kama shule ya wasichana ya Mtakatifu Francis inavyofanya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza anakibidhiwa kwa mwanafunzi wa kidato cha pili ili amsaidie, kwa mtindo huo utakuta wananfunzi wanasaidiana,” anasema Dk Mkonongwa.

Hata hivyo, Serikali imesema inaendela na mikakati ya kuziboresha shule zake kwa kuongeza idadi ya walimu, vifaa vya kufundishia na miundombinu msingi.

Hivi karibuni, Wizara ya Fedha na Mipango imebainisha kuwa mpaka sasa Serikali imeshatoa zaidi ya Sh42 bilioni kutekeleza mradi wa kukarabati miundombinu ya shule kongwe za sekondari 42 katika jitihada za kurudisha hadhi shule hizo ambazo zilitamba kitaaluma miaka ya nyuma.


Related Post