Tanzania kunufaika na mabilioni ya kukabiliana na Nzige

April 2, 2020 9:54 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ruzuku ya Sh3.5 bilioni itakayotolewa katika nchi tisa za Mashariki na Pembe ya Afrika, Tanzania ikiwemo.
  • Fedha hizo zitasaidia kukabiliana na wimbi la nzige wanaovamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima. 
  • Nchi nyingine zitakazonufaika na ruzuku hiyo ni  Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. 

Dar es Salaam. Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa za Mashariki na Pembe ya Afrika zitakazofaidika na ruzuku ya dharura ya dola za Marekani 1.5 milioni uliotolewa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kukabiliana na nzige ambao wanatishia maisha ya watu na uhaba wa chakula katika eneo hilo. 

Nzige hao wa jangwani walishambulia zaidi eneo la Pembe ya Afrika mapema mwaka huu hasa Ethiopia, Kenya na Somalia na kwa sehemu Uganda, huku Sudan Kusini na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizowekwa katika tahadhari.

Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana (Aprili 1, 2020) Jijini Abidjan, Ivory Coast imeeleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya AfDB imeidhinisha ruzuku hiyo ya Sh3.5 bilioni kuzisaidia nchi tisa za ukanda huo kukabiliana na janga hilo la nzige wanaoharibu mazao ya wakulima. 

Nchi hizo ni Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda and Tanzania.

“Msaada ulioidhinishwa utapitia katika  Mamlaka ya shirikisho la Maendeleo la Pembe ya Afrika (IGAD) ambayo imepewa nguvu ya kuunganisha rasilimali kwa niaba ya Umoja wa Afrika,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Katika matumizi ya fedha hizo, IGAD itashirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) ambalo litakuwa wakala mkuu katika ruzuku hiyo ya kukabiliana na wadudu hao waharibifu. 


Zinahusiana: 


Kazi kubwa ya msaada huo itakuwa kudhibiti kuenea kwa wadudu hao, vizazi vijavyo vya nzige hao, kufanya tathmini ya athari zilizotokea na usimamizi mzuri wa kujiandaa na uelewa juu ya kukabiliana na wadudu hao. 

“Kiasi fulani cha msaada kitaelekezwa katika shudhuli za utawala,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Benki hiyo haijasema kila nchi itapata kiasi gani cha fedha.

Hata hivyo, AfDB imesema ili kukabiliana kikamilifu na nzige zinahitajika dola za Marekani 147 milioni (Sh340 bilioni).  

Hivi karibuni, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura (OCHA), Mark Lowcock alisema wimbi moja la nzige waliozingira ukubwa wa kilometa moja ambalo linajumuisha nzige milioni 40 hadi milioni 80, wanaweza kula kwa siku moja chakula ambacho kinatosheleza kulisha watu 35,000.

Nzige hao wa jangwani ambao wana urefu wa kidole cha mwanadamu huruka kwa makundi makubwa makubwa wakitafuta lishe.

Enable Notifications OK No thanks