Pesa inavyopachikwa majina mapya na vijana Tanzania

March 3, 2026 3:29 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Wengine huita, sasampa, mapene na hata njuruku.
  • Majina haya yanadhihirisha mvutano kati ya lugha ya mtaani na Kiswahili sanifu.

Dar es Salaam.  Kadiri nyakati zinavyobadilika, ndivyo baadhi ya istilahi za kiswahili huzaliwa upya na kubadilishwa majina ikichochewa na mitindo ya maisha, ushawishi wa mitandao ya kijamii,tungo za muziki, na mazingira ya kizazi husika.

Miongoni mwa istilahi hizo ni pesa ambayo miaka ya hivi karibunni imekuwa ikipachikwa majina kila kukicha na vijana wa kizazi kipya kiasi kwamba usipokuwa makini unaweza usiambulie chochote katika maongezi yao yanayohusu suala hilo.

Majina kama sasampa, kanjenje, na njuruku yamekuwa yakitumika kwa wingi mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, yakionyesha namna lugha ya Kiswahili inavyoendelea kuundwa upya na wazungumzaji wake.

Moja ya wahamasishaji wa matumizi ya neno sasampa ni mtengeneza maudhui maarufu mtandaoni anayefahamika kwa jina la Official_ankot, mwenye wafuasi wapatao 352,700 kwenye mtandao wa TikTok. 

Licha ya baadhi watu kutumia majina ya kikabila kwa kuitambuloisha fedha katika mazungumzo yao bado thamani yake huendelea kuwa ile ile. Picha| Nukta Habari|Fatuma Hussein.

Kupitia maudhui yake, amekuwa akiwahimiza wanaume kuwapa wenza wao “sasampa” ili kugharamia mahitaji yao ya muhimu, akisisitiza suala hilo huoenesha upendo kwa vitendo.

Kwa mtazamo wake, neno sasampa linabeba maana ile ile ya fedha, lakini likiwa na mvuto wa kizazi cha sasa.

Aidha, majina mengine kama shupia, hubia, faranga, na mapene  yamekuwa yakitumika mara kwa mara yakiashiria  nguvu ya lugha inayochipuka kutoka katika jamii. 

Fedha ni kila kitu kinachokubalika na watu katika kubadilishana bidhaa na huduma. Picha| Nukta Habari| Fatuma Hussein. 

Hata hivyo, mabadiliko haya yanazua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili hususan pale maneno mapya yanapokosa mchango wa moja kwa moja katika kukuza na kuimarisha lugha sanifu. Lakini swali linabaki je, kila neno jipya linapaswa kukumbatiwa?

Akizungumza katika mahojiano na Nukta Habari, mtaalam wa kiswahili kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Onno Sigara amesema kuwa ili neno litambuliwe rasmi kama neno la Kiswahili sanifu, ni lazima lisanifiwe na jopo maalumu la wataalamu wa lugha.

Kwa umuhimu wa fedha katika kuendesha shughuli za maisha ikiwemo biashara, mapenzi na hata elimu Gen Z huita sabuni ya roho. Picha| Nukta Habari| Fatuma Hussein.

Ameongeza kuwa matumizi ya lugha isiyo fasaha hayana mchango chanya katika ukuaji na uendelezaji wa Kiswahili.

“Kuna Lugha fasaha na isiyo fasaha.. mazungumzo ambayo hayana lugha fasaha hayana mchango wowote katika ukuaji wa kiswahili,” ameeleza Sigara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks