BOT kununua dhahabu kwa wafanyabiashara, wachimbaji wa ndani

Mwandishi Wetu 0953Hrs   Septemba 25, 2023 Biashara
  • Madini hayo yatanunuliwa kwa Shilingi ya Tanzania.
  • Ni mkakati wa Serikali kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni nchini.

Dar es Salaam. Benki kuu ya Tanzania (BOT) imetangaza kuanza kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa ndani kwa Shilingi ya Tanzania ili kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni.

Gavana wa BOT Emanuel Tutuba, amebainisha katika taarifa yake kwa wanahabari leo Septemba 25, 2023 kuwa, benki hiyo itanunua madini hayo yanayochangia asilimia 80 ya mapato ya rasilimali madini.

“Wadau wote wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika mpango huu,” amesema Tutuba.



Mapema wiki iliyopita Tutuba alisema  kwa mwaka 2023 BOT imejipanga kukusanya tani 6 za dhahabu kutoka kwa wafanya biashara na wadau wengine wa dhahabu. kiasi hicho kinatarajiwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa madini hayo nchini.

Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022 uzalishaji wa dhahabu ulipungua kwa asilimia 4.1 kutoka kilogramu 59,392.50 mwaka 2021 hadi kilogramu 56,942.98 mwaka 2022.

Siku za hivi karibuni Serikali ilitangaza kununua dhahabu ili kukabiliana na uhaba wa Dola ya Marekani ambapo hadi  kufikia mwezi Julai, 2023 zaidi ya kilo 400 za dhahabu zilinunuliwa.

“Kati ya mwezi wa tano na wa saba tumenunua takribani kilo 400 na kitu hivi za dhahabu  tumezihifadhi Benki Kuu ambazo tukiuza tutapata dola (za marekani),” Aliyekuwa msemaji wa Serikali Gerson Msigwa aliwaambia wanahabari Agosti 26, 2023 jijini Dar es Salaam.

Huenda ununuzi wa madini ulioanza kufanywa na BOT ukafanikisha adhma ya Serikali ya kuwa na benki ya dhahabu itakayoihakikishia Tanzania uchumi imara.


Soma zaidi


Wadau wapongeza

Kennedy Mmari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Serengeti Byte inayohusika na Teknolojia na Masoko ya Dijitali, kupitia mtandao wa Twitter, amebainisha kuwa hatua hiyo ni nzuri kwa usalama wa kiuchumi wa nchi.

“Hongereni sana BOT kwa kuanza utaratibu. Ni hatua nzuri kwa usalama wa kiuchumi wa nchi yetu hasa wakati huu ambao uchumi na siasa za dunia zinaweza kurudi kuwa maltipola na kupungua nguvu kwa baadhi ya sarafu ambazo zimetawala uchumi wa dunia kwa miongo kadhaa,” amesema Mmari 

Related Post