Barua kwa mpenzi wangu wa zamani

August 9, 2020 1:14 pm · Jane
Share
Tweet
Copy Link

Mwaka jana mwezi kama huu kidonda kilikuwa kibichi sana, kilikuwa kinauma kila nikijigusa hata kwa bahati mbaya. Kuna muda nilijaribu kusahau kama nina kidonda, lakini hazikupita hata siku nyingi niliendelea kukumbushwa na vitu mbalimbali kwamba moyo wangu umejaa maumivu.

Kuna muda nilikuwa nalia sana. Nilikuwa najiuliza maswali mengi ambayo yalikuwa hayana majibu zaidi yalikuwa yakiongeza maumivu kwenye kidonda ambacho nilikuwa nahitaji sana kipone.

Maswali kama kwanini ulifanya ulichofanya? Jibu lako lilikuwa “hata sielewi kwanini kilitokea kilichotokea, naomba unisamehe”. Jibu hili lilizidi kunipa wakati mgumu sana.

Nilitamani sana kuondoka na kuendelea na maisha yangu. Maisha ambayo yalikuwa hayakuhusishi wewe kwa namna yoyote ile, lakini sikuweza kwa kuwa nilikuwa sijui maisha yangu yangekuwa vipi kama usikuwepo. Maisha yangu kwa muda mrefu yalikuwa ni mimi na wewe.

Tulikuwa wapenzi ambao ni marafiki walioshibana. Kuondoka kwangu kungemaanisha kumpoteza rafiki yangu na mpenzi wangu kwa wakati mmoja na sikudhani kama nilikuwa tayari kuyakabili maumivu ambayo ningeyapata pamoja na kwamba nilikuwa naumia sana kutokana na kidonda ulichokisababisha ndani ya moyo wangu.

Mahusiano yana changamoto nyingi sana lakini changamoto hizi hazishushi thamani ya mahusiano tuliyonayo. Picha|Bruno Sousa/Unsplash.

Maisha yetu yalibadilika kwa kiasi kikubwa. Uaminifu ulipotea. Maswali yalizidi. Wasiwasi ukaongezeka. Anaongea na nani? Anarudia tena? Kwani nimekosa nini? Kuna sababu gani ya kuwa mwaminifu kwa mtu anayeshindwa kuthamini uaminifu wako kwake?

Kwa upande mwingine, niliona labda hakuna haja ya kujiumiza sana kwa kushindwa kusamehe na kujaribu kulipa kisasi. Wanasema unaposamehe ni rahisi sana kusonga mbele na kuanza upya. Nikasamehe. Ukanisamehe mapungufu yangu pia, ambayo si machache. Kama binadamu yeyote sina ukamilifu.

Safari mpya ikaanza. Kwa bahati mbaya haikudumu sana. Yaliyotokea mwanzo yakaanza kujirudia. Urafiki wa ‘kuchati’na watu wengine ukaanza, kila nilipouliza jibu lilikuwa ‘ni urafiki tu, hakuna cha zaidi’. Jibu hilo kwa bahati mbaya lilimaanisha kitu kingine kwangu kutokana na historia.

Kuna wakati nilikuuliza sana ukakasirika. Kwamba kwanini sielewi na umeshanielewesha? Ndani ya nafsi yangu nikajua tunarudi tulikotoka na sikuwa tayari tena kuanza kutonesha kidonda ambacho kilianza kupona. Kwa mara ya kwanza nikawa tayari kuugulia maumivu ya kumpoteza rafiki na mpenzi ninayependa kuliko kuendelea kuumia na kuwa na maswali yasiyokuwa na majibu.

Mwanzo wa kitu chochote huwa mgumu. Iwe biashara, iwe kazi mpya, iwe penzi jipya iwe chochote kile, mwanzo huwa mgumu. Kuanza upya kuna changamoto zake nyingi sana lakini si kosa kuanza upya. Si kosa kuondoka sehemu ambayo inakupa maumivu na kukufanya ujiulize juu ya thamani yako kama binadamu. Kikubwa nilichojifunza ni kwamba hakuna mwanzo usio na mwisho. Maumivu pia yana mwisho wake.


Zinazohusiana: 


Bado ninaugulia. Na kuna wakati nakumbuka mazuri ambayo tuliyafanya kwa pamoja. Natabasamu. Kuna wakati nahuzunika. Naendelea na maisha. Siku hazigandi. Maisha lazima yasonge mbele.

Nimeandika barua si kwa nia ya kuyaweka maisha yetu ya zamani hadharani la hasha bali nimefanya hivi ili vijana wengine na watu wazima waliomo kwenye mahusiano kwa pamoka tujifunze umuhimu wa kuthamini wengine wanaotujali na kutupenda. Watu ambao hujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya mafanikio makubwa mbeleni. Watu ambao hawataki kutuona tuna huzuni katika kipindi chochote. Hawa si watu wa kuchezea mioyo yao.

Pia, nimekuandikia barua hii ya wazi kuwajulisha wapenzi wengine kuwa hofu na woga ni maadui wakubwa sana katika maisha. Uoga wa kuwa peke yako. Uoga wa kuwa ‘single’ je watu watasemaje nikiwa sipo katika mahusiano? Jamii zetu zimetuaminisha kwamba ukifika umri fulani ni lazima uwe umefanya kitu fulani au upo sehemu fulani. Lakini maisha hayapo hivyo.

Ifike mahali tuelewe kwamba kila mmoja wetu ana sababu ya kuwa hapo alipo sasa na kuamua maamuzi aliyoamua. Haujavaa viatu vyake hivyo huwezi kujua ni kwa kiasi gani viatu vinambana au vinampwaya. Hivyo usihukumu watu kwa kuwa hujui wanachokijua. Kuwa mkarimu na heshimu maamuzi ya watu wengine. Maisha ni safari na kila mtu ana njia yake. Usilazimishe mtu mwingine atumie njia yako wewe.

Mahusiano yana changamoto nyingi sana lakini changamoto hizi hazishushi thamani ya mahusiano tuliyonayo. Changamoto hizi zisitufanye tukose uaminifu kwa watu wanaotupenda. Mahusiano mengi yanavunjika kwa kukosa uaminifu. Uaminifu ni sawa na umuhimu wa mafuta kwenye gari na ili gari liende linahitaji mafuta. Ili mahusiano yadumu yanahitaji uaminifu na unapokosekana mahusiano hayawezi kwenda popote.

Nakutakia kila lenye kheri na ni matumaini yangu utapata kila hitaji la moyo wako.

Enable Notifications OK No thanks