Filamu mpya za “The Good Liar”, “Frozen 2” zaingia sokoni rasmi

Rodgers George 0156Hrs   Novemba 22, 2019 Maoni & Uchambuzi

Tumia wikiendi hii na mwanao kutazama kisa hiki chenye nyimbo za kukonga nyoyo kilichotumia gharama ya Sh72 bilioni. Picha| Disney.


  • Ni filamu mpya zitakazoonyeshwa kwenye kumbi za sinema wiki hii.
  • Zimejaa visa vyenye mafunzo lukuki kwa watoto na wanaosaka mapenzi ya kweli. 
  • Kutana na waigizaji nguli akiwemo Ian McKellen na Helen Mirren. 

Dar es Salaam. Haijalishi umepitia mangapi ya kukatisha tamaa wiki nzima. Unatakiwa kufikiria ni nini cha kufanya ili usonge mbele na maisha yaendelee. 

Vipi kama ukiweka tai na umaridadi wako pembeni na kuvalia viwalo vya kawaida ili utimbe ndani ya kumbi za sinema kwaajili ya burudani yako ya wikiendi? 

Nafikiri ni wazo zuri. Hizi ni baadhi ya filamu zilizoingia sokoni wiki hii ambazo zitakusahaulisha machungu na msongo wa mawazo wa wiki nzima.

Frozen 2

Kama mzazi, hii siyo filamu ambayo mtoto wako anatakiwa kuikosa kwani Frozen 1 ni kati ya katuni zilizoacha alama kubwa kwenye mioyo ya watoto wakifundishwa ujasiri na uthubutu unaofaa.

Mwisho wa Frozen 1 ulionyesha kuwepo kwa maisha mazuri ya milele au kama hadithi za kufikirika zinavyoipa hali hiyo jina la “happy ever after”. Inakuwaje hali hiyo ghafla inabadilika baada ya taa zote kuzima, upepo wa kumsambaratisha Olaf unapovuma na kengere za tahadhali zinapolia?

Kimya kinatawala kiasi cha kusikia mapigo ya moyo na baada ya tafakari nini kimetokea, Mganga Mkuu (Old troll) anatangaza safari ya pili ya Elsa inayohusisha kutafuta kijiji kilichopotea. Lakini, ipo hatihati ya Elsa kujipoteza tena kwenye mazingaombwe lakini Anna yupo upande wake.


Zinazohusiana


Tumia wikiendi hii na mwanao kutazama kisa hiki chenye nyimbo za kukonga nyoyo kilichotumia gharama ya Sh72 bilioni chini ya kiongozi Jennifer Lee ambaye pia ameongoza filamu za “A Wrinkle in Time” na “Wreck it Ralph” akisaidiana na Chris Buck aliyesimamia filamu za “Tarzan” na “Pocahantas”.

The Good Liar

Roy Courtnay (Ian McKellen) ni mwizi aliyebobea. Tofauti na wezi wengine, yeye anatumia sanaa katika kazi yake. Anapokutana na Betty McLeish (Helen Mirren) akiwa na lengo la kumuibia, hisia zinatulizana hasa pale anapomuona Betty kuwa wa tofauti na mwenye dhamira ya dhati naye.

Jifunze jinsi gani mapenzi ya kweli yana nafasi ya kubadilisha hata wale wanaojidhani hawana hisia na wanaodhani mapenzi ni fikra zisizo hai.

Filamu hii iko chini ya kiongozi Bill Condon ambaye amefunika katika filamu za “Beauty and The Beast” na “Dream Girls”.

Related Post