Wanne wafariki dunia tukio la kurushiana risasi Dar

August 25, 2021 2:58 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kufyatuliwa risasi na mtu asiyejulikana.
  • Limetokea katika makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni.
  • Rais Samia atoa pole kwa wafiwa, aagiza uchunguzi kufanyika.

Dar es Salaam. Watu wanne wamefariki dunia na sita kujeruhiwa katika tukio la mauaji lililotokea leo mchana katika katika eneo la Selander jijini Dar es Salaam baada ya mtu mmoja kuwashambulia kwa risasi.

Katika tukio hilo, lililotokea mchana wa leo Agosti 25, 2021 katika makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni jirani na Ubalozi wa Ufaransa, jijini hapa, mtu huyo asiyefahamika alizua taharuki baada ya  kutekeleza mauji hayo huku akifyatua risasi hewani.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Liberatus Sabas amewaaambia wanahabari katika eneo la tukio kuwa mtu huyo aliyetekeleza kitendo hicho alidhibitiwa na baadaye kuuawa.

“Wakiwa kazini (askari) alikuja mtu mmoja akawashambulia askari hao kwa silaha ya aina ya bastola baada ya kuwashambulia na kuanguka alichukua bunduki zao mbili na kuanza kurusha risasi ovyo na kuelekea ubalozi wa Ufaransa…,” amesema kamishna huyo.

Sabas ameeleza kuwa baada ya kufika Ubalozi wa Ufaransa, mtu huyo alianza kujihami katika kibanda kilichopo katika eneo hilo huku akirusha risasi hovyo. 

Katika tukio hilo la kusikitisha, askari watatu wa Jeshi la Polisi na askari mmoja wa kampuni ya ulinzi ya SGA walipoteza maisha, huku uchunguzi ukiendelea kufanyika.

“Tuna watu sita ambao ni majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” ameeleza Sabas. 

Hadi sasa haijafahamika mtu huyo ni raia wa wapi na alikuwa na lengo gani katika shambulizi hilo lilozua taharuki kwa wakazi wa maeneo hayo ambayo yanahusisasha balozi na ofisi za biashara zikiwemo benki.

Katika baadhi ya video zinaonyesha kuwa mtu huyo aliyekuwa amevalia suruali inayoonekana kama rangi ya kaki na shati la drafti na kofia akipiga risasi hovyo.

Kifuani, mtu huyo alikuwa amening’iniza bunduki huku nyingine ameishika mkononi akitamka maneno yasiyosikika.

Mtu huyo asiyejulikana ameoneka akiwa abeba silaha na kufyatua hewani katika eneo hilo na kisha baadaye kuuwawa na askari. Picha| Mtandao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewaeleza wanahabari kuwa hadi sasa jiji hilo la kibiashara ni salama na wakazi wake hawana sababu ya kuwa na hofu. 

“Tukio limeshatokea ngoja tulifanyie kazi tuweze kujua ni nini, lakini nipongeze Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya. Kwanza kumdhibiti ili madhara mengine yasitokee na pili kuweza kuchukua zile silaha,” amesema Makalla ambaye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa mkoa.

Katika mahojiano hayo na wanahabari, Makalla amewataka watu kuchukua tahadhari endapo matukio kama hayo yanatokea kwa kuondoka eneo la tukio mara moja ili kuepuka madhara zaidi. 

Tukio hilo limetokea saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufungua kikao kazi cha viongozi wa juu wa jeshi la polisi kwa ajili kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka 2020/21 katika bwalo la polisi la Oysterbay.

Ni umbali wa takriban kilomita 2 tu kutoka eneo yaliyopotokea mauaji hayo na mkutano huo wa viongozi wa polisi.

Rais Samia atoa pole

Kufuatia tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Jeshi la Polisi na familia za askari watatu na askari mmoja wa kampuni ya ulinzi ya SGA waliopoteza maisha. 

“Nawaagiza Polisi kuchunguza kwa kina,” amesema Rais Samia.

Enable Notifications OK No thanks