FAO yaeleza ilivyowadhibiti nzige hatari Afrika Mashariki

May 12, 2020 7:24 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imefanikiwa kuokoa tani 720,000 za nafaka na kunusuru kaya 350,000 za wafugaji.
  • Hatua hiyo inatokana na kudhibiti kusambaa kwa nzige wa jangwani.
  • Imesema bado nzige hao wanatishia uhakika wa chakula katika nchi hizo.

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) limesema limefanikiwa kuokoa tani 720,000 za nafaka zinazotosheleza kulisha watu milioni 5 kwa mwaka mzima katika nchi 10 za ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania baada ya kudhibiti kusambaa kwa nzige wa jangwani. 

Pia kaya 350,000 za wafugaji zimenusurika na zahma ya nzige hao ambao wamekuwa wakishambulia ukanda huo wenye nchi za Djibout, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Yemen.

Ripoti ya FAO kuhusu vita dhidi ya nzige iliyotolewa Mei 11, 2020 jijini Roma Italia imeeleza kuwa wamepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya nzige wa jangwani katika eneo hilo lakini imeonya kuwa tishio la nzige hao katika uhakika wa chakula bado ni kubwa. 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema pamoja na mafanikio hayo, hatua zaidi zinahitajika ili kuzuia ukosefu wa chakula cha uhakika kwa wakulima na wafugaji. 

Nzige wa jangwani ni miongoni mwa wadudu waharibifu zaidi duniani ambapo wimbi moja linaweza kusafiri likiwa na jumla ya nzige milioni 80.

 Amesema msimu wa mvua unaoendelea siyo tu unatoa mazingira mazuri ya maisha kwa wakulima na wafugaji lakini pia ni mazingira muafaka kwa nzige hao kuendelea kuzaliana.


Zinahusiana: 


Amesisitiza kuwa FAO inaendelea kufuatilia na kudhibiti operesheni za kutokomeza nzige hao licha ya changamoto kuwa iliyotokana na mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19) pamoja na changamoto zingine.

“Mafanikio yetu ni makubwa lakini vita ni vya muda mrefu na havijaisha bado. Watu wengi zaidi wako katika hatari ya kupoteza kila kitu na kuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika miezi ijayo,” amesema Dongyu.

Pamoja na kuwa nzige hao wametokomezwa kwa kiasi kikubwa amesema wimbi lingine la watoto wao waliozaliwa wanakomaa na kuwa wakubwa ifikapo Juni  wakati ambao ni muhimu sana kwa wakulima Afrika Mashariki wakijiandaa kuvuna mazao yao.

“Tunahitaji kuongeza juhudi zaidi na kujikita siyo tu katika kudhibiti bali pia kuwasaidia wakulima na wafugaji ili wapite kipindi hiki kigumu,” amesema Dongyu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zinazofaidika na ruzuku ya dharura ya dola za Marekani 1.5 milioni (Sh3.5 bilioni) iliyotolewa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kukabiliana na nzige ambao wanatishia maisha ya watu na uhaba wa chakula katika eneo hilo.

Enable Notifications OK No thanks