Ashtakiwa kwa kujiteka ili apate mtaji Mwanza

Mariam John 1037Hrs   Aprili 24, 2024 Habari
  • Alijiteka ili kujipatia mtaji wa Sh5 milioni kutoka kwa ndugu na marafiki zake wa karibu.
  • Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa watu kuacha tabia iliyooneshwa na kijana huyo.


Mwanza. Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu saba katika matukio mawili tofauti akiwemo Zayoga John (28) mkazi wa mtaa wa Mkuyuni wilayani Nyamagana aliyejiteka ili kujipatia mtaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, April 24, 2024, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea April 9 mwaka huu ambapo watu wafanyabiashara wawili ambao ni George Mapunda (34) na Veronica Zayoga alipotoa taarifa juu ya kutoweka kwa mfanyabiashara mwenzao huku jitihada za kumtafuta zikigonga mwamba.

“Wakati upelelezi wa tukio hilo ukiendelea, April 11 tulifanikiwa kupata taarifa kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki kuwa Zayoga kwa muda tofauti amekuwa akiwapigia ndugu zake akiwajulisha kuwa ametekwa na watekaji alimtaka kutoa kiasi cha Sh10 milioni ili wamwachie,” amesema DCP Mutafungwa

Kwa mujibu wa DCP Mutafungwa, Zayoga aliwaeleza nduzu zake kuwa kati ya fedha hizo tayari amewapatia kiasi cha Sh5 milioni kutoka kwenye akaunti yake ya benki na kuwa hawatomwachiwa iwapo hatakamilisha kiasi hicho.


Soma zaidi:Bajeti ya Wizara ya Nishati Tanzania yapungua kwa Sh1.1 trilioni


DCP Mutafungwa amesema makachero wa Jeshi la Polisi waliendelea na ufuatiliaji wa kina kuhusu tukio hilo huku wakishirikiana na taasisi nyingine za Serikali kwa kufuatilia mienendo ya tukio hilo toka alipofika kituoni hapo April 3 mwaka huu akidai kufuatiliwa na watu wasiojulikana waliokuwa wanatumia gari aina Toyota ‘land cruiser’ rangi ya fedha (silver).

“Ilipofika Aprli 13 huko  Tunduma mkoani Songwe, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo  akiendelea na shughuli zake na mwenye afya njema na baada ya mahojiano aliweka wazi kuwa aliamua kutoa taarifa za uongozo ili aweze kujipatia fedha za mtaji wa biashara yake ya kuuza mbao,”amesema DCP Mutafungwa

Hata hivyo Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu kuacha tabia iliyoonyeshwa na kijana huyu kuwa halitawafumbia macho wote watakaohusika kupotosha umma na kijana tayari ameshafanyiwa uchunguzi wa kitabibu na atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni pamoja Iddy Hamis(30), Method Charles (44), Mikweba  Irangi (53) Freddy Nyakega(46) na Salumu Hussein( 32) wanaoshtakiwa  kuiba mabomba ya maji ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa).

Mwingine ni Kelvin Boneth  ambaye anatuhumiwa kuiba gari aina ya BMW.

Related Post