Elimu ya malezi: Suluhu ya mauaji ya kikatili

January 28, 2022 8:31 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Jamii yatakiwa kuongeza elimu ya malezi kwa watoto.
  • Wadau wasema itasaidia kupunguza matukio ya watu kuwaua wenzao.

Dar es Salaam. Kufuatiwa kuripotiwa kwa mauaji ya watu mbalimbali hivi karibuni nchini, Serikali imetoa wito kwa jamii kuongeza elimu ya malezi kwa watoto ili kupunguza matukio hayo ambayo yanaathiri nguvukazi ya Taifa.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ametoa wito huo Januari 28, 2022 wakati akiongoza shughuli ya mazishi ya kijana Egidi Gangata aliyechomwa kisu na kijana mwenzie wa mtaani wakati kijana huyo akijaribu kupigania haki za vijana wadogo waishio mitaani jijini Dodoma.

Dk Dorothy Gwajima amesema ya elimu ya malezi kwa watoto inahitajika sana wakati huu ili kuepusha jamii kuacha watoto kukimbilia mitaani ambapo hukumbana na kadhia kadha wa kadha ambazo huwasababishia kupoteza maisha kama ilivyotokea kwa kijana Egidi na hivyo kupoteza ndoto zao.

“Tukio hili la kusikitisha la kijana Egidi, linatufundisha kuwa ndoto za watoto wengi zinapotea tangu wakiwa watoto kwa kujikuta wameingia kwenye mkondo hasi wa mfumo wa maisha hususan maisha ya mitaani na kuacha kuishi ndani ya familia ambazo mwisho wa siku huangukia kwenye madhila kama haya,” amesema Dk Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema maisha ya mtaani yanawafundisha watoto mambo mengi mabaya na ya uovu, na kwamba kama Taifa hatuwezi kuwa na jamii salama kama tukizungukwa na watoto wasio na fursa za makuzi mema.

“Matokeo yake hata pale Serikali au wadau wanapotaka kuwapa maisha mapya wanatupilia mbali fursa hiyo. Hii siyo sawa,” amesisitiza Dk Gwajima.


Soma zaidi:


Baadhi ya mauaji ambayo yameitikisa nchi hivi karibuni ni kuuwawa kwa mfabiashara wa madini Mussa Hamis anayedaiwa kuuawa na maofisa wa polisi na kuporwa Sh70 milioni mkoani Mtwara.

Mauaji mengie ni yaliyofanyika mkoani Mbeya ambapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Edward Ndonde anadaiwa kuuawa kikatili kwa kuchomwa visu na mtoto wake, Mussa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT.

Mussa anadaiwa kufanya mauaji hayo  Januari 12, 2022 nyumbani kwa baba yake mtaa wa Lumbira Kata ya Iwambi jijini Mbeya.

Afisa Maendeleo wa Jiji la Dodoma, Rebbeca Ndaki akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, amesema kilichotokea kwa kijana huyo ni matokeo ya jamii, kujitenga na watoto wao wakati wa makuzi, na kubainisha kuwa “hivyo tunaiomba jamii iwe bega kwa bega na watoto na kutaka kila mzazi kutimiza wajibu wake.”

Mwaka 2017/18 Serikali ilizindua Mpango Kazi wa Kupambana na Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWA) ambao umeelekeza kuundwa kwa Kamati za mapambano kuanzia kitongoji, mtaa, kijiji, halmashauri, mkoa na Taifa ambapo Waziri Gwajima amezitaka kamati hizo kuamka na kutekeleza wajibu wao.

Enable Notifications OK No thanks