Bomoa bomoa Mwanza: zaidi ya 30 wakosa makazi

Mariam John 0745Hrs   Aprili 23, 2024 Habari
  • Ubomoaji huo umefanyika katika kiwanja namba 585 (PB) kitalu 'KK' kilichopo Nyakato jijini Mwanza.
  • Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda awashauri watanchi kukata rufaa.

Mwanza: Zaidi ya watu 30 kutoka kaya 16 mtaa wa Temeke kata ya Nyakato jijini Mwanza wamekosa makazi mara baada ya nyumba zao  kubomolewa kufuatia amri iliyotolewa na mahakama huku wawakidai bado shauri lipo mahakamani. 

Ubomoaji huo umefanyika katika kiwanja namba 585 (PB) kitalu 'KK' kilichopo Nyakato jijini Mwanza ambacho hati miliki namba 15425 inaonyesha ni mali halali ya Taasisi ya Islamiya Education Foundation tofauti na maelezo ya wananchi wanaodai eneo hilo kuwa mali ya marehemu baba yao Makungu Sengerema. 

Wakakazi hao wamesema askari migambo kutoka Halmashauri ya jiji la Mwanza walivamia nyumba hizo na kuhamisha vitu vilivyokuwemo ndani kisha kuanza kuvunja nyumba hizo.


Soma zaidi:Bajeti ya Muungano na Mazingira yapaa kwa Sh6.3 bilioni


Mkazi wa eneo hilo, Benjamin Njiga amesema hawakupokea barua yoyote ya kubomoa nyumba hizo kwakuwa mgogoro huo ulikuwa bado mahakamani.

“Tunaiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati kwani wanadai mgogoro huo upo mezani kwao,” amesema Njiga.

Njiga anadai wamekata rufaa ya ardhi namba 68/2023 katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza ya kupinga utekelezaji wa hukumu namba 31B/2007 kuendelea ambapo rufaa hiyo imepangiwa kusikilizwa leo Aprili 23, 2024. 

Mjumbe wa Mtaa Temeke Kata ya Mhandu jijini Mwanza, Abeli Weja amesema kama uongozi wa Serikali ya Mtaa hawakushirikishwa wala kupewa taarifa hivyo kuiomba Serikali kuwasaidia wananchi hao kupata makazi na chakula katika kipindi hiki ambacho hawana makazi. 

Mkazi wa mtaa wa temeke, akiangalia vitu vyake vilivyotolewa ndani ya nyumba baada ya askari migambo kubomoa nyumba yao kwa amri ya mahakama mwishoni mwa wiki. Picha|Mariam John

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Islamiya, Abdallah Malomo amesema ubomoaji huo umetelezwa na dalali ambaye hakutaja kampuni lake kwa amri ya mahakama huku pia akidai wananchi hao wana taarifa ya kupisha eneo hilo tangu Septemba 2023. 

Akizungumza kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda mbali na kukiri kufahamu mgogoro amedai wao kama wizara baada ya kugundua kesi hiyo ipo mahakamani walishindwa kuingilia kati huku akiwashauri wananchi hao kufungua shauri la kupinga utekelezaji huo.

Related Post